HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, October 25, 2022

IJA YAENDESHA MAFUNZO YA NAMNA BORA YA UENDESHAJI WA MASHAURI YA WANYAMAPORI NA MISITU

 JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tanga, Latifa Mansoor leo 24 Oktoba, 2022 amefungua mafunzo ya uendeshaji wa mashauri ya makosa dhidi ya wanyamapori ikiwepo ujangiri na makosa yanayohusiana na hayo kwa wadau wa haki jinai. Mafunzo hayo yanaendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania kwa ufadhili wa PAMS Foundation.


Mafunzo hayo ya siku tano ni mtiririko wa mafunzo mengine kama hayo yaliyofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 10 hadi 14 Oktoba 2022 kwa kundi la kwanza lililojumuisha Majaji wa Mahakama Kuu, Waendesha Mashtaka Waandamizi na Wapelelezi Waandamizi, na kufuatiwa na kundi la pili la mahakimu, waendesha mashtaka na wapelelezi kuanzia tarehe 17 hadi 21 Oktoba 2022. Hili ni kundi la tatu na mwisho ambalo linashiriki mafunzo hayo katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ambayo yanahitimishwa.

Akiongea wakati wa ufunguzi Mhe. Latifa Mansour alieleza kuwa mafunzo haya yana lengo la kuwaleta pamoja wadau wa utoaji haki jinai na kubadilishana uzoefu kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo sheria za kimataifa na kitaifa za wanyamapori na misitu ikiwemo upelelezi na uendeshaji wa mashauri ya makosa dhidi ya wanyamapori na makosa yanayohusiana na hayo.

Aidha, Mhe. Mansour aliongeza kwa kusema kuwa mafunzo haya yatawawezesha wapelelezi namna ya kufanya upelelezi kama sheria inavyotaka ili kuwezesha kesi za namna hiyo zinapofikishwa Mahakamani na waendesha mashitaka ziwe na ushahidi wa kutosha na kutokutoa mwanya kwa mtu aliyefanya kosa kukwepa kwa visingizio mbalimbali.

“Tunaamini kwamba kama Mahakama pamoja na upelelezi itashirikiana na kuhakikisha kwamba hawa watakaobainika na makosa hayo watachukuliwa hatua zipasazo na wanapata adhabu za kutosha ili iwe funzo kwa jamii yote na wale wote wanaofanya biashara hizi haramu.” Alisema Jaji huyo.

Naye mwakilishi wa PAMS Foundation, Bw. Samson Kasala alieleza kuwa Taasisi hiyo isiyo ya kiserikali inajishughulisha na masuala ya uhifadhi wa mazingira na usalama wa wanyamapori. Makao Makuu ya Taasisi hiyo yako jijini Arusha. Bw. Kassala alifafanua kwa kusema PAMS Foundation imekuwa ikisaidia katika kuwajengea uwezo wale wote walio mstari wa mbele katika kulinda ulinzi wa maliasili zetu kwa manufaa ya wananchi na vizazi vijavyo kama sheria za nchi zinavyosema.

Bw. Kasala aliendelea kwa kusema kuwa PAMS Foundation imeendelea kushirikiana na Serikali na wanafanya hivyo ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania kwenye maeneo mengi ikiwemo utalii na hasa baada ya ziara ya Utalii (Royal Tour) ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano kati ya IJA na PAMS Foundation ambayo yalisainiwa tarehe 23/06/2022 jijini Dar es Salaam kati ya Mkuu wa Chuo pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa PAMS Foundation.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Latifa Mansour akiwa anafungua mafunzo ya uendeshaji wa mashauri ya makosa dhidi ya wanyamapori yanayofanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA)

Picha mbalimbali za washiriki wa mafunzo ya uendeshaji wa mashauri ya makosa dhidi ya wanyamapori yanayofanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wakiwafuatilia hotuba ya Mgeni rasmi wakati wa ufunguzi.

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Latifa Mansour akiwa katika picha pamoja ya washiriki wa mafunzo ya uendeshaji wa mashauri ya makosa dhidi ya wanyamapori yanayofanyika  Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).  Waliokaa kutoka kulia ni Bw. Goodluck Chuwa, Makamu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, kulia zaidi ni Mhe. Awadhi Mohamed, Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Na kutoka kushoto ni Bw. Samsoni Kasala, Mkurugenzi wa Mafunzo na Tafiti PAMS Foundation (Mafunzo), kushoto zaidi ni Bw. Elisifa  Ngowi, Mkurugenzi wa Intelijensia na Oparationi  PAMS Foundation.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad