HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, June 30, 2022

MAKAMU WA RAIS AFANYA MAZUNGUMZO NA RAIS WA URENO

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Ureno Mheshimiwa Marcelo Rebelo de Sousa, mazungumzo yaliofanyika Ikulu ya Ureno mjini Lisbon.


Katika mazungumzo hayo viongozi hao wamejadili namna ya kuimarisha zaidi ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Ureno hususani katika sekta ya uchumi wa buluu kwa kutumia rasilimali za bahari kwa kuzingatia Ureno imepata maendeleo zaidi katika sekta hiyo.

Makamu wa Rais amemueleza Rais wa Ureno adhma ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza uchumi wa buluu ikiwemo mikakati ya kutumia vema bahari na rasilimali zake. Amesema Tanzania imejaaliwa kuwa na ukanda mrefu wa pwani wa takribani kilomita 1,450 na Ukanda wa Kiuchumi wa Kipekee unaofikia kilomita za mraba 223,000 hivyo ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili utakua na manufaa zaidi.

Pia Makamu wa Rais amesema Tanzania imeweka mikakati ya kujenga bandari ya Uvuvi katika bahari ya Hindi pamoja na ziwa Victoria na Tanganyika itakayochangia katika kuongeza mapato katika sekta hiyo.

Kwa upande wake Rais wa Ureno Mheshimiwa Marcelo Rebelo de Sousa amesema Ureno ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kujenga bandari ya uvuvi itakayosaidia Tanzania kunufaika zaidi kupitia rasilimali za bahari na kuimarisha uchumi wa buluu.

Halikadhalika Rais Marcelo ameongeza kwamba Ureno ipo tayari kushirikiana na kuhakikisha Tanzania inapiga hatua za kimaendeleo katika uchumi wa buluu pamoja na kukuza sekta ya biashara na uwekezaji.

Makamu wa Rais yupo nchini Ureno kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Pili wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uhifadhi wa Bahari na Rasilimali zake wenye lengo la kuhamasisha juhudi za Mataifa katika kufanikisha utekelezaji wa Lengo la 14 la Maendeleo Endelevu.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Rais wa Jamhuri ya Ureno Mheshimiwa Marcelo Rebelo de Sousa kabla ya mazungumzo yao yaliofanyika Ikulu ya Ureno mjini Lisbon.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akifanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Ureno Mheshimiwa Marcelo Rebelo de Sousa, mazungumzo yaliofanyika Ikulu ya Ureno mjini Lisbon.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akimuonesha zawadi mbalimbali kutoka Tanzania Rais wa Jamhuri ya Ureno Mheshimiwa Marcelo Rebelo de Sousa, mara baada ya mazungumzo yao yaliofanyika Ikulu ya Ureno mjini Lisbon.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Jamhuri ya Ureno Mheshimiwa Marcelo Rebelo de Sousa, mara baada ya mazungumzo yao yaliofanyika Ikulu ya Ureno mjini Lisbon.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad