HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, August 26, 2022

NSSF YAUNGA MKONO MCHANGO WA DIASPORA KATIKA KUKUZA UCHUMI WA NCHI

 


*Yatoa shilingi milioni 50 kufadhili mfumo wa taarifa za Diaspora

Na MWANDISHI WETU

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeunga mkono mchango mkubwa unaotolewa na Watanzania Wanaoishi Nje ya Nchi (DIASPORA), katika kujenga uchumi wa Taifa kwa kutoa Shilingi milioni 50 ili kufadhili matengenezo ya mfumo wa kidigitali wa utunzaji wa taarifa za Diaspora.

Hayo yalisemwa  jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Uthaminishaji, Takwimu na Usimamizi wa Hadhari wa NSSF, Ibrahim Maftah, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufadhili matengenezo ya mfumo huo.

“NSSF tunatambua na kuthamini mchango wa Diaspora katika kujenga uchumi wa Taifa na wakati wote Mfuko umekuwa moja ya wadau muhimu katika shughuli za matukio mbalimbali za Diaspora,” alisema.

Maftah alisema ushiriki wa NSSF katika kufanikisha kuanzishwa kwa mfumo huo ni kuunga mkono Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha Diaspora wanachangia kikamilifu maendeleo ya Taifa.

Alisema mfumo huo utakapoanza utatoa utatibu wa kazi mbalimbali za Diaspora kufanyika kwa mtandao jambo ambalo ni fursa kwa NSSF kutangaza fursa mbalimbali za miradi ya uwekezaji kama vile nyumba, viwanja, hoteli na shughuli nyingine zinazotolewa na Mfuko.

Naye, Mhe. Balozi James Bwana ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhe. Balozi Joseph Sokoine, aliishukuru Bodi ya NSSF kwa kukubali kufadhili matengenezo ya mfumo huo, ambao utakapokamilika utawatambua, kuwasajili na kutunza taarifa za Diaspora wa Tanzania waliotapakaa duniani kote kupata huduma muhimu.

Mhe. Balozi Bwana alisema mfumo huo utakuwa chachu ya ushiriki wa Diaspora wa Kitanzania kidigitali katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo biashara, uchumi na uwekezaji licha ya umbali waliopo.

“Kwa niaba ya uongozi wa Wizara na Serikali kwa ujumla natoa shukrani za dhati kwa uongozi mzima wa NSSF wa kukubali kushirikiana nasi katika jambo hili muhimu kwa kutoa Shilingi milioni 50,” alisema.

Balozi Bwana alisema NSSF ni wadau muhimu wa kutoa huduma kwa Diaspora ambapo pamoja na huduma hizo kupitia dirisha la uwekezaji, Wizara imekuwa na mazungumzo na NSSF ili kuangalia namna wanavyoweza kushirikiana zaidi katika eneo la Uwekezaji kupitia uendelezaji wa viwanja vilivyopo katika Balozi za Tanzania nje ya nchi.

Alisema mfumo huo pia utawezesha kutekeleza kwa vitendo azma ya Serikali kuhamasisha taasisi mbalimbali nchini kuwekeza katika digitali ili kuongeza tija ya matumizi sahihi ya muda wanaohudumiwa na kupunguza urasimu, pamoja na kuiwezesha Wizara hiyo kwenda sambamba na dunia katika teknolojia.

Mwakilishi wa Kitengo cha Diaspora Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Semeni Nandonde, alisema kupitia mfumo huo Serikali itaweza kufahamu idadi ya Diaspora, ujuzi walionao, elimu pamoja na kupata huduma maalum ambazo zitaandaliwa kwa ajili yao kama vile huduma za hifadhi ya jamii, benki, bima ya afya, uwekezaji, biashara na masoko.


Mkurugenzi wa Uthaminishaji, Takwimu na Usimamizi wa Hadhari wa NSSF, Ibrahim Maftah (kushoto) akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba (hayupo pichani) wakibadilishana hati jijini Dar es Salaam, jana na Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana, baada ya kutiliana saini makubaliano ya ufadhili wa matengenezo ya mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora.










 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad