HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, September 25, 2022

Waziri mkuu atambua mchango wa marehebu Balozi Paul Rupia na utumishi uliotukuka siku za uhai wake.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inatambua mchango mkubwa alioutoa Mwenyekiti wa kwanza wa Benki ya DCB, Marehemu Balozi Paul Rupia katika kufanikisha uanzishwaji na maendeleo ya benki hiyo na utumishi wake uliotukuka katika maeneo mbalimbali wakati wa uhai wake.

Waziri Mkuu aliyasema hayo katika hafla ya kuuaga mwili wa marehemu Balozi Paul Rupia katika Viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam na baadae kufuatiwa na maziko yaliyofanyika katika makaburi ya Kinondoni jijini humo.

Waziri Mkuu alisema moja ya jambo ambalo halitasahaulika kwa Marehemu Balozi Paul Rupia ni mchango wake mkubwa kwa benki hiyo kwani hadi anaondoka katika Uongozi aliiacha benki hiyo ikiwa na matawi nane.

“Mheshimiwa Rais Samia amenituma kuja kumuwakilisha katika msiba huu, amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo za Balozi Rupia, hakuweza kuhudhuria kwa sababu yupo nchini Msumbiji kwa ziara ya kikazi, pia ametoa pole kwa familia na waombolezaji wote”, alisema Waziri Mkuu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya DCB, Bi. Zawadia Nanyaro alisema, benki ilipata mshtuko na masikitiko makubwa mara baada ya kupata taarifa za kifo cha Mwenyekiti huyo wa kwanza wa benki hiyo, Balozi Paul Rupia.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na viongozi wengine kiserikali na kisiasa alisema Marehemu Balozi Paul Rupia aliivusha benki katika vipindi muhimu vya hatua za ukuaji wa benki tokea mchakato wa uanzishwaji wa Benki ya DCB mnamo Mwaka 2000 hadi inaanzishwa rasmi mwaka 2002.

“kwa kipindi cha miaka 15 cha uongozi wake, marehemu Balozi Rupia alifanikisha hatua mbalimbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na benki kuorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), na pia kubadilika kwa benki kutoka kuwa Benki ya Watu wa Dar es Salaam na kuwa Benki ya Biashara ya DCB.

“Wakati DCB ikiendelea kusherehekea miaka 20 tokea ilipoanzishwa, mchango wa marehemu Balozi Paul Rupia hautaweza kusahaulika, kwani aliiongoza benki kwa weledi mkubwa na alihakikisha benki inakuwa kimtaji na kuongeza matawi kutoka moja hadi nane alipostaafu”, aliongeza Bi. Zawadia.

Aidha mwenyekiti hiyo alisema, Marehemu Balozi Rupia hata baada ya kustaafu kwake aliendelea kushirikishana na DCB akiwa pia mmoja wa wanahisa waanzilishi wa benki hiyo na wakati benki ikiadhimisha miaka 20 Mwezi Mei, licha ya kukabiliwa na matatizo ya kiafya, Balozi Rupia alikubali kushiriki sherehe hizo kwa njia ya video.

“Tutaendelea kuenzi yale yote mema aliyoyafanya katika benki yetu, nasi tunaungana na waombolezaji wengine kuwapa pole wanafamilia na viongozi wote kwa msiba huu uliotufikia na tunaendelea kuiombea roho ya marehemu ipumzike kwa amani”, alisema.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu Balozi Paul Rupia katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam kabla ya maziko yaliyofanyika katika Makaburi ya Kinondoni jijini humo. Balozi Rupia alikuwa mwenyekiti wa kwanza wa Benki ya DCB na kuingoza kwa kipindi cha miaka 15 alifariki Dunia Septemba 16 mwaka huu nchini Afrika Kusini.

Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Biashara ya DCB , Bi. Zawadia Nanyaro (kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Godfrey Ndalahwa, na Mwenyekiti wa Bodi Mstaafu wa DCB, Prof. Msambichana wakitoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu Balozi Paul Rupia katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam kabla ya maziko yaliyofanyika katika Makaburi ya Kinondoni jijini humo. Balozi Rupia alikuwa mwenyekiti wa kwanza wa Benki ya DCB na kuingoza kwa kipindi cha miaka 15 alifariki Dunia Septemba 16 mwaka huu nchini Afrika Kusini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB , Bwana Godfrey Ndalahwa (kushoto), akizungumza katika hafla ya kuuaga mwili wa marehemu Balozi Paul Rupia katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam kabla ya mazishi yaliyofanyika katika Makaburi ya Kinondoni jijini humo. Balozi Rupia alikuwa mwenyekiti wa kwanza wa Benki ya DCB na kuingoza kwa kipindi cha miaka 15 alifariki Dunia Septemba 16 mwaka huu nchini Afrika Kusini. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya DCB, Bi. Zawadia Nanyaro.

 Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Biashara ya DCB , Bi. Zawadia Nanyaro (kushoto), akitoa salamu za pole kwa niaba ya bodi na menejimenti ya DCB katika hafla ya kuuaga mwili wa marehemu Balozi Paul Rupia katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam, kabla ya maziko yaliyofanyika katika Makaburi ya Kinondoni jijini humo. Balozi Rupia alikuwa mwenyekiti wa kwanza wa Benki ya DCB na kuingoza kwa kipindi cha miaka 15 alifariki Dunia Septemba 16 mwaka huu nchini Afrika Kusini.

Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa Benki ya Biashara ya DCB, Regina Mduma (kulia) na Ofisa Masoko, Agnes Ntabaye (kushoto) wakiweka shada la maua kwenye kaburi alimozikwa Marehemu Balozi Paul Rupia wakati wa maziko yaliyofanyika katika makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam. Balozi Rupia alikuwa mwenyekiti wa kwanza wa Benki ya DCB na kuingoza kwa kipindi cha miaka 15 alifariki Dunia Septemba 16 mwaka huu nchini Afrika Kusini.
 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad