HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, August 29, 2022

TCRA YATOA TAHADHALI KWA MAUDHUI YASIYOENDANA NA MAADILI YA KITANZANIA

 


Kwa mujibu wa kifungu cha 27(3)(a) cha Sheria iliyoanzisha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Kamati ya Maudhui imepewa jukumu la kusimamia maudhui yote yanayorushwa na vituo vya Utangazaji pamoja na mitandao ya ki-elektroniki.


Siku za karibuni, kumekuwa na taarifa inayosambazwa na baadhi ya watumiaji wa mitandao ya Kijamii ikitahadharisha juu ya uwepo wa maudhui ya televisheni kwenye vipindi vya watoto yaliyo kinyume na Sheria, Kanuni za Utangazaji, maadili na miiko ya utangazaji nchini.


Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ingependa kuuhakikishia umma kuwa maudhui yote yanayorushwa na vyombo vya Utangazaji hapa nchini hufanyiwa uhakiki kwanza na pia kufuatiliwa na vifaa maalumu (content monitoring equipment) vinavyofuatilia matangazo yote ili kujiridhisha kuwa yanazingatia Sheria, Kanuni, Maadili na Utamaduni wa Mtanzania.


Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejiridhisha kuwa hakuna chombo cha Utangazaji kilichorusha maudhui hayo yasiyofaa kwa watoto. Hata hivyo, Kamati ya Maudhui inavikumbusha vyombo vyote vya Utangazaji kuendelea kuzingatia matakwa ya Sheria, Kanuni na Masharti ya Leseni ya Utangazaji kwa kuhakikisha vituo vyao haviendi kinyume na maadili ya Ki-Tanzania.


Aidha, Kamati ya Maudhui inaendelea kusisitiza kuwa wajibu wa kuwalinda Watoto kutokana na maudhui yasiyofaa hasa kwenye mitandao ya kijamii ni wa kwetu sote ikianzia kwa Wazazi, Walezi na Mashuleni ambapo Watoto wetu hutumia muda mwingi huko wakiwa masomoni.


Pia Kamati ya Maudhui inaiasa jamii kutosambaza katika mitandao ya kijamii jumbe zinazoleta taharuki, upotoshaji na hofu katika jamii. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wale wote watakaobainika kusambaza jumbe hizo. TCRA ikishirikiana na Jeshi la Polisi inafuatilia kwa ukaribu maudhui yanayowekwa kwenye mitandaoni; kwa yeyote atakayebainika kuweka habari za upotoshaji mitandaoni, hatua kali za kisheria zitachukuliwa.


Imetolewa na:
Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania,
Jengo la Mawasiliano,
Kitalu Na. 20 Barabara ya Sam Nujoma,
S. L. P 474,
14414 DAR ES SALAAM

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad