HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, July 17, 2022

MAHAKIMU WAPYA WAASWA KUTOFUNGWA NA KANUNI ZA KIUFUNDI WANAPOTOA HAKI

 Na Mary Gwera, Mahakama


Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma amewaasa Mahakimu Wakazi wapya kutenda haki bila kufungwa kupita kiasi na masharti ya kiufundi wanapohudumia wananchi katika Mahakama za Mwanzo.

Akizungumza na jumla ya Mahakimu Wakazi wapya 20 mara baada ya kuwaapisha tarehe 16 Julai, 2022 katika ukumbi wa Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam, Jaji Mkuu amesema kuwa, idadi kubwa ya mashauri hufunguliwa Mahakama za Mwanzo hivyo vipingamizi na sababu nyingi zisizo na msingi husababisha ucheleweshaji wa mashauri hayo.

“Mnaenda kuhudumia wananchi wa karne ya 21, ambao wana upeo mkubwa wa masuala ya sheria kwakuwa wanasoma na wanafahamu haki zao, hivyo jitahidini kuwa makini na kutofungwa na kanuni za msingi mnapotoa haki kwa kuwa Mahakama za Mwanzo ndio haki inapoanzia hivyo msicheleweshe mashauri hayo bali mfanye jitihada za kumaliza mashauri hata chini ya muda uliopangwa na Mahakama wa kumaliza mashauri ya Mahakama za Mwanzo ambao ni miezi sita,” amesema Mhe. Prof. Juma.

Kadhalika, Jaji Mkuu amekemea maahirisho ya mara kwa mara kwa mashauri yanayofunguliwa katika Mahakama aidha, yanayosababishwa na Hakimu mwenyewe ama Wakili ambapo ameeleza kuwa, kwa kufanya hivyo haki ya mwananchi itacheleweshwa.

Aidha; Jaji Mkuu amewaasa Mahakimu hao kusoma kanuni za Maadili za Maafisa wa Mahakama na kuzingatia maadili kwa kutojihusisha na vitendo vyovyote ambavyo vinavyoweza kuleta maswali kwa jamii pindi wanapotekeleza majukumu yao.

“Maadili ni kiini muhimu ya haki zinazotafutwa Mahakamani. Naomba niwakumbushe Mahakimu wapya kuwa uwezo wenu wa kufanya kazi za Kimahakama ni upande mmoja tu wa sarafu. Upande wa pili wa sarafu, ambao pia una umuhimu mkubwa, ni uwajibikaji na maadili. Uelewa, werevu na ujuzi mkubwa wa sheria na taratibu za utoaji haki lazima uambatane na uwajibikaji na maadili,” amesisitiza.

Mhe. Prof. Juma ameongeza kwa kuwataka Mahakimu hao kujitathmini hata aina ya marafiki wa kuwa nao, kujiangalia katika matumizi ya mitandao ya kijamii, masuala ya kisiasa na kutii kiapo walichokula ambacho kinawataka kuwa na utii kwa Jamhuri na kuhudumia wananchi.

Kwa upande wake, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amewaasa Mahakimu hao kuzingatia masuala kadhaa wanapotekeleza majukumu yao ikiwemo matumizi ya TEHAMA, matumizi ya usuluhishi/mapatano (mediation), kujiepusha na vitendo vya rushwa na wajibu wa kusikiliza na kutoa uamuzi kwa haraka.

“Kwanza nichukue fursa hii kuwapongeza Mahakimu wapya kwa kuwa mmepitia katika mchakato mrefu hadi kupatikana kwenu, hivyo napenda kuwaasa mnapoenda kuhudumia wananchi msisahau matumizi ya TEHAMA kwakuwa Mahakama imefanya uboreshaji wa huduma zake ikiwemo Matumizi ya TEHAMA,” amesema Mhe. Siyani.

Kwa mujibu wa Msajili wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Kevin Mhina amesema kuwa, kuapishwa kwa Mahakimu Wakazi 20 leo kunaongeza idadi ya Mahakimu Wakazi na kuwa na jumla ya Mahakimu Wakazi 1,135 kwa nchi nzima ambapo 552 kati yao ni wanaume na 583 ni wanawake.

Baada ya kuapishwa Mahakimu hao wanatarajia kushiriki katika Mafunzo elekezi katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto kwa lengo la kuelekezwa zaidi mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kuanza kazi rasmi.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akimkabidhi vitendea kazi Hakimu Mkazi mara baada ya Kuapishwa Mahakimu Wakazi wapya 20, tarehe 16 Julai, 2022 katika ukumbi wa Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa naasa kwa Mahakimu Wakazi wapya 20 (hawapo pichani) na kusisitiza wakatende kutenda haki.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akitoa neno kwa Mahakimu Wakazi Wapya 20 (hawapo pichani)
Sehemu ya Mahakimu Wakazi Wapya wakifuatilia hotuba ya Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo pichani) mara baada ya Kuapishwa Mahakimu Wakazi wapya 20.
Jaji Mkuu wa Tanznaia Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mahakimu Wakazi Wapya mara baada ya Kuapishwa, wengine ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (kushoto) na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es salaam, Mhe. Amir Mruma (kulia).
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Majaji Wafawidhi wa Divisheni mbalimbali za Mahakama Kuu, mara baada ya kushudia Kuapishwa kwa Mahakaimu Wakazi Wapya 20, wengine ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (kushoto) na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es salaam, Mhe. Amir Mruma (kulia)
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wasajili, Manaibu Wasajili na Watendaji mara baada ya kushudia Kuapishwa kwa Mahakaimu Wakazi Wapya 20, wengine ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (kushoto) na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es salaam, Mhe. Amir Mruma (kulia)
Baadhi ya Hakimu Mkazi akila Kiapo cha Uhakimu mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo pichani) wakati wa uapisho huo
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitia sahihi kwenye moja ya Hati ya Kiapo cha Hakimu Mkazi mara baada ya kukishuhudia kiapo hicho.
Sehemu ya Majaji na Majaji Wafawidhi wa Divisheni mbalimbali za Mahakama Kuu, wakifuatilia hafla ya Kuapishwa kwa Mahakaimu Wakazi Wapya 20. (PICHA na Innocent Kansha - Mahakama)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad