HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, June 6, 2022

WANAHISA BENKI YA NMB WAIDHINISHA GAWIO BIL. 96.7/-

 

 




Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna akimkabithi Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya NMB, Dk. Edwin Mhede ripoti ya mwaka 2021 kwenye Mkutano Mkuu wa 22 wa Wanahisa, uliofanyika ukumbi wa JNICC, Dar es Salaam. Kushoto ni Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Juma Kimori na Kaimu katibu wa NMB, Consolatha Mosha. Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa 22 wa Wanahisa, uliofanyika ukumbi wa JNICC, Dar es Salaam.

*******************

Wanahisa wa Benki ya NMB wameidhinisha gawio la Sh 96.7 bilioni kwa mwaka 2021, huku wakiwa na imani kubwa benki yao kuendelea kufanya vizuri zaidi mwaka huu.

Gawio la mwaka 2021 linatokana na kuongezeka kwa faida baada ya kodi kutoka Sh206 bilioni mwaka 2020 na kufikia Sh290 bilioni mwaka jana, mwaka 2021

Katika Mkutano wake Mkuu wa 22 wa Mwaka uliofanyika mwishoni mwa wiki, wanahisa walipitisha kiasi hicho cha fedha ambacho ni sawa na malipo ya Sh193 kwa kila hisa kwa kipindi kilichoishia Desemba 31, 2021 (wanahisa walipata gawio la Shs 137 kwa kila hisa kwa mwaka 2020).

Akizungumza na wandishi wa habari, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB- Ruth Zaipuna alisema Benki hiyo itaendeleza mwenendo wake wa kufanya vizuri kwa kuvuka malengo iliyojiwekea kwa mwaka huu pia.

Matarajio hayo yanatokana na matokeo mazuri ya robo ya kwanza ya mwaka huu ambapo Benki tayari imepata faida baada ya kodi ya Sh101bilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 55 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.

“Ni kweli tumeuanza mwaka 2022 vizuri. Mafanikio makubwa ya kiutendaji kwa mwaka 2021 na matokeo mazuri ya robo ya kwanza ya mwaka 2022 ni kielelezo cha ufanisi mzuri unaotokana na utekelezaji makini wa mikakati yetu. Tutaendelea kutekeleza kwa umakini sana mikakati tuliyojiwekea na tunaamini kwamba malengo tuliyojiwekea kama benki tutayafikia na kuyapita mwaka huu wa 2022,” alisema Zaipuna.

Alisema kwa mahesabu ya kawaida, matokeo ya robo ya kwanza ya mwaka huu yanaleta picha kuwa utakuwa mwaka mzuri pamoja na changamoto zinazoendelea kujitokeza duniani. “Kadri tunavyoendelea kukabiliana na mazingira ya biashara yanayobadilika kwa kiasi kikubwa, tumejipanga kwa umakini kupata matokeo mengine mazuri yatakayoendeleza rekodi yetu sokoni” alisema.

Mwaka jana, Benki ya NMB ilifanikiwa kuvuka malengo yake katika vigezo karibu vyote vya kiutendaji, huku amana za wateja zikipanda hadi Sh6.6 trilioni na mikopo ikifikia Sh4.8 trilioni.

Benki hiyo pia imeweka rekodi katika sekta ya benki kwa kuwa na uwiano bora wa gharama za mapato wa asilimia 46 hadi kufika Desemba 31, 2021 ikiwa imepungua kwa asilimia 5 ikilinganishwa na mwaka 2020 (asilimia 51), huku uwiano wa mikopo chechefu (NPL) ukifikia asilimia 4 ya mikopo ghafi, kiwango ambacho ni chini ya kile kinachotakiwa na Mdhibiti (Benki Kuu).

Kwa ujumla katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita benki ya NMB ilishuhudia Mizania bora, ukwasi wa kutosha na viwango thabiti vya mtaji ambavyo viko juu ya viwango vya udhibiti. Benki hiyo pia ilitambulika kimataifa kama benki bora na salama.

Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya NMB, Dk. Edwin Mhede alisema “Tumeendelea kudhihirisha ufanisi na ustahimilivu mkubwa kwenye biashara. Tutaendelea kujumuisha mafanikio makubwa yaliyopatikana, tuendelee kuzingatia kuwainua wafanyakazi wenye ujuzi unaofaa ili kuwasaidia kufanya kazi kwa ufanisi. Ninawahakikishia wanahisa wote wa Benki ya NMB, dhamira ya Bodi ni kufanya maamuzi sahihi ya kifedha na kuongeza faida kwa wanahisa wetu kwa miaka mingi ijayo”.





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad