Waziri Ummy: Tafuteni eneo kubwa la matibabu ya moyo - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 4, 2022

Waziri Ummy: Tafuteni eneo kubwa la matibabu ya moyoNa Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
WAZIRI wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu ameiagiza Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kutafuta eneo kubwa litakalotosha kuwaruhusu wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji kupata mazingira rafiki ya kufanyia mazoezi baada ya matibabu.

Waziri amependekeza eneo hilo litafutwe ndani ya eneo la Hospitali ya Mlonganzila kwa kuwa mahali ilipo Taasisi hiyo pamejaa kwa sasa.

Mhe. Ummy Mwalimu alitoa mapendekezo hayo jana alipozindua bodi ya wadhamini ya JKCI katika ukumbi wake wa mikutano jijini Dar es Salaam.

Mhe. Ummy alisema mahali ilipo JKCI kwasasa si rafiki kwa wagonjwa kwani pamezungukwa na majengo mengi hivyo kubakiwa na nafasi finyu inayowanyima wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa moyo uhuru wa kufanya mazoezi.

Wajumbe hao pia wamepewa jukumu la kuhakikisha wataalamu mabingwa wa magonjwa ya moyo kutoka JKCI wanawajengea uwezo na kuwasimamia wataalam wa afya kutoka hospitali za kanda na wilaya kwa kuanza na hospitali ya kanda ya Chato, hospitali ya rufaa ya kanda ya Mtwara na hospitali ya kanda ya mwalimu Nyerere Memorial Hospital iliyopo mkoani Mara.

“Wagonjwa wengi wamekuwa wakifuata huduma hasa za vipimo JKCI lakini kama wataalam waliopo katika hospitali za kanda na rufaa watajengewa uwezo wa kutoa huduma hizi itapunguza msongamano wa wagonjwa wanaofika hapa kwaajili ya matibabu”, alisema Mhe. Ummy.

Mhe. Ummy alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo magonjwa ya moyo ambapo takwimu zinaonesha wagonjwa wa nje na wale wanaolazwa inaongezeka hii ni kwa sababu ya kuboresha huduma za matibabu hapa nchini hivyo kuwawezesha wananchi kufika katika vituo vya afya kupata huduma lakini pia ongezeko hili linaweza kusababishwa na ukosefu wa elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa hayo.

“Moja ya jukumu la Bodi hii mpya kwa kushirikiana na menejimenti ya Taasisi hii ni kuhakikisha mnaandaa mpango mkakati wa kuweza kuwafikia watanzania wengi zaidi ili waweze kupata elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa haya yasiyoambukiza kwani mtu anaweza kuyaepuka kama atafuata mtindo bora wa maisha na hivyo kupunguza ongezeko la wagonjwa ya moyo”,.

“Bodi hii pia iandae mpango mkakati ambao utawawezesha wataalam mabingwa wa magonjwa ya moyo kuwafikia watanzania wengi kupitia upimaji wa kuwafuata wananchi mahali walipo (outreach program) kwa kufanya hivi kutasaidia wagonjwa kugundulika mapema na hivyo kupata matibabu kwa wakati kuliko kusubiri hadi tatizo limekuwa kubwa”, alisema Mhe. Ummy.

Aidha Waziri huyo wa Afya aliwashukuru na kuwapongeza wajumbe wa bodi mpya ambao wamekubali kupokea uamuzi wake wa kuwateua kwani wangeweza kusema hapana kutokana na majukumu waliyonayo lakini wakaona umuhimu wa Taasisi hiyo na kukubali imani ambayo amewapa kuwa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini.

“Naishukuru Bodi ambayo imemaliza muda wake kwa kufanya kazi kubwa na nzuri ambayo tumeona matokeo ya kazi iliyofanyika katika utoaji wa huduma za afya kwa watanzania wanaohitaji huduma za matibabu ya moyo. Ninaamini Bodi hii mpya nayo itakuwa mstari wa mbele kuiwezesha taasisi hii kutekeleza majukumu yake kikamilifu hivyo kufikia malengo ya kuanzishwa kwake”, alisema Waziri Ummy.

Waziri Ummy alisema kwakuwa JKCI imeweza kupunguza rufaa za kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi sasa ni wakati wa Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Bodi mpya ya wadhamini kuona namna ambavyo fedha iliyokuwa imetengwa kwaajili ya kupeleka wagonjwa nje ya nchi inaombwa Hazina ili fedha hizo ziweze kuwasaidia wagonjwa ambao hawana uwezo wa kugharamia matibabu.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shakalaghe aliwapongeza wafanyakazi wa JKCI kwa kazi nzuri wanayoifanya tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 2016 hadi sasa bila kuisahau bodi ambayo imemaliza muda wake kwani matokeo mazuri ya JKCI ni kwasababu ya ushirikiano mzuri uliofanywa na Bodi hiyo.

“Nawapongeza wataalam wa JKCI kwasababu mafanikio haya yaliyosemwa hapa ya kuokoa maisha ya wagonjwa bila ya watendaji hawa nadhani yasingekuwepo, mmekuwa chachu na mfano mzuri katika jamii yetu”,.

“Majukumu makubwa ya JKCI ni pamoja na kutoa elimu, utafiti na matibabu ya moyo ambapo leo hii tumeona matokeo makubwa katika sehemu ya matibabu hili halipingiki lakini eneo la elimu na utafiti tungependa kuona matokeo zaidi hivyo kupunguza idadi ya wagonjwa ambayo tumeona kila mwaka inaongezeka”, alisema Dkt. Shakalaghe.

Akisoma taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi alisema tangu kuanzishwa kwa Taasisi hiyo mwaka 2016 hadi sasa aina 30 za upasuaji wa moyo zinafanyika hivyo kupunguza wagonjwa wanaokwenda nje ya nchi kwaajili ya matibabu ya moyo.

“Taasisi imekuwa na mafanikio makubwa kwani tumeweza kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 51 baada ya kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya moyo”, alisema Prof. Janabi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof.William Mahalu aliwashukuru wajumbe wa Bodi ya awali kwa ushirikikano mkubwa waliouonyesha hivyo kufanya kazi ya uendeshaji wa Bodi hiyo kuwa nyepesi.

Prof. Mahalu ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu alisema moja ya mikakati waliyojiwekea na Bodi iliyomaliza muda wake ilikuwa ni kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi kutibiwa magonjwa ya moyo ambapo lengo hilo lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa.

“Leo hii tunajivunia kuwa sehemu ya kupunguza wagonjwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu ya moyo, kama tulivyosikia idadi ya wagonjwa wanaokwenda nje ya nchi imepungua na kufikia asilimia tano (5) ninaamini miaka michache ijayo hakutakuwa na wagonjwa watakaokwenda kutibiwa magonjwa haya nje ya nchi”, alisema Prof. Mahalu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad