HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, October 5, 2022

CHUO CHA IAA CHATAKIWA KUONGEZA UBUNIFU

  Na. Saidina Msangi, WFM, Arusha.

Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kimetakiwa kuongeza ubunifu katika utendaji kazi wake ili kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani yatakayowezesha Chuo hicho kujiendesha kikamilifu kwa kutumia mapato hayo.

 

Maagizo hayo yametolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Jenifa Omolo, wakati wa ziara yake katika Chuo hicho ambapo alitembelea miradi inayotekelezwa pamoja na kuzungumza na Menejimenti ya Chuo hicho, jijini Arusha.

 

Bi. Omolo alisema kuwa kuongeza ubunifu kutawezesha mapato ya ndani kuongezeka kwa kuwa changamoto zinapojitokeza zitaweza kutatuliwa kwa ushirikiano na kuibua mbinu mpya za kuongeza mapato.

 

‘’Kwenye kujiendesha lazima tuwe na timu ambayo inatengeneza ubunifu, ikiwa tumekupa chuo kwa miaka mitano unapotoka unatuachia nini, hakuna mtu mwingine atakuja kukutengenezea lakini ili mfanye vizuri lazima kuimarisha utawala bora,’’ alisema Bi. Omolo.

 

Alisisitiza kuwa ili kuweza kufanikiwa katika kuongeza mapato lazima Chuo kijenge jina na kuongeza sifa kwa kuhakikisha kuwa kinazingatia ubora wa elimu inayotolewa ili kuvutia wanafunzi wengi zaidi na pia kuwa na wahitimu watakaoweza kushindana katika soko la ajira kitaifa na kimataifa.

 

Aidha, Bi. Omolo, aliitaka Menejimenti ya Chuo hicho kuimarisha ushirikiano katika taasisi hiyo na kuhakikisha kuwa utekelezaji wa miradi mbalimbali chuoni hapo unafanyika kwa ushirikiano na kutafuta mbinu za kutatua changamoto zinapojitokeza mapema kwa pamoja.

 

Alisema kuwa ameridhishwa na miradi ya ujenzi inayotekelezwa chuoni hapo na kuwasisitiza kila mmoja kuwa na taarifa za miradi hiyo ili kuwa na uelewa wa pamoja na kuhakikisha kuwa Taasisi inaweza kuendelea na shughuli zake bila kukwama.

 

Bi. Omolo aliongeza kuwa Wizara ya Fedha na Mipango itaendelea kushirikiana na Chuo hicho ili kiweze kufanikisha malengo na mipango ya muda mrefu kwa kukiwezesha kifedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kuendeleza Chuo.

 

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Cairo Mwaitete, aliishukuru Wizara ya Fedha na Mipango kwa ushirikiano na kukiwezesha Chuo hicho katika kutimiza majukumu yake pamoja na kukipatia ruzuku ya Sh. bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala, Kampasi ya Babati na kutoa kibali cha kukopa Sh. bilioni nane, kwa ajili ya ujenzi wa hosteli.

 

Akizungumzia mafanikio ha Chuo hicho, Dkt. Cairo Mwaitete, alisema kuwa Chuo kimeboresha uwezo wake wa kukusanya mapato yake ya ndani kutoka kiasi cha zaidi ya Sh. bilioni 6.4 kwa mwaka 2019/20 hadi kufikia Sh. bilioni 15.65 kwa mwaka wa fedha 2021/22.

 

‘’Chuo kimefanya jitihada za kujitangaza na kufanikisha kuongezeka kwa wanafunzi kwa miaka mitatu mfululizo kutoka wanafunzi 4,769 ambapo kufikia June 2022 Chuo kilikuwa na wanafunzi 10,342 na matarajio kwa mwaka wa masomo 2022/2023 ni kufikia wanafunzi zaidi ya 12,080’’, alisema Dkt. Cairo Mwaitete.

 

Alisisitiza kuwa Chuo hicho kitaendelea kutekeleza majukumu yake kufanikisha na kutimiza maono ya Serikali ya kuwezesha Taifa kupata nguvu kazi itakayokubalika kwenye soko la ajira kimataifa na kutoa mchango katika utatuzi wa changamoto za kijamii na kiuchumi kupitia tafiti na ushauri wa kitaalam.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Jenifa Omolo, akizungumza wakati wa kikao na Menejimenti ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), alipotembelea chuoni hapo, jijini Arusha.
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Dkt. Cairo Mwaitete, akizungumza wakati akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Jenifa Omolo, (hayumo pichani) alipotembelea chuoni hapo, jijini Arusha.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Jenifa Omolo akiongozwa na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha Dkt. Cairo Mwaitete, kutembelea miradi ya ujenzi inayoendela chuoni hapo wakati wa ziara yake katika chuo hicho, jijini Arusha.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Jenifa Omolo, akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Dk. Cairo Mwaitete (katikati) na Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango, Fedha na Miundombinu ya Baraza la Uongozi (IAA), Bw. Sylvester Rugeihyamu (kushoto), alipotembelea chuoni hapo, jijini Arusha.
Baadhi ya watumishi wa Chuo cha Uhasibu Arusha -IAA, wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Jenifa Omolo, (hayumo pichani) wakati akizungumza na Menejimenti ya Chuo hicho, jijini Arusha.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Jenifa Omolo, (wa nne kulia), akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Chuo cha Uhasibu Arusha-IAA, alipotembelea chuoni hapo, jijini Arusha.

 

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Arusha)

 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad