HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, September 9, 2022

WADAU WA ELIMU WAWEKA BAYANA UMUHIMU WA MAKTABA MAADHIMISHO SIKU YA USOMAJI

 Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Room to Read Tanzania, Bw. Juvenalius Kuruletera akizugumza kwenye Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Usomaji Duniani lililofanyika jijini Dar es Salaam na kushirikisha baadhi ya wadau wa elimu nchini.

Mkurugenzi Idara ya Ubunifu na Uandaaji wa Vifaa vya Kielimu kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE), Bw. Fixon Mtelesi akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, kwenye Maadhimisho ya Siku ya Usomaji Duniani yalioratibiwa na Shirika la Room to Read Tanzania.
Baadhi ya washiriki wa Kongamano hilo wakishiriki katika mjadala.
Mkufunzi Mwandamizi wa Usomaji na Maktaba, Room to Read, Bi. Eva Sanga akizungumza kwenye Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Usomaji Duniani lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya washiriki kwenye hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Usomaji Duniani yalioratibiwa na Shirika la Room to Read Tanzania.

Na Mwandishi Wetu, Dar
WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema itaendelea kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji ikiwemo kukuza stadi za usomaji kwa wanafunzi hasa wa shule za msingi ili kuwaongezea uelewa na uwezo wa kuyamudu masomo yao.

Kauli hiyo imetolewa na jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Idara ya Ubunifu na Uandaaji wa Vifaa vya Kielimu kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) , Bw. Fixon Mtelesi alipozungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, kwenye Maadhimisho ya Siku ya Usomaji Duniani yalioratibiwa na Shirika la Room to Read Tanzania.

Akizungumza Bw. Mtelesi alisema kumjengea mwanafunzi utamaduni wa kupenda kujisomea kunakuza stadi na kumuongezea uelewa wa kumudu masomo yake mengine na kuleta mabadiliko chanya katika jamii na taifa kwa ujumla.

Alisema TIE inaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kuboresha elimu kwa ngazi zote, hasa uboreshaji wa miundombinu ya elimu ikiwemo madarasa, vyoo na ukarabati wa shule mbalimbali; hivyo kuiomba pia kuangalia suala zima la uanzishwaji wa maktaba kwa shule za msingi kwa kuwa ni kitovu cha maarifa katika ujifunzaji.

"..Kama tunavyofahamu kuwa kujenga utamaduni usomaji imekuwa mada na lengo la muda mrefu la nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania. Hata hivyo licha ya jitihada hizo zinazochuliwa na mataifa katika kukuza usomaji, tafiti zinaonesha kuwa bado kuna idadi kubwa ya watu duniani wasiojua kusoma vizuri na wasiokuwa na tabia ya usomaji," alisema Bw. Mtelezi katika kongamano hilo lililobeba kauli mbiu; 'Uboreshaji wa Mazingira ya Usomaji na Ujifunzaji'.

Naye, Mkurugenzi wa Mradi wa Usomaji na Maktaba Room to Read Tanzania, Bw. Joachim Kahwa akizungumza katika kongamano hilo, alisema wanaamini kuwa maktaba ndio sehemu pekee ambayo mtoto huweza kupata fursa ya kuendeleza stadi za kusoma na kujenga tabia ya usomaji.

Room to Read humsaidia katika kujenga msingi bora wa kumudu stadi za kusoma na kuandika katika darasa la kwanza na la pili ili kujua kusoma kwa wakati, kisha, kutumia stadi hizo kujisomea maktaba ili kujenga tabia ya usomaji ili kujifunza zaidi.

Hata hivyo, alibainisha kuwa mtoto mwenye tabia ya usomaji hupenda kusoma kwa hiari mara kwa mara na hufurahia usomaji. ili kumvutia mtoto kujenga tabia ya usomaji Room to Read tunahamasisha uwepo wa maktaba zenye vitabu vya hadithi vilivyoandaliwa vizuri, vyenye kuvutia, vilivyopangiliwa kwa ngazi kulingana na uwezo wa usomaji wa watoto na mazingira rafiki kwa mtoto," alisisitiza, Bw. Kahwa.

Maadhimiso ya Siku ya Usomaji Duniani hufanyika kila mwaka Septemba 8 ikiwa ni matokeo ya tamko la Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (UNESCO) lililotolewa tarehe 26 Oktoba 1966.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad