HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, September 29, 2022

DC MANGOSONGO AZINDUA MIONGOZO YA ELIMU HALMASHAURI YA WILAYA MBINGA, AKEMEA WALIMU WA KIUME KUWA NA MAHUSIANO YA KINGONO NA WANAFUNZI

Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Aziza Mangosongo, akionyesha miongozo ya usimamizi na uendeshaji wa elimu wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa miongozi hiyo uliofanyika katika viwanja vya Halmashauri ya wilaya Mbinga,kulia Mwenyekiti wa Halmashauri Desderius Haule na kushoto Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Juma Haji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Mbinga Juma Haji kushoto, akipokea moja kati ya miongozi mitatu ya usimamizi na uendeshaji wa elimu kutoka kwa Mkuu wa wilaya ya Mbinga Aziza Mangosongo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma Desderius Haule akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa miongozo na uendeshaji wa elimu katika Halmashauri hiyo uliozinduliwa na Mkuu wa wilaya ya Mbinga Azazi Mangosongo katikati katika viwanja vya Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji eneo la Kihamili wilayani Mbinga,kushoto Mkurugenzi wa Halmashauri Juma Haji.
Afisa elimu Sekondari wa Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma Peter Ntalamka kulia,akipokea mwongozo wa usimamizi na uendeshaji wa elimu kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Juma Haji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma Juma Haji kushoto,akimkabidhi Afisa elimu msingi wa Halmashauri hiyo Samwel Komba miongozo ya usimamizi na uendeshaji wa elimu wakati wa uzinduzi wa wa miongozo ya usimamizi na uendeshaji wa elimu katika Halmashauri hiyo. 
 
Na Muhidin Amri, Mbinga

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Aziza Mangosongo,amezindua miongozo ya usimamizi na uendeshaji wa elimu huku akikemea tabia ya baadhi ya walimu wa kiume kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wao.

Mangosongo alisema,tabia hiyo imechangia kuporomoka kwa maadili kwani baadhi ya walimu wanatumia nafasi zao kuwarubuni wanafunzi  na kufanya nao mapenzi,hivyo kusababisha wanafunzi kufanya vibaya  katika masomo yao.

Mangosongo ametoa kauli hiyo,alipokuwa akizungunza na walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari na viongozi wa Halmashauri ya wilaya Mbinga kwenye uzinduzi wa miongozo hiyo katika Halmashauri  ya wilaya Mbinga.

“kuna mwalimu mmoja sitaki kutaja jina lake na shule anayofundisha, amempa mimba mwanafunzi wake aliyetakiwa kujiandaa na mitihani ya kidato cha nne mwaka huu,lakini jambo la kusikitisha hata walimu wenzake hawataki kumtaja”alisema Mangosongo.

Alisema,Halmashauri ya wilaya Mbinga hakuna sababu ya kutofanya vizuri katika  suala la kitaaluma kutokana na kuwepo kwa mazingira mazuri ya kujifunzia na kufundishia ikilinganisha na Halmashauri nyingine katika mkoa wa Ruvuma.

Mangosongo alieleza kuwa,miongozo hiyo hususani wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji ngazi ya elimu ya msingi ni mikakati ya kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji,usimamizi na ufuatiliaji na ushiriki wa wadau ili kufanikisha utekelezaji huo.

Hivyo,amewataka walimu wa shule za  msingi na sekondari kutumia miongozo ya usimamizi na uendeshaji  iliyotolewa na serikali kufanya tathimini ya mara kwa mara ya hali ya elimu ili kurudisha heshima ya wilaya ya Mbinga kitaaluma.

Amewaagiza,kuanza kuwafuatilia na kuwaandikisha watoto wote wenye umri wa kuanza elimu ya awali na shule ya msingi ili waanze masomo ifikapo mwezi Januari 2023 na kusimamia watoto watakaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wawe wameripoti mara shule zitakapofunguliwa.

Pia,amewahimiza walimu kuwa wabunifu, kujifunza ikiwamo kusoma vitabu mara kwa mara ili kupata maarifa na mbinu mpya zitakazowasaidia kufanya vizuri katika kazi zao za kila siku.

Miongozo iliyozinduliwa katika Halmashauri hiyo,ni mkakati wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji ngazi ya elimu ya msingi,uteuzi wa viongozi wa elimu katika mamlaka za serikali za mitaa na changamoto katika  uboreshaji wa elimu ya msingi na sekondari.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Juma Haji alisema,wamejipanga  kufanya vizuri katika sekta ya elimu ili watoto wote waliopo  kwenye shule za msingi na sekondari wapate elimu bora na hatimaye waweze kufanya vizuri katika  masomo yao.

Naye Afisa elimu sekondari wa Halmashauri hiyo Peter Ntalamka alisema, Halmashauri ya wilaya Mbinga ina shule za msingi 167 kati ya hizo shule za serikali ni 164, na shule binafsi 3  na kwa upande wa sekondari kuna shule 47 ambapo za serikali 31 na binafsi 16.

Alieleza kuwa, kwa  shule za msingi kuna wanafunzi 67,078 na sekondari 14,652 na mahitaji ya walimu wa shule za msingi 1,936 waliopo 938 pungufu 998 na sekondari mahitaji ya walimu 716 waliopo 535 na pungufu walimu 181.

Aidha alisema, mwaka 2022 uandikishaji kwa wanafunzi wa shule za msingi ulivuka lengo kwa asilimia 133 kwa darasa la awali na asilimia 123 kwa darasa la kwanza.

Kwa mujibu wa Afisa elimu huyo,kwa shule za sekondari uandikishaji ulikuwa asilimia 94 kwa kidato cha kwanza, na asilimia 76 kwa kidato cha tano,hata hivyo juhudi za kuhakikisha wanafunzi wote wanaandikishwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad