Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor
Mpango leo tarehe 2 Juni 2022 ameshiriki mkutano wa Umoja wa Mataifa wa
Stockholm +50 unaoendelea nchini Sweden. Katika mkutano huo, viongozi
kutoka mataifa mbalimbali duniani pamoja na wawakilishi wa jumuiya za
kimataifa wametoa ahadi pamoja na mapendekezo mbalimbali ya namna ya
kukabiliana na uharibifu wa mazingira duniani.
Akizungumza
katika mkutano huo, Makamu wa Rais Dkt. Mpango amesema ili kuhakikisha
dunia inakua salama kwa viumbe wote wanaoishi, hakuna budi kutekeleza
kikamilifu makubaliano mbalimbali ya kimataifa ya kukabiliana na athari
za uharibifu wa mazingira yaliofanyika maeneo mbalimbali duniani kama
vile Rio de Jeneiro, Paris, Kyoto pamoja na Glasgow. Amesema
kinachohitajika ni utayari wa kisiasa pamoja na jitihada za pamoja
katika kukabiliana na changamoto hizo ambazo zinasababishwa na shughuli
za binadamu.
Aidha Makamu wa Rais amesema Tanzania imefanya
jitihada mbalimbali katika kupambana na uharibifu wa mazingira ikiwemo
kulinda misitu ya asili pamoja na juhudi za kitaifa za upandaji miti
huku ikienda sambamba na kuhifadhi kilometa za mraba 307,800 ambazo ni
sawa na asilimia 32.5 ya eneo lote la nchi kwaajili ya Hifadhi za Taifa
pamoja na misitu.
Makamu wa Rais amewakaribisha wawekezaji
kuwekeza nchini Tanzania katika teknolojia rafiki kwa mazingira ikiwemo
teknolojia zinazoweza kubadili taka kuwa nishati ya gesi na mbolea. Pia
amawaalika watafiti kutoka mataifa yalioendelea kushirikiana na
makampuni pamoja na watafiti wa ndani nchini Tanzania kwa kuendeleza
teknolojia rahisi na rafiki kwa mazingira katika kutumia nishati ya jua
na upepo iliopo nchini Tanzania.
Halikadhalika Makamu wa Rais
amesema pamoja na Tanzania kuchukua hatua mbalimbali katika kukabiliana
na uharibifu wa mazingira bado suala hilo lipaswa kupewa kipaumbele na
mataifa yote kwani juhudi za Tanzania pekee hazitoweza kukabiliana na
changamoto hiyo duniani. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.
Philip Isdor Mpango akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali
waliohudhuria ufunguzi wa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Stockholm +50
unaoendelea mjini Stockholm nchini Sweden leo tarehe 2 Juni 2022.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor
Mpango akihutubia katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Stockholm +50
unaoendelea mjini Stockholm nchini Sweden leo tarehe 2 Juni 2022.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor
Mpango akishiriki mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Stockholm +50
unaoendelea mjini Stockholm nchini Sweden leo tarehe 2 Juni 2022.
No comments:
Post a Comment