HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, June 22, 2022

CMSA YAKUTANA NA WADAU KUJADILI MPANGO MKAKATI KUENDELEZA SEKTA YA FEDHA

 

 KATIKA kuhakikisha ukuaji wa sekta ya fedha nchini Mamlaka ya Masoko na Mitaji ya Dhamana (CMSA,) imekutana na  wadau katika sekta ya masoko ya mitaji  pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango na kujadili utekelezaji wa mpango mkakati wa kuendeleza sekta ya fedha hususani katika masoko ya mitaji. 

 Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko na Mitaji ya Dhamana (CMSA,) Nicodemus Mkama amesema mkutano huo umewakutanisha na wadau mbalimbali zikiwemo benki na taasisi ambazo zimepata leseni kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji, soko la hisa pamoja na soko la bidhaa na wamekutana na kujadili mpango mkakati wa kuendeleza sekta ya fedha.

Amesema katika mkutano huo wamejadili bidhaa mpya ambazo zitatolewa katika masoko ya mitaji zitakazowesha sekta binafsi na Umma kupata fedha zitakazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta hizo.

''Kampuni mbalimbali, Serikali zitaweza kutumia bidhaa katika masoko ya mitaji kuweza kupata fedha zitakazotumika kutekeleza miradi mbalimbali yenye tija kwa jamii.'' Amesema.

Mkama amesema kuwa bidhaa hizo ni pamoja na kuuza hisa kwa kampuni na kutoa hati fungani ambazo ni hati fungani za Serikali Kuu na hati fungani ambazo zitatolewa na Halmashauri za mitaa na majiji, Manispaa na Miji ambapo wataweza kupata fedha za kutekeleza miradi ambayo inaweza kujiendesha kibiashara na kuweza kupunguza mzigo kwa Serikali Kuu.

Pia amesema, utekelezaji wa mpango mkakati huo unategemewa kutekelezwa kwa ufanisi kwa kipindi cha miaka mitatu  ni pamoja na kutoa elimu kwa Umma juu ya faida na fursa zinazopatikana katika masoko ya mitaji na kuna mpango mkakati wa kuhakikisha watu wote mijini na vijijini wanaweza kufikiwa.

''Katika kufanikisha hili kuna programu  mbalimbali ambazo zimewekwa katika mpango mkakati kwa kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa, na  kuna mpango wa kuhakikisha vijana na makundi maalumu ya wanawake na watu wenye walemavu wanafikiwa.... pia kuna programu maalum zitakazofanyika katika vyuo vikuu na taasisi ya elimu ya juu kwa kuhakikisha kwamba  uelewa unajengwa katika makundi yote na wataalam wakiwemo manesi, wanasheria, wahasibu wanafikiwa, tunaamini tutawafikia asilimia 85 watanzania ndani ya miaka mitatu iyajo ili kujenga uelewa na fursa zinazopatika katika masoko ya mitaji kwa wananchi wengi zaidi." Amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya FIMCO Ivan Tarimo amesema mkutano huo ni fursa ya CMSA kwa kukaa na wadau wake wakubwa na kujadili mpango mkakati katika kuyafikia malengo yao kiufanisi kwa miaka mitatu iyajo.

Amesema ushiriki wa masoko ya mitaji kwa watanzania bado ni mdogo licha ya kuwa na fursa lukuki kiuchumi na kupata kipato, na kuwataka watanzania kuendelea kujifunza kuhusu masoko ya mitaji.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko na Mitaji ya Dhamana (CMSA,) Nicodemus Mkama akizungumza wakati wa kikao hicho na kueleza kuwa mkutano huo umewakutanisha na wadau mbalimbali zikiwemo benki na taasisi ambazo zimepata leseni kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji, soko la hisa pamoja na soko la bidhaa na wamekutana na kujadili mpango mkakati wa kuendeleza sekta ya fedha. Leo jijini Dar es Salaam.

 Majadiliano yakiendeleea.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad