HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, July 18, 2022

RITA YAKUTANA NA WADAU KUJADILI MABORESHO YA UTOAJI HUDUMA

 
 
 
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Mary Makondo akizungumza wakati akifungua mkutano ulioikutanisha RITA na wadau wanaofanya nao kazi kwa karibu na kuipongeza wakala hiyo kwa jithada za kufanikikisha kusajili na kutoa vyeti kwa watoto walio chini ya miaka mitano kwa asilimia 65 ukilinganisha na asilimia 13 ya zoezi hilo kwa mwaka 2013.

Kabidhi Wasii Mkuu na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA,) Bi. Angela Anatory akizungumza katika kikao hicho kilichowakutanisha na wadau wanaofanya nao kazi kwa ukaribu katika utoaji huduma na kueleza kuwa majibu ya ufikiwaji wa usajili na utoaji vyeti kwa watoto walio chini ya miaka mitano kwa asilimia 65 utatoa majibu kupitia zoezi la sensa litakalofanyika Agosti 23 mwaka huu na kuwataka watanzania kushiriki vyema zoezi hilo kwa manufaa na maendeleo ya Taifa.
Msajili wa matukio ya kijamii Zanzibar Mohamed Makame akizungumza wakati wa kikao hicho na kueleza kuwa elimu kwa Umma inahitajika zaidi ili waweze kuwafikia na kutoa huduma kwa wananchi wote ambao wanahitajika kutoa taarifa sahihi na kupata haki ya kupata vyeti vyao vya kuzaliwa. 

 

* Mwamko mdogo wa watanzania kuandika Wosia waelezwa, watakiwa kuandika na kuhifadhi Wosia kupitia RITA  ili kuepusha migogoro ya kifamilia


WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA,) imepongezwa kwa jithada za kufanikikisha usajili na kutoa vyeti kwa watoto walio chini ya miaka mitano kwa asilimia 65 ukilinganisha na asilimia 13 ya zoezi hilo kwa mwaka 2013.


Hayo yameelezwa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Mary Makondo wakati akifungua mkutano ulioikutanisha RITA na wadau wanaofanya nao kazi kwa karibu kikao kilicholenga kujadili mafanikio, fursa kutoka kwa wadau katika kuboresha huduma pamoja na hali ya ushirikiano na wadau pamoja na kutafuta suluhu za changamoto ili kupanua wigo wa utoaji wa huduma.

Katibu Mkuu Makondo amesema, ufanisi uliooneshwa na RITA katika kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto walio chini ya miaka mitano katika mikoa 23 huku mikoa 3 iliyosalia kupatiwa huduma hiyo kwa siku za karibuni imelipa Taifa heshima ya kutembea kifua mbele katika mkutano mkuu wa Mawaziri barani Afrika utakaofanyika Oktoba mwaka huu ambapo kila nchi itaeleza hali ya usajili na kwa Tanzania hali ni nzuri kutokana na ufanisi uliooneshwa na RITA katika usajili wa na utoaji vyeti vya kuzaliwa kwa watoto walio chini ya miaka mitano milioni 7.7 kwa msaada wa Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo UNICEF, Balozi za Canada, Italy na kampuni ya mawasiliano ya Tigo Tanzania.


Amesema, kikao hicho kilichoikutanisha wakala hiyo na wadau wanaotumia huduma zao ni muhimu katika kuboresha huduma za kijamii kupitia usajili huo ambao pia husaidia Serikali katika mipango ya maendeleo pamoja na huduma za kijamii ikiwemo afya na elimu.


'' Programu hii ya usajili na kutoa vyeti kwa watoto walio chini ya miaka mitano iliyobuniwa na RITA na kushirikiasha wadau wa maendele wakiwemo UNICEF ni muhimu sana na imefanikiwa kwa kiwango kikubwa na fanisi wa hali ya juu..endeleeni kutoa elimu kwa Umma juu ya umuhimu wa nyaraka hii muhimu na Wizara inaielekeza RITA kuwa zoezi hili liwe endelevu ili kuwafikia watoto wote nchini wakiwemo walio na miaka 7 hadi 18 ambao wapo katika mifumo rasmi ya shule au vinginevyo kwa kuwa ni haki ya kila mtanzania kuwa na cheti cha kuzaliwa.''Amesema.

Akieleza kuhusiana na mwamko wa watanzania kuandika na kuhifadhi Wosia huduma ambayo inatolewa na RITA Bi. Makondo amesema, mwamko si wakuridhisha hali inayosababisha kuendelea kwa migogoro katika jamii huku waathirika wakubwa wakiwa ni watoto na wanawake.


''RITA inaandika na kuhifadhi Wosia kwa gharama nafuu kabisa na sio uchuro kufanya hivyo ni salama na uhakika tukiwa hatupo kile tulichofanyia kazi kwa ajili ya familia zetu kiendelee hivyo na tunachotakiwa kufanya ni kuandika wosia ili kuepusha migogoro na kuweka salama familia na wapendwa wetu.'' Amesema.


Aidha amesema kuwa Wizara imeielekeza RITA kufanya tafiti ya kwanini watu wengi hawaandiki Wosia na dodoso litaweka katika tovuti ya wakala hiyo na maoni yatakayotolewa na wananchi yatafanyiwa kazi katika kuboresha kipengele hicho.


Pia amewataka wadau kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania ambayo milango yake ipo wazi kwa ushirikiano katika kuhakikisha jamii ya watanzania inafikiwa na huduma zote muhimu.


Kwa upande wake Kabidhi Wasii Mkuu na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA,) Bi. Angela Anatory amesema, katika kuboresha huduma kwa wananchi watakuwa wakikutana na wadau hao mara mbili kwa mwaka ili kuboresha taasisi kwa manufaa ya jamii kwa kuhakikisha kupitia TEHAMA wanafanikisha zoezi la usajili na utoaji vyeti vya kuzaliwa kwa watoto walio chini ya miaka mitano na watanzania kwa ujumla kwa ushirikiano wa karibu na wadau.


Amesema majibu ya ufikiwaji wa watoto kwa asilimia 65 utaletwa na zoezi la sensa litakalofanyika Agosti 23 mwaka huu na kuwataka watanzania kushiriki vyema zoezi hilo kwa manufaa na maendeleo ya Taifa.


Kuhusiana na mwamko wa watanzania kuandika na kuhifadhi Wosia kupitia RITA Bi. Angela amesema bado ni mdogo na hadi sasa wakala hiyo imeandika na kuhifadhi Wosia 700 na kutoa rai watanzania kutumia huduma hiyo ya kuandika na kuhifadhi Wosia inayotolewa na wakala hiyo kwa gharama nafuu.

Kikao hicho kilichobeba kauli mbiu ya 'Ushiriki wa Wadau ni Muhimu katika Utoaji wa Huduma Bora, Kujenga Mifumo Thabiti, Kuongeza Ubunifu na Kusogeza Huduma kwa Wananchi' kimeikutanisha RITA na wadau mbalimbali zikiwemo benki, kampuni za mawasiliano, Balozi, taasisi za Serikali na binafsi pamoja na viongozi wa dini ambao kwa pamoja wametoka na maadhimio ya ushirikiano, matumizi ya TEHAMA pamoja na kutoa elimu kwa juu ya umuhimu wa kuwa na nyaraka muhimu ya kuzaliwa na wametoa rai kwa watanzania kushiriki zoezi la sensa litakalofanyika Agosti 23 ili kuiwezesha Serikali kupanga mipango thabiti ya maendeleo na huduma za kijamii.









Baadhi ya wadau wakitoa neno wakati wa kikao hicho ambapo wamehaidi ushirikiano na Serikali kupitia RITA kwa manufaa ya watanzania.







Matukio mbalimbali katika picha wakati wa kikao hicho.






Matukio ya picha za pamoja za wadau walioshiriki katika kikao hicho.(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MASSAKA, MICHUZI TV.)








 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad