HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, June 8, 2022

Samia awahakikishia wafanyabiashara ujenzi miundombinu wezeshi

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
RAIS Samia Suluhu Hassan amesema serikali itaendelea kuwekeza kwenye miundombinu wezeshi kama moja mkakati wa serikali yake wa kuboresha mazingira ya kufanya biashara kuvutia uwekezaji hapa nchini.

“Kuwepo kwa miundombinu wezeshi kutasaidia kujenga uchumi jumuishi sambamba na kuboresha utoaji wa huduma. Tumefanikiwa kuondoa tozo ambazo hazina tija ili kuongeza ukuaji wa biashara na uwekezaji,” amesema.

Akizungumza kwenye Mkutano wa 13 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Jijini Dodoma jana, Rais Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa TNBC alisema serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi zitaendelea kufanya kazi pamoja,

Kwa mujibu wa Rais Samia, serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa sekta za biashara na uwekezaji zinakuwa na kutoa mchango stahiki katika kukuza uchumi na pato la taifa kwa manufaa ya watanzania.

“Uboreshaji huu wa mazingira ya biashara uhusishe pia chini kwenye ngazi za wilaya na mikoa kwani itakuwa maana zaidi. Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kuwa na raslimali nyingi hivyo sekta za umma na binafsi zinapaswa kufanya kazi kwa pamoja ili kuwaletea watanzania maendeleo,” alisema.

Rais Samia pia aliwashukuru wafanyabiashara kwa kuchangia fedha zilizofanikisha kutengeneza filamu ya ‘ROYAL TOUR’ ambayo imesaidia sana kuzitangaza fursa mbalimbali ikiwemo za utalii hapa Tanzania.

“Royal Tour ni moja ya jitihada za kimkakati zilizolenga kuvutia watalii hapa nchuni,” alisema Rais Samia na kuongeza kuwa filamu hiyo imeshaanza kuleta matokeo chanya katika sekta ya utalii.

Kwa upande wake,Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Bw Paul Makanza mbali ya kuipongeza serikali kwa kutekeleza maazimio ya Mkutano wa 12, alisema katika kifupi cha uongozi wa Awamu ya Sita Rais Samia Suluhu Hassan mafanikio mengi yamepatikana.

“Sekta binafsi ina imani kubwa na uongozi wa Rais Samia kwani katika kipindi cha mwaka mmoja na miezi kadhaa tumeona kukua kwa ushirikiano na kuaminiana kwa sekta za umma na binafsi,” alisema.

Alishauri kuwepo kwa sera tulivu na zinazotabirika za kodi pamoja na kuwepo pia mfumo unaoeleweka wa kodi.

Akimkaribisha Rais, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga alisema mpango wa kukuza uchumi lazima uende sambamba na kuimarisha uhusiano mzuri kati ya sekta za umma na binafsi ili kufikia malengo yaliyo kusudiwa.

“Tunapenda kuwa na ‘Displined and compliant private sector’ kwani na kuanzishwa kwa ‘Blue Print’ ni moja ya hatua zilizochukuliwa kuboresha mazingira ya kufanya biashara,” alisema Balozi Kattanga.

Aliwataka wafanyabiashara kujipanga kupokea wimbi kubwa la watalii na wawekezaji kutoka nje kutokana na mafanikio yaliyotokana na filamu ya Royal Tour.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad