HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, November 7, 2022

LHRC, TAS WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU WALAANI MAUAJI YA MTU MWENYE UALBINO MWANZA

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Wakili Anna Henga akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 7, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia mauaji mtu mwenye Ualbino, Joseph Mathias (50) Mkazi wa Kata ya Ngula katika Kijiji cha Ngula Wilayani Kwimba Mwanza.
Mwenyekiti Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (TAS), Mussa Kabimba akifafanua jambo kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Novemba 7, 2022 kuhusiana na mauaji ya mtu mwenye Ualbino, Joseph Mathias (50) Mkazi wa Kata ya Ngula katika Kijiji cha Ngula Wilayani Kwimba Mwanza.


Na Mwandishi wetu, Michuzi Tv
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu, (LHRC) Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania wamelaani tukio la Mauaji ya mtu mwenye Ualbino, Joseph Mathias (50) Mkazi wa Kata ya Ngula katika Kijiji cha Ngula Wilayani Kwimba Mwanza.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Wakili Anna Henga wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 7, 2022 jijini Dar es Salaam. Amesema kuwa wamepokea kwa masikitiko taarifa za mauaji mtu huyo.

Akielezea tukio hilo Wakili Anna amesema kuwa Mathias alivamiwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Novemba, 2, 2022 nyumbani kwake akiwa amelala, wakamkata mkono wa kulia na hivyo kumsababishia kutokwa na damu nyingi hadi kufikia umauti.

Licha ya hayo Wakili Anna ametoa wito kwa Jeshi la polisi na serikali kuhakikisha kuwa watuhumiwa wa kesi za mauaji za watu wenye Ualbino wanakamatwa, upelelezi unafanyika kwa wakati na wanafikishwa mahakamani na kupatiwa adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wengine.

”Tunataka upelelezi wa kesi hizi upanuliwe ili wahamasishaji wa soko hili haramu la viungo vya watu wenye ualbino ikiwemo waganga wa kienyeji wachukuliwe hatua kali za kisheria.” Amesema Wakili Anna

Pia amewomba Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, kukamilisha mchakato wa upitishwaji wa Rasimu ya Mpango Mkakati wa Kitaifa Kuhusu Watu Wenye Ualbino (2020-2024).

”Ikumbukwe kwamba Rasimu hii ni zao la ushirikiano kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi mbalimbali za serikali na wadau wa asasi za kiraia uliodumu kwa takribani miaka mitatu sasa tangu mwaka 2019. Endapo Rasimu hii itapitishwa, Serikali itakua na Mpango Mkakati thabiti wa kukabiliana na madhila dhidi ya watu wenye ualbino nchini pamoja na changamoto zingine zinazowakumba.”

Aidha, ameiomba Serikali kuridhia Mkataba wa Afrika wa Haki za Watu Wenye Ulemavu uliopitishwa na Umoja wa Afrika mwaka 2018. Mkataba huo uliangazia haki za watu wenye ulemavu katika mazingira halisia ya Kiafrika ikiwemo kwa kutambua changamoto ya imani potofu zisababishazo madhila dhidi ya watu wenye ualbino.

Tume ya Haki za Bindamu na Utawala Bora na Asasi za kiraia wametoa wito kwa Serikali, Jeshi la Polisi, Tume ya Haki za Bindamu na Utawala Bora na Asasi za kiraia kurudisha upya juhudi za pamoja za kukemea vitendo hivi vya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino na mauaji, pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusu utu wa watu wenye ualbino kwani kurudi upya kwa matukio haya mfululizo kunaashiria kurudi nyuma kwa maendeleo yakliyotokana na juhudi za hapo kabla.

Pia ametoa wito kwa Taasisi na Viongozi wa Kidini na Wananchi kuwafundisha waumini wao na jamii kwa ujumla kuhusu utu wa watu wenye ualbino na kuwaonya kuachana na imani za kishirikina na tamaa zenye kudhuru binadamu wenzao na kutambua kuwa kila mmoja ana wajibu wa kuheshimu haki za mwenzake na kuzilinda.

Aidha LHRC Kinaunga mkono juhudi ambazo tayari zimeanza kufanywa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima ambaye ametoa siku saba kwa jeshi la polisi kuhakikisha wanawakamata watu hao Pia wanatoa wito kwamba mrejesho utolewe waziwazi ili kuondoa taharuki na hali ya uoga kwa kundi hili la watu wenye ualbino.

Kwa Upande wa Mwenyekiti Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (TAS), Mussa Kabimba amesema kuwa usalama wa watu na taifa kwa ujumla ni mhimu kwani huchochea watalii kuja nchini kuangalia vivutio vilivyopo lakini kama kunamatukio yanayoleta hofu hawaweze kuja nchini.

”Watalii huangalia hali ya usalama wa nchi ambayo wanaenda kufanya utalii lakini pia wawekezaji nao huangalia usalama wanapo wekeza. ” Amesema Kabimba

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad