SERIKALI kwa ufadhili wa Benki ya Dunia imezindua Programu ya kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji katika shule za awali na msingi (BOOST) yenye thamani zaidi ya Shilingi trilioni 1.15.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika leo Juni 6, jijini Arusha, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Programu hiyo ambayo itatekelezwa kwa miaka mitano inalenga kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji, ujuzi na ubora wa walimu katika ufundishaji na kuimarisha upatikanaji wa rasilimali za kuwezesha utoaji wa huduma katika ngazi ya Halmashauri.
Prof. Mkenda ameeleza kuwa Programu itajikita katika kuboresha miundombinu ya shule za Msingi kwa kuzingatia mahitaji ambapo madarasa 12,000 yatajengwa, uimarishaji wa mpango wa shule salama katika shule 600, kuimarisha uwiano wa uandikishaji wa wanafunzi wa Elimu ya Awali na kuboresha vifaa na njia za ufundishaji katika madarasa ya Elimu ya Awali.
“Pia itaimarisha na kuendeleza mpango wa mafunzo ya walimu kazini, kuimarisha vituo vya walimu na shule za msingi katika utekelezaji wa mtaala wa TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji na kuendeleza utengaji wa bajeti kwa ajili ya kugharimia shughuli mbalimbali za utoaji wa Elimu na kuimarisha utawala bora katika elimu,” amesema Prof. Mkenda
Waziri Mkenda amewataka watendaji wote katika ngazi ya Wizara na Taasisi watakaohusika na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Programu kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kufikia lengo kila mwaka na kuzingatia vigezo na viwango vyote vilivyowekwa ili kutekeleza programu hiyo kwa ufanisi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. David Silinde (Mb) amesema ofisi yake imepanga kuwajengea uwezo watekelezaji wa programu hiyo ili itekelezwe kama ilivyopangwa.
Mhe. Silinde amesema kuwa TAMISEMI itaendelea kuchukua hatua za haraka na maboresho pale inapohitajika ili kuondoa changamoto zote ambazo zinaweza kukwamisha programu hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini, Mara Warwick amesema matarajio ya taasisi hiyo ni kuona elimu ya awali na msingi inakuwa bora, salama na jumuishi kwa watoto wote wanaotakiwa kuwa shuleni.
“Tunatarajia programu hii ya BOOST itanufaisha wanafunzi zaidi ya milioni 12 katika eneo la Tanzania Bara, uwekezaji katika eneo hili unaweza ukawa kichocheo kikubwa katika kukabiliana na umaskini,” ameeleza Mkurugenzi Mara Warwick
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Aloyce Kamamba ameipongeza Serikali kwa kuzindua programu hiyo, ambapo ameshauri miundombinu inayokwenda kujengwa isimamiwe kwa umakini ili iwe bora na ikamilike kwa wakati huku akisisitiza juu ya walimu kupatiwa mafunzo endelevu na kuajiri walimu wapya.
No comments:
Post a Comment