HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, June 17, 2022

NAPE ASISITIZA ULINZI WA MTOTO DHIDI YA MATUMIZI YA TEHAMA

 

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (kulia) Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde (kushoto) wakikabidhi vifaa vya TEHAMA kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Chinangali leo Juni 16, 2022 jijini DodomaNa Mwandishi Wetu, Dodoma

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye ametoa rai kwa jamii ya kitanzania kumlinda mtoto dhidi ya matumizi ya intanenti yanayotokana na ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo ikitumika visivyo huchangia kuharibu mila na desturi za kitanzania kwa kufuata tamaduni za kigeni zinazokinzana na maadili ya kitanzania

Rai hiyo ameitoa Juni 16 jijini Dodoma, wakati akigawa vifaa vya TEHAMA katika shule ya Sekondari ya Chinangali ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika kwa Wizara anayoisimamia kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kuendelea kuwapatia watoto wa kitanzania nafasi ya kujifunza na kutumia TEHAMA

Waziri Nape amewataka wazazi na walezi kuadhimisha Siku ya mtoto wa Afrika kwa kutafakari, kutathmini na kukumbushana wajibu wa jamii ya kiafrika katika kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto, haki na maendeleo yao ili kulinda mila na desturi za kiafrika kwa vizazi vijavyo na kuwa na kesho bora na jamii inayojali na kurithisha maadili mema kwa vizazi vijavyo

Ameongeza kuwa, Serikali imewekeza kwenye miundombinu ya elimu ikiwa ni sehemu ya kumuandaa mtoto wa Kitanzania kuchukua dhamana ya kuijenga nchi, ikiwa ni pamoja na elimu ya matumizi ya TEHAMA ambayo hayaepukiki katika ulimwengu wa kidijitali.

“Kama ilivyo maisha bila moto haiwezekana lakini ukitumika vibaya unaweza kuleta madhara makubwa hata kupoteza maisha vivyo hivyo TEHAMA ikitumika vibaya inaweza kumuathiri mtoto wa kiafrika kujifunza tamaduni zisizofaa na matendo ya uovu kupitia mtandao hasa intaneti”, amezungumza Waziri huyo.

Amesema kuwa,“Wizara ninayoisimamia ina wajibu wa kuhakikisha kunakuwa na matumizi salama ya mtandao, lakini pia ni wajibu wa wazazi na walezi wakiwemo walimu kuwalinda watoto wetu dhidi ya changamoto zinazotokana na ukuaji wa TEHAMA na kwa kuchungulia nini watoto wanafanya kwenye mtandao na kutoona aibu kuwaeleza ukweli juu ya faida na hasara za ukuaji wa TEHAMA.”

Naye Naibu Waziri wa Kilimo na Mbunge wa Dodoma Mjijni, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa jamii inatakiwa kuimarisha ulinzi wa mtoto na kutoa fursa sawa kwa watoto wote ambapo kwa upande wa Serikali ya Tanzania chini ya Rais Samia tayari imefanya uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu ya elimu pamoja na kuongeza fursa ya watoto wote kupata elimu kwa kuhakikisha elimu inatolewa bure kuanzia elimu ya msingi mpaka kidato cha sita.

Akimwakilisha Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mkuu wa Idara ya Ununuzi na Ugavi wa mfuko huo, John Munkondya amesema kuwa ugawaji wa vifaa vya TEHAMA kwa shule za msingi na Sekondari ni moja ya mradi unaotekelezwa na mfuko huo kwa lengo la kukuza matumizi ya TEHAMA nchini.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Chinangali, Victor Salisali ameishukuru Serikali kwa kupeleka vifaa hivyo vya TEHAMA ambavyo vitasaidia kupanua wigo wa matumizi ya TEHAMA na kuimarisha mifumo ya utendaji wa walimu na wanafunzi.

“Ukitaka kuiona kesho ya Afrika, Kesho ya Tanzania unaangalia jinsi jamii zetu zinavyomjali na kumlinda mtoto kama kauli Mbiu inavyosema,”Maendeleo Endelevu 2030, Imarisha ulinzi na Fursa sawa kwa watoto”, Waziri Nape
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye akikaribishwa na wanafunzi wa shule ya Sekondari Chinangali alipofika shuleni hapo kukabidhi vifaa vya TEHAMA leo Juni 16, 2022 jijini Dodoma ikiwa ni siku ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika.
Baadhi ya wanafunzi na walimu wa Shule ya Sekondari Chinangali wakiwa kwenye picha na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye baada ya kukabidhi vifaa vya TEHAMA katika shule hiyo leo Juni 16, 2022 jijini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad