HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, November 22, 2022

RUWASA KUTUMIA BILIONI 600 KUSAMBAZA MAJI VIJIJINI

 


MKURUGENZI Mkuu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi Clement Kivegalo amesema RUWASA inatarajia kutumia zaidi ya shilingi bilioni 600 kusambaza maji vijijini.

Amesema hayo baada ya kukagua mradi wa maji katika Kijiji cha Lipaya Halmashauri ya Songea mkoani Ruvuma katika ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi mbalimbali ya maji inayotekelezwa na RUWASA.

Amesema kutokana na utekelezaji mzuri wa miradi ya maji, Benki ya Dunia imeridhia kuongeza fedha Dola milioni 300 za Marekani ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi bilioni 600 zote zinakwenda kuboresha maji vijijini.

Ameahidi mradi wa maji Lipaya unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni moja unatarajia kuanza kutoa maji kabla ya Desemba 30 mwaka huu ili kuwawezesha wananchi kupata maji safi na salama.

“Shida ya maji kwa utamaduni wa Afrika wanaumia zaidi ni akinamama kwa sababu wao ndiyo wanakwenda kutafuta maji,sisi kwetu RUWASA uwepo wa Rais Mama umesababisha bajeti ya fedha kuwa kubwa hivyo kuweza kutekeleza miradi mingi ya maji ndani ya muda mfupi’’,alisisitiza Mhandisi Kivegalo.

Amempongeza Meneja wa RUWASA Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Rebman Ganshonga kwa kusimamia na kutekeleza vizuri miradi ya maji hali iliyosababisha kuongezewa bajeti ya miradi ya katika Mkoa wa Ruvuma toka bilioni saba hadi kufikia bilioni 11.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Peramiho na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.Jenista Mhagama amewapongeza RUWASA kwa juhudi wanazofanya za kuhakikisha wanamaliza kero ya maji maeneo ya vijijini likiwemo Jimbo la Peramiho.

Amesema katika historia ya Jimbo la Peramiho hii ni mara ya kwanza kwa timu nzima kutoka RUWASA makao makuu kufika kukagua utekelezaji wa miradi ya maji na ile yenye changamoto kuitafutia ufumbuzi ili wananchi wapate maji safi.

Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA akiwa na watendaji wakuu toka makao makuu yupo mkoani Ruvuma kwa ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maji na miradi yenye changamoto kuipatia ufumbuzi ili wananchi waanze kunufaika na upatikanaji wa maji safi na salama.

Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe.Pololet Mgema amesema Mkoa wa Ruvuma una kila sababu ya kumshukuru Rais kwa kuupiga mwingi kutokana na kutoa fedha za kutekeleza miradi mingi ya maendeleo ikiwemo miradi ya maji.

“Kuna watu wakisikia wananchi na viongozi wanamshukuru na kumsifia Rais wetu kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya kwa watanzania wanakasirika,sisi tunaotambua kazi yake tunasema anaupiga mwingi’’,alisema.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad