MKURUGENZI UN-WOMEN ATEMBELEA DAWATI LA JINSIA NA WATOTO SITAKISHARI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, October 11, 2022

MKURUGENZI UN-WOMEN ATEMBELEA DAWATI LA JINSIA NA WATOTO SITAKISHARI

 

 


Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN-Women) Bi. Sima Sami Bahous (Kulia,) akiwasili katika Dawati la Jinsia na Watoto lililopo katika kituo cha polisi Sitakishari jijini Dar es Salaam.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN-Women) Bi. Sima Sami Bahous (Katikati) akifuraahi na baadhi ya wahamasishaji wa kupinga vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto mara baada ya kuwasili katika   Dawati la Jinsia na Watoto lililopo katika kituo cha polisi Sitakishari jijini Dar es Salaam.

 

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN- Women,) limeeleza kuwa litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha kunakuwa na usawa wa jinsia, uimara na miundombinu katika madawati ya jinsia na watoto, uelewa kwa jamii na hatua stahiki dhidi ya vitendo hivyo katikaa maeneo yote nchini.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa UN-Women Bi. Sima Sami Bahous alipotembelea Dawati la Jinsia na Watoto katika kituo cha polisi Sitakishari jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa UN –WOMEN inafurahi kuona jitihada za jeshi la polisi katika kuimarisha uhusiano na wafuasi waliojitolea katika kupambana na vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto.

‘’Ninaipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuweka juhudi za kisekta katika kukabiliana na kuzuia vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto pamoja na jeshi la polisi kwa kuweka mazingira wezeshi ya kuwasaidia waathirika wa vitendo hivyo tangu kuanzishwa kwa dawati hilo mwaka 2012.’’ Amesema.

Bi. Sima amesema UN- Women itaendelea kushiriki na kufanya kazi na vituo hivyo ili kuboresha zaidi upatikanaji wa miundombinu ya dawati la jinsia na watoto, mafunzo, maendeleo, uhamasishaji kwa Umma katika kuzuia vitendo hivyo kote nchini kwa viwango vya kimataifa.

Aidha amelitaka jeshi la polisi kuhakikisha sheria husika hasa zinazohusu unyanyasaji wa kijinsia zinatafsiriwa kupitia kanuni na viwango vya kimataifa na zinatekelezwa ipasavyo na kuwahamasisha waathirika na Umma kwa ujumla kushiriki katika shughuli za kiuchumi na maendeleo ili kupunguza hatari za ukatili kwa wanawake pamoja na kujikwamua kiuchumi.

‘’Nimepata moyo sana kwa kuona juhudi zinazofanywa na jeshi la polisi katika kutekeleza mpango mkakati wa Taifa wa kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na watoto, nimefurahi ushirikiano na uratibu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wanawake na Makundi Maalum, Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa ya Dar es Salaan na asasi za kiraia zinazoshiriki katika kukomesha vitendo vya ukatili, Kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko.’’ Amesema.

Kuhusiana na mjadala wa simu mahususi ‘Hotmail’ katika kuwafikia walionusurika na vitendo vya ukatili Bi. Sima amesema UN-Women wamedhamiria kuunga mkono mchakato huo na kuazisha simu maalum ‘Hotmail’ itakayosimamiwa na polisi katika kuhakikisha wanawake na watoto walionusurika na vitendo hivyo wanapata haki zao na kulitaka jeshi hilo kuhamasisha shughuli za maendeleo kwa waathirika hao.

Kwa upande wake Ofisa wa polisi jamii wa Mkoa wa Ilala ASP Eugene Mwampondele amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa kituo hicho mwamko wa wananchi katika kuripoti matukio ya ukatili kwa wanawake na watoto umeongezeka ukilinganisha na kipindi cha nyuma.

‘’Tangu kuanzishwa kwa dawati la jinsia na watoto hapa Sitakishari kwa ufadhili wa UN- Women tumekuwa tukipokea kesi nne hadi tano kwa siku, kwa mwezi tumekuwa tukipokea kesi 40 hadi 60 na kwa mwaka takribani kesi zipatazo 366 hupokelewa na hii ni mara tatu zaidi kabla ya kuanzishwa kwa dawati hili na mwamko wa wananchi ni mkubwa zaidi.’’ Amesema.

Aidha amesema kuwa kwa mwaka 2018 hadi 2021 jumla ya kesi 1271 ziliripotiwa na kati ya hizo kesi 54 zilishinda mahakamani na kesi 203 zinaendelea kusikilizwa huku kesi 65 zikiwa kwa mwanasheria mkuu wa Serikali (AG) na kesi nyingine kuondolewa kutokana na wahusika kushindwa kufika Mahakamani kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo wahusika kupatana katika ngazi ya jamii.

Mwampondele ameishukuru UN-Women  kwa kujenga kituo hicho ambacho kimekuwa msaada mkubwa wa kukabiliana na kukabiliana na vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto.

‘’Kituo hiki kina manufaa makubwa kwa jamii ambayo imepata mwamko wa kuripoti matukio haya na mamlaka husika kuyapatia ufumbuzi licha ya kuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo usafiri wa kuwafikia walengwa pamoja na vitendea kazi hasa kompyuta za kuhifadhi kumbukumbu.’’ Amesema.

Aidha amesema, wataendelea kushirikiana na wadau na Serikali katika kukomshaa vitendo hivyo pamoja na kushirikiana na Klabu za wanafunzi mashuleni katika kuhakikisha kila mmoja anashiriki katika mapambano ya ukatili wa kijinsia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN-Women) Bi. Sima Sami Bahous (Katikati,) akiwapata maelekezo juu ya uendeshaji wa  Dawati la Jinsia na Watoto lililopo katika kituo cha polisi Sitakishari jijini Dar es Salaam.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN-Women) Bi. Sima Sami Bahous akiwa katika picha ya pamoja na wanachama wa chama cha majaj wanawake mara baada ya kutembelea Dawati la Jinsia na Watoto lililopo katika kituo cha polisi Sitakishari jijini Dar es Salaam.

 No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad