HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 27, 2022

Vodacom waja na huduma mpya ya kutuma na kupokea Pesa nchi za SADC

Picha ya Pamoja.Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya simu za Mkononi ya Vodacom imezindua huduma mpya ya nyongeza ya Vodacom M-Pesa inayoitwa “Dunia Kijiji, Afrika ni M-Pesa” itakayomuwezesha Mtanzania kutuma na kupokea pesa katika nchi za Ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Ukiacha nchi za Afrika Mashariki Vodacom imepanua wigo wake wa Fedha wa Kimataifa (IMT) mpaka katika nchi za Afrika Kusini, Malawi, Zambia, Zimbabwe, Lesotho, Msumbiji, Swaziland na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma huyo, waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Stargomena Tax, amesema, hatua hiyo ni kubwa katika maendeleo ya uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Amesema watanzania wanatakiwa kutambua kuwa huduma hii ni muhimu na waitumie vizuri kujikwamua kiuchumi katika ukanda huo wa SADC.

"Sisi kama serikali tunaona jambo hili lililofanywa na Vodacom ni kubwa na la umuhimu katika sekta ya fedha..... tunatambua kwamba sasa hivi nchi iko katika uchumi wa kidigitali. Uchumi wa kidigitali unafanyika kidigitali hivyo na sekta ya fedha lazima ifanye kazi ki digitali, niwaombe watanzania mahali popote walipo ndani na nje ya nchi kutambua kwamba kuna hii huduma hivyo waitumie iweze kuwasaidia kujiletea Maendeleo ya binafsi na pia kuchangia katika Maendeleo ya Taifa letu" amesema Tax

Ameongeza kuwa kupitia huduma hiyo mpya ya M-pesa diaspora pia watanufaika kwa kuleta pesa zao nchini na ba kupokea hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inatoa kipaumbele sana katika kuvutia uwekezaji na kuhakikisha mazingira ya kufanya na biashara na uwekezaji yanakuwa rahisi.

Amesema alipokuwa SADC walianzisha mfumo wa Sekta ya Fedha Jumuishi kwa nchi hizo, hivyo kilichofanywa na M-Pesa ni sehemu ya ule mpango.

“Mbali na ukuaji wa kiuchumi, lakini hatua hii imesaidia mtu mmoja mmoja kwani inarahisisha gharama za kutuma pesa na urahisi kwani pesa zinamfikia mlengwa kwa wakati huo huo ambao anadhamiria kutuma,” amesema Tax.

Aidha Tax ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa kutoa Leseni kwa Vodacom chini ya kifungu cha16 (3) ya kanuni ya ubadilishaji wa nje ya 2022 ambayo inaruhusu Watanzania na Mpesa kutuma pesa zaidi ya Afrika Mashariki na sasa kwa nchi za SADC,

Naye, Mkurugenzi wa M-Pesa Tanzania, Epimack Mbeteni amesema M-Pesa baada ya kufanya vizuri katika ukanda wa Afrika Mashariki sasa wameamua kupanua wigo huo kwa nchi za SADC.

Mbeteni amesema safari ya Vodacom M-Pesa IMT ilianza mnamo 2014 kwa kuungana na Kenya, mnamo 2019 kufanikiwa kutuma na kupokea pesa kote Afrika Mashariki na kupokea pesa kutoka nchi zaidi ya 200 duniani.

Amesema Septemba 2022, wameongeza hiki kipya ambacho kinawawezesha wateja wa Tanzania kutuma malipo kutoka M-Pesa kwenda kwa akaunti zote za Benki nchini Kenya, Uganda, na Rwanda.

Amesema malipo ya kimataifa hufanya iwezekanavyo kwa watu na biashara ndogo ndogo kukaa bila kujali jiografia.

“Mbali na masuala ya biashara lakini pia mfumo huo umerahisisha kwa wanafunzi wanaosoma nje ya nchi, wagonjwa wanaotibiwa lakini pia hata ndugu na jamaa ambao wanaweza kutumiwa pesa na kupokea,” amesema Mbeteni.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Stergomena Tax, akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma ya M-Pesa kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ambayo inawezesha kutuma na kupokea pesa katika nchi hizo, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa M-Pesa wa Vodacom, Epimack Mbeteni. akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma ya M-Pesa kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ambayo inawezesha kutuma na kupokea pesa katika nchi hizo, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wageni wakifurahia jambo wakati wa uzinduzi wa huduma ya M-Pesa kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ambayo inawezesha kutuma na kupokea pesa katika nchi hizo, jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad