HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, July 9, 2022

DKT STERGOMENA: ENDELEZENI UTII, WELEDI NA UAMINIFU KAZINI


WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb), amewataka watumishi wa Wizara ya Ulinzi na JKT kuendeleza utii, weledi na uaminifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi, na kuepuka migogoro mahali pa kazi.

“ Pamoja na kuwa sina mashaka kuhusu nidhamu mliyonayo katika kazi, naendelea kusisitiza kuendeleza utii, weledi na uaminifu katika utekelezaji wa majukumu yenu ya kazi, na kuepuka migogoro mahali pa kazi”, alisema.

Dkt. Stergomena ameyasema hayo wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi na vyeti kwa wafanyakazi bora kwa mwaka 2022, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ndogo ya Wizara - Upanga, Jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Waziri pia, amewashukuru watumishi wote kwa utendaji wao, pamoja na changamoto kadhaa wanazokabiliana nazo, wameendelea kujitoa na kutumia weledi wao katika kutekeleza majukumu mbalimbali.

“Nitumie fursa hii pia, kuwashukuru watumishi wote kwa utendaji wenu, pamoja na changamoto kadhaa tunazokabiliana nazo, mmeendelea kujitoa na kutumia weledi wenu katika kutekeleza majukumu mbalimbali. Hili ni jambo la kujivunia na ninawapongeza na niwatake kuendelea na moyo huo ili kulijenga Taifa letu”, alisema.

Dkt. Stergomena alibainisha kuwa siku hii ya leo ni muhimu sana, maana wamekusanyika kwa lengo la kukabidhi zawadi kwa wafanyakazi bora, kwa maana hiyo akawasihi na watumishi ambao hawakubahatika kuchaguliwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii. “Sote tumefanya kazi na kuchangia katika mafanikio ya Wizara, hata hivyo, katika ushindani wapo watakaoibuka kidedea. Tunawapongeza washindi, na Wizara inautambua mchango wa kila mmoja. Hivyo tuendelee kujituma na kuwa washindi wa kesho”, alisistiza.

Waziri Stergomena amewatoa wasiwasi Watumishi hao kuwa “Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais na Amiri Jeshi Mkuu, inajali na kuuthamini sana mchango unaotolewa na watumishi wa umma. Hili linathibitishwa na hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa, ikiwa ni pamoja na kuwapandisha watumishi vyeo na madaraja, kulipa malimbikizo, kupandisha viwango vya posho za kujikimu, na kupandisha mishahara, ambapo watumishi wa umma wa kima cha chini wapate ongezeko la asilimia 23.3”, alisema.

Aidha, Mheshimiwa Waziri amewataka Watumishi wa Umma kuendelee kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais, katika kuongeza hamasa ya utendaji kazi kwa kuleta tija, na kuimarisha amani na kuliletea maendeleo Taifa letu.

Akihitimisha Hotuba yake kwa Watumishi hao, Dkt. Stergomena amewakumbusha na kuwasisitiza watumishi wote kushiriki Zoezi la Sensa Kitaifa ifikapo tarehe 23 Agosti, 2022. Zoezi hili ni muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu, hivyo basi, akasistiza kuzihimiza familia na jamii zao kushiriki zoezi hili muhimu kitaifa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad