HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, June 1, 2022

MAKAMU WA RAIS ATEMBELEA KIWANDA CHA SCANIA NCHINI SWEDEN

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango leo tarehe 1 Juni 2022 ametembelea makao makuu ya kampuni ya utengenezaji wa magari ya Scania iliopo Stockholm nchini Sweden. Katika ziara hiyo Makamu wa Rais ameshuhudia teknolojia ya utengenezaji wa magari yanayotumia nishati ya gesi ikiwemo gesi inayotokana na taka ngumu inayotumiwa na kampuni ya utengenezaji magari ya Scania kwa lengo la kupunguza ongezeko la gesi joto duniani.

Makamu wa Rais ameshiriki mazungumzo na mkurugenzi wa teknolojia endelevu ya utengenezaji magari wa Kampuni ya Scania Jonas Strömberg pamoja na mkuu wa teknolojia endelevu ya usafirishaji wa kampuni ya Scania Fredrik Wijkander, mazungumzo yaliolenga kuongeza ushirikiano baina ya Tanzania na Kampuni hiyo.

Makamu wa Rais amesema Tanzania ipo tayari kwaajili ya ushirikiano na kampuni hiyo hasa katika vyuo vya ufundi vitakavyowezesha uhamilishaji wa teknolojia. Aidha ameikaribisha kampuni hiyo kushirikiana na wafanyabiashara pamoja na wawekezaji wa sekta ya usafiri waliopo Tanzania ili kueneza teknolojia ya matumizi ya nishati mbadala katika usafirishaji na kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira.

Kwa upande wake mkuu wa teknolojia endelevu ya usafirishaji wa Kampuni ya Scania Fredrik Wijkander amemshukuru Makamu wa Rais kwa kuitembelea kampuni hiyo na kuipongeza nchi ya Tanzania kwa kuendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na uharibifu wa mazingira. Amesema kampuni ya Scania inavutia  na mabadiliko mbalimbali yanayofanyika nchini Tanzania ikiwemo uboreshaji wa sekta ya uwekezaji ambayo inawapa hamasa ya kushirikiana na Tanzania katika sekta ya usafirishaji hususani usafiri wa mizigo na abiria.

Makamu wa Rais yupo nchini Sweden kuhudhuria mkutano wa umoja wa Mataifa wa Stockholm +50 wenye dhumuni la  kuchochea utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (Ajenda 2030) hususani katika upande wa mazingira na kujadili namna ya kurejesha uchumi endelevu katika kukabiliana na  janga la Uviko 19.

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akisalimiana na Mkurugenzi wa Teknolojia endelevu ya utengenezaji magari wa Kampuni ya Scania Jonas Strömberg wakati alipowasili katika ofisi za Kampuni hiyo zilizopo Stockholm nchini Sweden leo tarehe 1 Juni 2022.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akisikiliza maelezo kutoka muongoza watalii wa makumbusho maalum ya kampuni ya utengenezaji magari ya Scania Charlotte Gelotte wakati alipotembelea makumbusho hiyo iliopo makao makuu ya kampuni ya Scania, Stockholm  nchini Sweden leo tarehe 1 Juni 2022.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akitazama moja ya  injini inayotumia nishati ya gesi iliotengenezwa na kampuni ya Scania yenye makao makuu yake Stockholm nchini Sweden  wakati alipotembelea  makumbusho ya kampuni hiyo  leo tarehe 1 Juni 2022.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa mkuu wa teknolojia endelevu ya usafirishaji wa Kampuni ya Scania Fredrik Wijkander  wakati alipotembelea  Makao Makuu ya ofisi za Kampuni hiyo iliopo Stockholm nchini Sweden leo tarehe 1 Juni 2022.

 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad