HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, July 24, 2022

MSAJILI WA HAZINA AZITAKA TAASISI NA MASHIRIKA YA UMMA KUTUMIA FURSA ZA BENKI YA CRDB KUONGEZA UFANISI WA KIFEDHA

Taasisi na mashirika ya umma nchini yametakiwa kutumia fursa zinazotolewa na Benki ya CRDB kwa ajili ya kuongeza ufanisi na tija. Rai hiyo imetolewa na Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto katika semina maalum iliyoandaliwa na benki hiyo na kuwaleta pamoja wakuu wa taasisi, mashirika na wakala za Serikali.

Akizungumza katika semina hiyo iliyofanyika katika hoteli ya Johari Rotana Jijini Dar es Salaam, Mgonya amesema ili taasisi, wakala na mashirika hayo kuendana na kasi na malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita kunahitajika ufanisi wa kifedha ambao utasaidia kuboresha utendaji na huduma wanazozitoa kwa wananchi. 
“Benki ya CRDB imetudhihirishia hapa utayari wake wakushirikiana na taasisi, mashirika na wakala zetu katika kuboresha ufanisi kupitia huduma na bidhaa bunifu zinazotolewa na benki hii. Tuitumie fursa hii vizuri kwani benki hii ina uwezo mkubwa wa uwezeshaji wa kimifumo na kifedha kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia katika miradi ya kimkakati,” aliongezea Mgonya.

Aidha, Mgonya alibainisha kuwa Serikali imeweka mkakati madhubuti wa kuhakikisha taasisi, mashirika, na wakala za Serikali zinaleta tija kwa Taifa. Serikali ina uwekezaji katika taasisi na mashirika 297, wenye thamani ya Sh. trilioni 67. 

“Mkakati huu umekuwa na manufaa kwa Serikali kwani katika Mwaka wa Fedha wa 2021/22 ulioishia Juni 30, Ofisi tumefanikiwa kukusanya mapato yasiyo ya kodi ya jumla ya Sh bilioni 852.98 ikiwa ni asilimia 109.50 ya lengo.”
Akihitimisha hotuba yake Mgonya aliyataka taasisi na mashirika ya Serikali pia kujifunza kutokana na mafanikio ya Benki ya CRDB ambayo imekuwa ikitengeneza faida kila mwaka na kutoa faida kwa Wanahisa wake ikiwamo Serikali.

“Serikali inajivunia utendaji wa Benki ya CRDB ambapo kila mwaka imekuwa ikitupa gawio, ambapo hivi karibuni tu wametupa gawio la Sh. bilioni 36.1. Niwapongeze sana, na pia niwapongeze kwa namna ambavyo wamedhamiria kuzijengea uwezo taasisi, mashirika, na wakala zetu za Serikali,” 

Akiwasilisha mada katika semina hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alimhakikishia Msajili wa Hazina kuwa Benki hiyo ipo tayari kufanyakazi kwa ukaribu na taasisi, mashirika, na wakala za Serikali ili kuongeza ufanisi katika utendaji wao, kuboresha huduma kwa Watanzania, na kuongeza tija ya mchango wao katika mapato ya Serikali.
“Semina hii ni mwitikio wa wito wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wakuzitaka taasisi za umma kushirikiana na taasisi binafsi ili kuboresha utendaji na kuleta tija zaidi kwa Watanzania. Tukiwa ‘Benki ya Kizalendo’ hili ni eneo ambalo tumelipa kipaumbaule na malengo yetu ni kujenga ushirikiano ambao utaziongezea taasisi za Serikali ufanisi wa kifedha,” alisema Nsekela.

Akielezea maeneo ambayo benki hiyo imejipanga kushirikiana na taasisi za Serikali, Nsekela alisema Benki ya CRDB ina mtaji wa kutosha kuwezesha miradi, na programu za maendeleo zinazotekelezwa na taasisi hizo. Aliongezea kuwa benki hiyo pia ina huduma za uwekezaji, pamoja na mifumo thabiti ya kusaidia ukusanyaji wa mapato na kufanyia malipo.
“Benki yetu pia inahuduma kwa ajili ya wafanyakazi wa taasisi na mashirika haya zinazolenga kusaidia kuboresha maisha yao. Tuna huduma za akaunti za mishara, huduma za uwezeshaji kupitia mikopo, na huduma za kidijtali ambapo hivi sasa mfanyakazi anaweza kupata mkopo popote pale alipo kidijitali kupitia huduma ya ‘Salary Advance’ inayopatikana katika SimBanking,” alisema.

Akiongea kwaniaba ya taasisi, mashirika na Wakala za Serikali zilizohudhuria semina hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), Abdulrazak Badru ameishukuru Benki ya CRDB kwa kuandaa semina hiyo ambayo imetoa fursa ya kujadili changamoto zinazozikabili taasisi na mashirika ya umma nchini, pamoja na fursa zinazotolewa na benki hiyo.

“Bodi ya Mikopo ni moja ya washirika wakaribu wa Benki ya CRDB kupitia mfumo wa usajili na utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ambao umetusaidia kuongeza ufanisi katika utoaji mikopo. Tunajivunia ushirikiano huu, na leo hii tumepata kujifunza fursa na maeneo mengine ya ushirikiano ambayo naamini yataongeza tija katika taasisi yetu,” alisema Badru.
Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto (watatu kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela wakati wa semina maalum iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa ajili ya taasisi, mashirika, na wakala za serikali iliyofanyika katika hoteli ya Johari Rotana Jijini Dar es Salaam. Wengine pichani kutoka kulia ni Afisa Mkuu wa Uendeshaji Benki ya CRDB, Bruce Mwile, Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa, na Afisa Mkuu wa Fedha Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo.
Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto (kulia) akiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela wakati muda mfupi baada ya ufunguzi wa semina maalum iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa ajili ya taasisi, mashirika, na wakala za serikali iliyofanyika katika hoteli ya Johari Rotana Jijini Dar es Salaam. Wengine pichani ni Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa, Afisa Mkuu wa Uendeshaji Benki ya CRDB, Bruce Mwile, Mkurugenzi wa Mawasiliano Benki ya CRDB, Tully Mwambapa, na Afisa Mkuu wa Fedha Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo.










No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad