HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, October 31, 2022

LHRC KIMETOA WITO KWA SERIKALI NA BUNGE KUTAZAMA UPYA MSWADA WA BIMA YA AFYA KWA WOTE, ULINZI WA TAARIFA

 Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Wakili Anna Henga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Oktoba 31, 2022 kuhusu uchambuzi wa miswada itakayojadiliwa na kupitishwa kuwa sheria katika mkutano wa nne (4) wa bunge la 12.

Na Avila Kakingo, Michuzi TV
KITUO Cha Haki Za Binadamu (LHRC) kimetoa wito kwa Serikali na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kutazama upya na kwa jicho la pili Miswada ya sheria itakayojadiliwa na kupitishwa katika Mkutano wa Nne wa Bunge la 12.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Wakili Anna Henga wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo. Oktoba 31, 2022. Amesema kuwa Bunge la Septemba mwaka huu kabla ya kuahirishwa Septemba 23, 2022 Miswada mipya minne ilisomwa na hatua iliyofuata ilikuwa ni kupokea maoni ya wadau juu ya Miswaada hiyo mbele ya Kamati za Kudumu za Bunge zinazohusika na Miswaada hiyo kisekta.

Akitaja miswada hiyo kuwa ni Mswada wa Bima ya Afya kwa Wote 2022, Mswada wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi 2022 na Mswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali.

"Tunaitaka serikali Pamoja na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuvitazama upya vifungu vyote vinavyompa mamlaka Waziri mwenye dhamana ya afya kutunga kanuni ili kuondoa uwezekano wa kukinzana kwa sheria mama na kanuni kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia siku za hizi karibuni kwenye baadhi ya sheria baada ya kupitishwa na bunge.

Pia Kukifuta kifungu cha 32 kinachoweka zuio la baadhi ya huduma kwani ni kinyume na haki za binadamu." Amesema Anna

Mswada wa Bima ya Afya kwa Wote 2022
Amesema mswada huu una vifungu tata na vinavyoweza sababisha uvunjifu wa haki za binadamu au kusababisha changamoto katika utekelezaji wake.

Amesema Kifungu cha 3 kinatoa tafsiri ya neno mtu asiye na uwezo lakini kwa bahati mbaya hakijadadavua vigezo vya mtu asiye na uwezo ni vipi na mtu asiye na uwezo ni nani.

“LHRC tunapendekeza na kutoa wito kwa serikali kifungu hiki kidadavuliwe na kieleze kwa kina na kiunagaubaga mtu asiye na uwezo ni nani na vigezo vya kumtambua mtu huyo”.

Pia ameomba ufafanuzi zaidi au maboresho katika vifungu mbalimbali ikiwemo Kifungu cha 13, Kifungu cha 20(1), Kifungu cha 21(2) Kifungu cha 22(2), Kifungu cha 22(3) na Kifungu cha 32.

Kwa upande wa Mswada wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi 2022, wameomba Kuondoa sharti la usajili wa lazima kwa taasisi binafsi zinazojihusisha na ukusanyaji, uchakataji na udhibiti wa taarifa binafsi kwani tayari taasisi hizo zimekwisha sajiliwa kwa mujibu wa sheria nyingine kama vile Sheria ya Makampuni na Sheria ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali na Kupunguza kiwango cha juu cha faini kutoka billion 5 mpaka million 500.

Kuhusu Mswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 3 2022
Ameiomba Serikali iachane nadhana ya usajili wa watafiti kwani iko kinyume na katiba haya ibara ya 18 inatoruhusu uhuru wa kupata na kutafuta Habari. Pia usajili wa watafiti itaminya upatikanaji wa taarifa huru za Tanzania ambazo nyingine zinahitajika na watu wanaotaka kuwekeza Tanzania. Tume ya Sayansi na Teknolojia ibaki na majukumu yake ya awali na tafiti ziwe huru.

Ikumbukwe kuwa Novemba,7 2022 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linatarajiwa kuanza vikao vyake hivyo wameomba Vifungu mbalimbali vilivyoainishwa vijadiliwe na kuboresha.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad