HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 23, 2022

Kuwait, JKCI kuimarisha matibabu ya moyo kwa watoto

 Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam


22/11/2022 Shirika la Children’s Heart Charity Association la nchini Kuwait linalotoa msaada wa matibabu ya moyo limepanga kuboresha huduma za kibingwa za matibabu kwa watoto nchini kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Licha ya huduma za kibingwa shirika hilo pia limepanga kujenga jengo jipya la JKCI, kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya wa JKCI, kutoa vifaa tiba na kuiwezesha Taasisi hiyo kutoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo kwa wananchi kwa kuwafuata mahali walipo.

Watalaam wa shirika hilo walitembelea taasisi hiyo leo na kuona watoto wanaotibiwa JKCI walifarijika kuona uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali kwa ajili ya matibabu ya moyo yanayotolewa hapa nchini kwa watanzania wenye uhitaji wa huduma hizo.

Akizungumza wakati wa ugeni huo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema Shirika la Children’s Heart Charity Association limeahidi kuangalia kama kutakuwa na uwezekano wa kujenga jengo jipya la JKCI ambalo litaongeza upatikanaji wa huduma za matibabu na upasuaji wa moyo hususani kwa watoto.

“Katika kushirikiana nasi wataalam hawa wameahidi pia kutuletea vifaa tiba ambavyo vitatumika katika matibabu ya watoto ikiwa ni sehemu ya kutoa huduma rafiki kwa watoto kwani watoto wengi wanatoka katika familia zisizokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu,” alisema Dkt. Kisenge.

Dkt. Kisenge alisema Shirika hilo pia limeahidi kushirikiana na JKCI kutoa mafunzo kwa wataalam kwa kuwaleta wataalam wao hapa nchini kubadilishana uzoefu na wataalam JKCI lengo likiwa ni kuifanya taasisi hiyo kuwa bora nchini Tanzania na Afrika yote.

“Magonjwa ya moyo kwa watoto yanazidi kuongezeka hapa nchini hivyo kuongeza uhitaji wa matibabu ya magonjwa hayo kuwa kubwa, naamini ujio wa wataalam hawa kutoka nchini Kuwait utaenda kusaidia watoto wengi kufikiwa na matibabu haya ya moyo,” alisema Dkt. Kisenge.

Aidha Dkt. Kisenge alisema JKCI katika mpango mkakati wake wa kutoa huduma bora na rafiki kwa watanzania imekuwa ikiwafuata wananchi mahali walipo ili kila mwenye uhitaji na huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo aweze kuzipata jambo ambalo limeungwa mkono na watalaam hao kutoka Shirika la Children’s Heart Charity kwa kuahidi kuiwezesha JKCI ili iweze kuwafikia wananchi nchi nzima.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. William Mahalu alisema watalam wa afya kutoka nchini Kuwait wameonesha nia ya kusaidia kutibu watoto wenye magonjwa ya moyo nia ambayo sio kila mtu anaweza kujitoa kwa ajili ya watoto hao.

“Tumeainisha mahitaji tuliyonayo ikiwemo ucheleweshwaji wa watoto kufikishwa hospitali kwa ajili ya matibabu hivyo kuwaomba watusaidie vitendea kazi ambavyo zitakuwa mikoa yote hapa nchini ili tuweze kutoa huduma za utambuzi wa magonjwa haya na kuwabaini mapema watoto wenye magonjwa ya moyo,”.

“Kwa hapa tulipo sasa tupo katika nafasi nzuri ya kutoa huduma za matibabu ya moyo kwani zimepunguza matatizo kwa asilimia kubwa lakini bado tunahitaji kufanikiwa zaidi hivyo tumewaomba wasichoke kubadilishana nasi uzoefu ili tuweze kupanda zaidi katika kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo,” alisema Prof. Mahalu.

Naye Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua kwa watoto kutoka Shirika linalotoa msaada wa matibabu ya moyo kwa watoto la Children’s Heart Charity Association lililopo nchini Kuwait Faisal Al-Saiedi alisema Shirika hilo limekuwa likitoa msaada wa matibabu kwa watoto wengi duniani na sasa likaona ni vizuri kama litawafikia watoto wa Tanzania ili nao waweze kufaidika na msaada wa matibabu hayo.

“Natambua kuwa kuna watoto wengi wanaohitaji msaada wa matibabu ya moyo hapa Tanzania, na wataalam wa hapa wanafanya kazi nzuri kuwasaidia watoto hao hivyo nasi tunataka kushirikiana nao kuwasaidia watoto hao lakini pia kuwavusha hatua moja zaidi katika kutoa huduma bora za matibabu ya moyo kwa watoto wetu,” alisema Dkt. Faisal.
Wataalam wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakishirikiana na mwenzao kutoka Shirika linalotoa msaada wa matibabu ya moyo kwa watoto la Children’s Heart Charity Association lililopo nchini Kuwait Dkt. Faisal Al-Saiedi kuangalia picha ya tundu lililopo kwenye moyo kwa kutumia mashine ya Trans esophageal ECHO kwa mtoto ambaye anarudiwa upasuaji wa moyo wa kuziba tundu na valvu inayovuja walipotembelea JKCI kwa kuangalia namna ya kushirikiana na Taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam.
Madaktari bingwa wa moyo kwa watoto kutoka Shirika linalotoa msaada wa matibabu ya moyo kwa watoto la Children’s Heart Charity Association lililopo nchini Kuwait wakiangalia huduma zinazotolewa katika moja ya chumba cha kliniki ya magonjwa ya moyo kwa watoto walipotembelea JKCI kwa ajili kuangalia namna ya kushirikiana na Taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam.
Daktari bingwa wa Upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Godwin Sharau akiwaelezea aina ya upasuaji wa moyo wanaoufanya kwa watoto Madaktari bingwa wa moyo kwa watoto kutoka Shirika linalotoa msaada wa matibabu ya moyo kwa watoto la Children’s Heart Charity Association lililopo nchini Kuwait walipotembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya kuona namna ya kushirikiana na Taasisi hiyo leo Jijini Dar es Salaam.
Daktari bingwa wa usingizi kutoka Shirika linalotoa msaada wa matibabu ya moyo kwa watoto la Children’s Heart Charity Association lililopo nchini Kuwait Hesham Menshawy akielezea namna ambavyo shirika hilo litashirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto walipotembelea JKCU leo jijini Dar es Salaam. Picha na JKCI

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad