KANJI WA RAHACO NA MASSAWE WAACHIWA HURU - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, November 6, 2022

KANJI WA RAHACO NA MASSAWE WAACHIWA HURU

 

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imewaachia huru mfanyabiashara Kanji Mwinyijuma na aliyekuwa Mwanasheria wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) na Emanuel Massawe, katika kesi ya jinai iliyokuwa inahusisha Mradi wa Njia ya Reli ya Kisasa (SGR) wenye thamani ya trilioni 15.

Hakimu Mkazi Mkuu Rhoda Ngimilanga amewaachilia huru washitakiwa hao baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuwasilisha ushahidi unaotengeneza kesi kuwataka kutoa utetezi dhidi ya mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili mahakamani hapo.

“Mshtakiwa wa pili (Kanji) na mshtakiwa wa tatu (Massawe) hawana kesi ya kujibu. Hawana hatia na wameachiwa kwa mujibu wa kifungu cha 230 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai. Imeamriwa hivyo,” hakimu huyo aliamuru.

Akisoma uamuzi huo hakimu Ngamilanga ameeleza kuwa ni takwa la kisheria kwamba upande wa mashtaka wana wajibu wa kuthibitisha kesi kwa kuleta ushahidi ambao hauna mashaka unaotosha kuthibitisha shtaka fulani au ukweli na kwamba ushahidi huo utamtaka mshtakiwa kuanza kujitetea.

Amesema baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi tisa ili kuthibitisha mashitaka, mahakama imeona kuwa upande wa mashtaka haujathibitisha kesi ya awali dhidi ya washtakiwa hao wawili.

Hata hivyo, upande wa mashtaka ukiongozwa na Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Magera Ndimbo na Wakili wa Serikali, Iman Nitume, walifanikiwa kutengeneza kesi dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO, Mhandisi Benhadard Tito ambayo ushahidi wake unamtaka ajitetee.

"Kesi ya awali inathibitishwa kuwa upande wa shtaka la pili hadi la saba linalomkabili mshtakiwa wa kwanza (Tito). Mshitakiwa huyo ana kesi ya kujibu na anatakiwa kujitetea kwa mujibu wa kifungu cha 231 (1) cha CPA,” amesema.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka manane yakiwamo uhujumu uchumi, matumizi mabaya ya madaraka, kula njama na kuisababishia RAHCO hasara ya USD 527,540.

Inadaiwa, Februari 27, 2015 katika ofisi za RAHCO Wilaya ya Ilala, mshtakiwa Tito wakati akitekeleza majukumu yake, akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, alitumia vibaya nafasi yake kimakusudi kwa kununua kampuni ya Rothschild (South Africa) Proprietary Limited.

Kwa mujibu wa mwendesha mashitaka, kampuni hiyo ilinunuliwa kama mshauri wa shughuli za mradi wa kuboresha ukanda wa reli ya kati nchini Tanzania kwa njia moja bila kupata kibali cha awali cha Bodi ya Zabuni ya RAHCO, kitendo ambacho kilikuwa ni ukiukwaji wa Sheria ya Manunuzi.

Pia Tito na Massawe wanadaiwa kutumia nafasi zao vibaya kwa kusaini barua ya kuteua kampuni hiyo ya Afrika Kusini na kushindwa kuwasilisha mkataba wa huduma za ushauri kati ya kampuni hiyo na RAHCO kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uhakiki.

Pia inadaiwa kati ya Mei 20 na Juni 20, 2015 wakiwa katika ofisi za RAHCO, Tito na Masawe walitumia vibaya nafasi zao kwa kusaini mkataba wa ushauri na kushindwa kuwasilisha nakala kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Mkaguzi Mkuu wa Ndani na Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Kati ya Machi 1 na Septemba 30, 2015, katika ofisi za RAHCO, kwa vitendo vyao vya makusudi, washtakiwa wote watatu wanadaiwa kupata huduma ya ushauri kutoka kwa kampuni ya Rothschild (South Africa) Proprietary Limited, ambayo haikutolewa, na hivyo kusababisha hasara ya dola za Marekani 527,540, ambazo zilipwa mapema.

Tito pia anakabiliwa na shtaka la matumizi mabaya ya nafasi yake ambapo inadaiwa Agosti 18, 2015, alidaiwa kulikabidhi Shirika la Ujenzi la China Railway Construction Corporation ya kilomita 2 ya njia ya reli ya Standard Gauge katika Soga yenye thamani ya USD 2,312,229.39, bila idhini ya Bodi ya Zabuni ya RAHCO.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad