TARURA WILAYA YA TUNDURU YARUDISHA MAWASILIANO KWA WAKAZI WA MCHOTEKA-MASUGURU-MARUMBA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, June 29, 2022

TARURA WILAYA YA TUNDURU YARUDISHA MAWASILIANO KWA WAKAZI WA MCHOTEKA-MASUGURU-MARUMBA

 Na Muhidin Amri, Tunduru

WANANCHI wa kata ya Mchoteka na Marumba wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,wameishukuru serikali kwa kukamilisha ujenzi wa barabara inayounganisha vijiji mbalimbali katika kata hizo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema,kukamilika kwa barabara ya Mchoteka-Masuguru-Marumba kwa kiwango cha Changarawe kumemaliza changamoto ya muda mrefu ya kukosa mawasiliano kati ya kata hizo mbili na kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi.

Matola Mohamed mkazi wa kijiji cha Masuguru alisema,uthubutu uliofanywa na Serikali ya awamu ya sita kujenga barabara hiyo ni kati ya mambo mazuri yaliyofanyika katika kipindi cha mwaka mmoja na miezi mitatu cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufungua fursa za kiuchumi na maendeleo ya kata hizo na wilaya ya Tunduru kwa ujumla.

Alisema,kujengwa kwa barabara hiyo wanaona kama zawadi iliyotolewa na Serikali hasa ikizingatia kwa muda mrefu walikuwa katika mateso makubwa, kwa kukosa mawasiliano ya uhakika kati ya kata hizo na maeneo mengine na wakati mwingine kushindwa kusafirisha mazao yao kwenda sokoni.

Mashale Salanje mkazi wa Mchoteka alisema,awali barabara hiyo ilikuwa kero kubwa kutokana na ubovu hasa mashimo makubwa katikati ya barabara jambo lililo sababisha maisha yao kuwa magumu kufuatia kupanda kwa bidhaa ikiwamo nauli ya magari na kutumia muda mwingi wanaposafiri kwenda Tunduru mjini.

“ kwa hali hii naipa hongera sana serikali ya mama yetu Samia Hassan kwa kazi nzuri,kwanza watakaozaliwa miaka ya 2025 hadi 2026 wanaweza kusema tangu enzi za Adam ilikuwa hivi hivi kumbe imejengwa mwakaa huu 2022”alisema.

Hassan Majongo,ameipongeza serikali kupitia wakala wa barabara za mjini na vijijini(Tarura) wilaya na mkoa kujenga barabara hiyo kwa viwango vya hali ya juu kwani imesaidia sana kurahisisha mawasiliano na kupungua kwa ugumu ya maisha.

Aidha alisema,kunafanya kata ya Mchoteka kuwa kitovu cha mawasiliano kati hizo na maeneo mengine ya wilaya ya Tunduru,kwani itatoa fursa kwa wananchi kufanya shughuli mbalimbali ikiwamo kusafirisha mazao yao kutoka mashambani kwenda sokoni.

Majongo,ameiomba Serikali kuendelea kujenga na kuboresha barabara nyingine ikiwamo barabara kuu ya Tunduru-Nalasi hadi Mtwarapachani wilayani Namtumbo kwa kiwango cha lami kwa kuwa barabara hiyo ni muhimu kiuchumi kwa wakazi wa wilaya hizo mbili.

Kwa upande wake Meneja wa Tarura wilaya ya Tunduru Silvanus Ngonyani alisema,imejengwa kwa gharama ya Sh.milioni 265 zilizotokana na ongezeko la tozo zilizoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kiwango cha changarawe kwa km zote 17 na imefunguliwa rasmi baada ya kukamilika.

Alisema, ilianza kujengwa mwezi Novemba mwaka jana na ilitakiwa kukamilika mwezi Februari mwaka huu,lakini ilishindwa kukamilika kwa muda uliopangwa kutokana na changamoto ya mvua kubwa zilizonyesha na imekamilka mwezi Mei mwaka huu.

Alisema,barabara hiyo ina faida nyingi kwa wakazi wa maeneo hayo kutokana na uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na biashara ikiwamo mpunga,mahindi,ufuta na korosho na muhimu kiulinzi wa nchi yetu kwa kuwa kata ya Mchoteka na Marumba zinapatikana na nchi Jirani ya Msumbiji.

Ngonyani,amewataka wananchi kuitunza na kuitumia barabara hiyo kama kichocheo cha kukuza kipato na kuondokana na umaskini hasa ikizingatia kuwa bado kuna fursa nyingi ambazo zikitumika vizuri kata hizo zitakuwa mfano wa kuigwa.
Muenekano wa sehemu ya Barabara ya Mchoteka-Masuguru-Marumba wilayani Tunduru yenye urefu wa km 17 iliyojengwa na Wakala wa Barabara za mijini na vijijini(Tarura)wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma kama inavyoonekana,kujengwa kwa barabara hiyo ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa maeneo hayo kiuchumi kwa kuwa itawezesha kusafirisha mazao kutoka mashambani kwenda Sokoni. Picha na Muhidin Amri

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad