HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, October 19, 2022

TANZANIA NA POLAND ZAKUBALIANA KUIMARISHA USHIRIKIANO

  

Serikali ya Tanzania na Poland zimekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano kwenye sekta mbalimbali zenye manufaa kwa nchi hizi mbili ikiwemo kilimo, elimu,  nishati, utalii, biashara na uwekezaji.

Makubaliano hayo yamefikiwa leo tarehe 18 Oktoba 2022 jijini Warsaw,  Poland wakati wa mazungumzo rasmi  yaliyofanyika kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland, Mhe. Zbigniew Rau.

Wakizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mazungumzo hayo,  Mawaziri hao  wamesema Tanzania na Poland ambazo zinaadhimisha miaka 60 ya ushirikiano, zina fursa nyingi zenye manufaa kwa pande zote mbili na kwamba  wamekubaliana kuweka mikakati madhubuti ya utekelezaji wa makubaliano hayo ikiwa ni pamoja na kuanzisha ushirikiano kwenye maeneo mapya ya ulinzi na usalama pamoja na nishati.

Akizungumza,  Mhe. Dkt. Tax amesema Poland imeandelea kuwa mshirika muhimu wa kimkakati kwa Tanzania katika kipindi chote cha miaka 60 ya ushirikiano wa kidiplomasia, na kwamba wamekubaliana kuendelea kushirikiana kwenye sekta ambazo zimekuwa na tija kubwa kwenye ushirikiano huo ikiwemo kilimo, elimu, utalii, biashara na uwekezaji.

"Katika majadiliano yetu leo, tumetathmini ushirikiano wetu katika maeneo ambayo tayari tunashirikina na Poland kama kilimo, elimu, biashara na uwekezaji na utalii. Pia tumekubaliana kuongeza maeneo ya  ushirikiano katika masuala ya nishati na ulinzi na usalama ambayo ni muhimu katika kukuza ushirikiano wetu” amesema Dkt. Tax.

Kadhalika Mhe. Dkt. Tax ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara kuja nchini kuwekeza kwani Tanzania bado inazo fursa nyingi za uwekezaji. Aidha, Mhe. Dkt. Tax ameipongeza Serikali ya Poland na Wananchi wake kwa kuendelea kuichagua Tanzania kama kituo chao muhimu cha utalii ambapo nchi hiyo ni miongoni mwa nchi tano  za juu zenye idadi kubwa ya  watalii waliotembelea nchini mwaka 2022.

“Ni imani yangu kuwa, baada ya ziara yangu hii biashara, uwekezaji, utalii na ushirikiano wa kisiasa kati ya Tanzania na Poland utaimarika zaidi. Pia kipekee nitumie fursa hii kuwashukuru wananchi wa Poland kwa upendo wao kwa Tanzania. Kwani kwa mwaka huu 2022, Poland ni miongoni mwa nchi tano zilizoshika nafasi ya juu kwa wananchi wake kutembelea nchini kwetu nawashukuru sana na karibuni tena, alisisitiza Dkt. Tax.

 Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland, Mhe. Zbigniew Rau amesema kuwa nchi yake inathamini ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na Tanzania na kwamba maeneo muhimu yaliyojadiliwa na kukubaliwa wakati wa mkutano wao yatatekelezwa na Serikali ya nchi hiyo.

“Tanzania ni mshirika muhimu sana kwa Poland na miongoni mwa nchi zinazopewa kipaumbele katika program za muda mrefu za maendeleo ikiwemo uwekezaji kwenye sekta ya kilimo,” amesema Mhe. Rau.

Pia alitumia fursa hiyo kumshukuru Mhe. Dkt. Tax kwa kukubali mwaliko wake na kuitembelea Poland ambapo alisema hatua hiyo ni muhimu katika kukuza ushirikiano kati ya nchi mbili kwani utaharakisha utekelezaji wa makubalino mbalimbali ambayo tayari yapo na mapya.

“Tumekuwa na mazungumzo yenye tija na Mhe. Waziri Dkt. Tax. Kupitia mazungumzo hayo ushirikiano wetu utaimarika zaidi. Nitumie fursa hii kumshukuru Mhe. Waziri na ujumbe wake kwa kukubali mwaliko wangu na kututembelea”, amesema Mhe. Rau.

Wakati huohuo,  Mhe. Dkt. Tax ametembelea na kuweka shada la maua kwenye kaburi la askari mashujaa wa nchi hiyo lililopo jijini Warsaw.

Mhe. Dkt. Tax yupo nchini Poland kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 17 hadi 19 Oktoba, 2022, ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi baina ya nchi hizi mbili.

Katika ziara hiyo Mhe. Waziri Tax amefuatana na Wajumbe kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Wizara ya Mambo ya  Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC),  Mamlaka ya Ukuzaji  Biashara na Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Wakala wa Taifa wa Hifadi ya Chakula (NFRA), Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akipokelewa rasmi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland, Mhe. Zbiniew Rau mara baada ya kuwasili katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje za nchi hiyo leo tarehe 18 Oktoba 2022. Akiwa Wizarani hapo, Mhe. Waziri Dkt. Tax na Mhe. Rau walikutana kwa mazungumzo rasmi pamoja na kuzungumza na waandishi wa habari. Pomioja na mambo mengine Tanzania na Poland zikubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta za kilimo, nishati, elimu, biashara na uwekezaji. Mhe. Dkt. Tax yupo nchini Poland kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 17 hadi 19 Oktoba 2022.

Mhe. Dkt. Tax akiwa katika picha ya pamoja namwenyeji wake Mhe. Rau mara baada ya kuwasili katika Ofisi za Mambo ya Nje zilizopo Warsaw nchini Poland

Mhe. Dkt. Tax na ujumbe wake akiwa kwenye mazungumzo rasmi na Mhe. Rau na ujumbe wake.
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania ulioshiriki mazungumzo kati ya Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Rau. Kulia ni balozi wa Tanzania nchini Ujerumani na Poalnd, Mhe. Abdallah Possi

Sehemu ya ujumbe wa Poland wakati wa mazungumzo hayo
Mhe. Waziri Dkt. Tax na mwenyeji wake, Mhe. Rau wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbali mbali ya ushirikiano waliyojadili na kukubaliana

Sehemu ya Ujumbe wa Tanzania akiwemo Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikisno wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme (Kushoto)

Mhe. Waziri akisindikizwa  na Naibu Mkuu wa Itifaki wa Poland, Bw. Artur Harazim kwenye kaburi la askari mashujaa wa Poland kwa ajili ya kuweka shada la maua kwa lengo la kuwaenzi na kuwakumbuka

Gwaride la heshima liloandaliwa rasmi kwa ajili ya Mhe. Dkt. Tax alipofika eneo hilo kwa ajili kuwakumbuka mashujaa wa Poland


Mhe. Dkt. Tax akisaini kitabu cha wageni alipowasili kwenye eneo hilo la makumbusho ya mashujaa

Mhe. Waziri Dkt. Tax akiwa na ujumbe wa Tanzania na Poland mara baada ya kukamilisha shughuli ya uwekaji shada la maua kuwakumbuka askari mashujaa wa Poland




 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad