Kwa
Ufupi: Benki ya NMB yaendelea kuwa kinara wa ufanisi nchini Tanzania.
Faida ya benki kabla ya kodi yafikia TZS bilioni 298, sawa na ongezeko
la asilimia 54.
· Faida baada ya kodi: TZS bilioni 208 - ongezeko la asilimia 53 kwa mwaka
· Jumla ya Mapato ya benki: TZS bilioni 562- ongezeko la asilimia 21 kwa mwaka
· Jumla ya Mali: TZS Trilioni 9 - ongezeko la asilimia 19 kwa mwaka
_________________________________________________________________
Dar
es Salaam. July 28, 2022- Benki ya NMB imeendeleza ufanisi wake
kiutendaji katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2022. Faida kabla
ya kodi imeongezeka kwa asilimia 54 na kufikia Shilingi bilioni 298
ikilinganishwa na Shilingi bilioni 193 ya kipindi kilichoishia June
2021. Faida baada ya kodi imeongezeka kwa asilimia 53 na kufikia
Shilingi bilioni 208 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 135 ya kipindi
kilichoishia June 2021. Faida hii inatokana na kuongezeka kwa ufanisi,
kukua kwa mizania ya benki, ubora na umakini katika kusimamia mikopo, na
kuongezeka kwa miamala ya wateja.
Mapato ya Benki yameongezeka
kwa asilimia 21 hadi kufikia shilingi bilioni 562 katika kipindi
kilichomalizikia mwezi Juni 2022 ikilinganishwa na shilingi bilioni 463
zilizopatikana kipindi kama hicho mwaka jana. Mapato haya yamechangiwa
na ongezeko la mikopo kwa wateja na uwekezaji kwenye hati fungani za
Serikali, pamoja na ongezeko la miamala ya kibenki.
Benki
imeendelea kuimarisha ufanisi kwenye gharama za uendeshaji, ulioshuhudia
uwiano wa gharama za uendeshaji na mapato ukishuka mpaka asilimia 42
kutoka asilimia 47 katika kipindi kama hichi mwaka uliopita. Benki
imeendelea kutilia mkazo uimarishaji wa ufanisi huku ikiboresha
uwekezaji katika teknolojia na vipao mbele vya kimkakati vyenye lengo la
kuongeza ubora wa huduma za kibenki.
Katika kipindi hiki cha
nusu ya mwaka 2022, ubora wa mali za NMB uliimarika kutokana na mikakati
thabiti ya kuimarisha mikopo ya benki. Uwiano wa mikopo chechefu
umeimarika hadi asilimia 3.8 kutoka asilimia 4.3 katika kipindi kama
hiki mwaka uliopita, ikiwa ndani ya kiwango cha juu cha asilimia 5
kilichowekwa na Benki Kuu ya Tanzania.
Katika kipindi hiki cha
nusu ya kwanza ya mwaka 2022, Mizania ya Benki iliongezeka kwa asilimia
19 na kufikia Shilingi Trilioni 9, ukilinganisha na Shilingi Trilioni
7.6 kutokana na kuongezeka kwa wateja, ikiashiria ubora na mahusiano
mazuri ya benki na wateja wake.
Akizungumzia mafanikio haya
makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2022,
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna amesema: “Tunajivunia
na kushukuru kwa ufanisi na uimara wa benki yetu ya NMB. Mafanikio haya
makubwa ya nusu ya mwaka 2022 ni kielelezo cha ufanisi mzuri uliotokana
na utekelezeji makini wa mikakati yetu. Tunayo furaha kuona benki
ikiendelea kupata matokeo mazuri na endelevu ya kiutendaji yenye kuleta
tija kwa wanahisa wetu, wateja wetu, na wadau wote wa Benki ya NMB.”
Aliongeza
kwa kusema kuwa: “Tutaendelea kuimarisha na kujikita katika misingi
yetu imara, pamoja na kutilia mkazo uwekezaji katika teknolojia, pamoja
na uboreshaji wa huduma zetu ili kuhakikisha benki inaendelea kupata
mafanikio endelevu zaidi na yenye kuleta maendeleo chanya kwa Taifa.”
Aidha,
Bi Ruth alimalizia kwa kusema, ‘Tunawashukuru wateja wetu, wafanyakazi,
wawekezaji, na wadau wote nchini Tanzania, kwa mchango wao mkubwa
katika mafanikio haya ya Benki ya NMB.”
No comments:
Post a Comment