HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, July 26, 2022

Korea kuendelea kusaidia Mloganzila

 Serikali ya Korea itaendelea kuwajengea uwezo wataalamu wa afya Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila na kutoa msaada wa vifaa tiba kadri itakavyowezekana ili kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.


Kauli hiyo imetolewa na Balozi msaidizi wa Korea nchini Bi. Songjoo Lee alipofanya ziara ya siku moja katika Hospitali ya Mloganzila na kutembelea miradi mbalimbali ikiwemo mtambo wa kuzalisha hewa tiba (Oxygen generating plant), wodi ya uangalizi maalumu ya wazazi (Maternal ICU), pamoja na mradi wa kuboresha huduma ya mama na mtoto uliohusisha uboreshaji wa wodi ya watoto wachanga mahututi (NICU) ambayo imejengwa kwa ufadhili wa Korea kupitia Taasisi ya Korea Foundation for International Health Care (KOFIH).

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Bi. Lee amesema Korea itaendelea kusaidia uboreshaji wa huduma za afya na kuendesha mafunzo mbalimbali hasa katika maeneo ambayo yanauhitaji ikiwemo matumizi ya vifaa tiba.

Akielezea ushirikiano ulipo baina ya MNH-Mloganzila na Serikali ya Korea kupitia KOFIH, Naibu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi ameeleza kuwa KOFIH imechangia kupunguza malalamiko ya wagonjwa kwani awali kulikua na malalamiko juu ya huduma ila kwa sasa malalamiko yamepungua kutokana na uboreshaji uliofanyika.

“Kupitia ushirikiano uliopo baina ya Mloganzila na KOFIH tumeweza kufanya maboresho makubwa kwenye utoaji wa huduma kitu ambacho kimesaidia wananchi kuongeza imani juu wa huduma tunazotoa”amesema Dkt. Magandi

Ameongeza kuwa KOFIH wametoa mafunzo juu ya matumizi ya vifaa tiba ambavyo vilikua havitumiki hapo awali ikiwemo mashine ya kuvunja mawe kwenye figo na mfumo wa mkojo kwa njia ya mawimbi mshituko (Extracorporeal shock wave lithotripsy), mashine ya kuponesha majeraha na maumivu ya hedhi, kukakamaa kwa misuli na utulivu kwa watu wanaokosa usingizi pia wamesaidia kuanzisha karakana ambayo inatumika kufanya matengenezo ya vifaa tiba ambavyo vimeharibika.

Pia wamesaidia kurahisisha upatikanaji wa baadhi ya vipuri ambavyo havipatikani kwa urahisi nchini na uwagizwaji wake unachukua muda mrefu kutufikia ila kutokana na ushirikiano uliopo kwa sasa vinatufikia kwa wakati.

Dkt. Magandi amemshukuru Bi. Lee kwa ziara yake na kuahidi kuwa watendelea kudumisha ushirikiano baina ya Mloganzila na KOFIH ili kunufaisha wananchi na kupunguza mzigo kwa serikali wa kupeleka wagonjwa nje.
Balozi Msaidizi wa Korea nchini Bi. Songjoo Lee akisaini kitabu cha wageni alipofanya ziara ya siku moja katika Hospitali ya Mloganzila na kutembelea baadhi ya miradi iliyofadhiliwa na Korea kupitia Taasisi ya Korea Foundation for International Health Care (KOFIH).
Naibu Mkurugenzi Mtendaji MNH-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi akielezea jinsi ushirikiano uliopo baina ya KOFIH na Mloganzila unavyosaidia kuboresha huduma za afya.
Bi. Lee (wa kwanza kushoto) akielezea namna alivyofurahishwa na uongozi wa MNH-Mloganzila pamoja na usimamizi mzuri katika uboreshaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Bi. Lee na Dkt. Magandi pamoja na baadhi ya wakurugenzi wakitembelea baadhi ya miradi iliyofadhiliwa na KOFIH.
Mhandisi Vifaa Tiba Bi. Diana Kimario akielezea namna ambayo karakana ya vifaa tiba ilivyosaidia kurahisisha utengenezaji wa vifaa tiba ambavyo vimeharibika.
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga MNH-Mloganzila Sis. Redemptha Matindi akielezea ni namna gani mradi wa kuboresha huduma ya mama na mtoto uliohusisha uboreshaji wa wodi ya watoto wachanga mahututi (NICU) ambayo imejengwa kwa ufadhili wa Korea kupitia Taasisi ya Korea Foundation for International Health Care (KOFIH) ulivyosaidia kuboresha huduma ya mama na mtoto.
Dkt. Magandi na Balozi Msaidizi wa Korea nchini Bi. Songjoo Lee wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wakurugenzi wa Mloganzila pamoja na ujumbe uliombatana na Bi. Lee

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad