HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 16, 2022

WAZIRI BASHE AZINDUA BODI TUME YA TAIFA YA UMWAGILIAJI,AIPA MALENGO YA KIMKAKATI SEKTA YA UMWAGILIAJI.

Waziri wa Kilimo Mhe.Hussein Bashe amezindua Bodi ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji jijini Dodoma na kuwataka wajumbe wa bodi hiyo kutumia taaluma zao na uzoefu walionao kazini kuisimamia na kuishauri Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika kutekeleza majukumu yake.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe, Bashe ameitaka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kutengeneza Kanzidata inayoonyesha yalipo maeneo yote yanayofaa kwa kilimo cha Umwagiliaji nchini ambayo ni Hekta Milioni 29, kuandaa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa maeneo yote yafaayo kwa kilimo cha Umwagiliaji ikiwemo ukanda wa Mto Rufiji, ukanda wa ziwa Victoria kuanzia Mwanza hadi Kagera, Ziwa Tanganyika, Ziwa Rukwa,Mto Ruvuma na bonde la Kilombero pamoja na taarifa ya mazao yanayostawi katika maeneo hayo ambapo pia amesisitiza kuwa maeneo hayo yahifadhiwe kisheria kuwa maeneo ya kilimo cha Umwagiliaji kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo.

Mhe, BASHE amesema Wizara yake itazitumia nafasi 800 zilizotolewa na Serikali kuajiri wahandisi 143 wa Umwagiliaji watakao huduma katika Ofisi za Wilaya zitakazofunguliwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika Mwaka wa fedha 2022 - 2023 ambao majukumu yao pamoja na mambo mengine ni kusimamia Skimu za Umwagiliaji.

“Tunafungua Ofisi kila Wilaya ili tuweze kusimamia kikamilifu Skimu tunazojenga,tumekuwa tukijenga Skimu za Umwagiliaji alafu tunaacha zinasimamiwa na Chama cha Ushirika tukitaraji kinasimamia vizuri, wanalima wao, wanavuna wao Banio likiharibika wanakuja Wizarani kuomba fedha za kujenga Banio”

Aidha Mhe, Bashe ameiagiza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kuweka Wasimamizi katika Skimu zote 1,097,000 nchi nzima ambazo Serikali imewekeza kwa kujenga Miundombinu kwa lengo la kusimamia zoezi la ukusanyaji wa ada na tozo za Umwagiliaji kwa mujibu wa Sheria.

“Kwa mujibu wa takwimu, tunapoteza zaidi ya shilingi Bilioni miamoja kila Mwaka kwa kushindwa kukusanya ada na tozo fedha ambazo zingesaidia kutunisha mfuko wa Umwagiliaji na kuwezesha Tume kukopa Mabilioni ya fedha kwaajili ya kuwekeza kwenye miradi mikubwa ya Umwagiliaji”(megar project)

Akizungumza kwa niaba ya Bodi, Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Prof. Henry Mahoo amewataka Wajumbe wa Bodi na Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kufanya kazi kwa kujituma ili kufikia malengo yaliyowekwa na serikali.

“Tutatumia mbinu zozote kuhakikisha haya malengo yanafikiwa”

Kwaupande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Raymond Mndolwa ameahidi kuisimamia Taasisi anayoiongoza kwa weledi kufikia matarajio ya wananchi hususani katika Kilimo cha Umwagiliaji.


Picha ya pamoja kati ya Waziri wa Kilimo, Wajumbe wa bodi ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.Waziri wa Kilimo Hussein Bashe wa saba kutoka kushoto.

Kulia kwa Mhe. Waziri Bashe ni Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Prof. Henry Mahoo, na kushoto kwa Waziri Mhe, Bashe ni Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw, Raymond Mndolwa.

Waziri wa Kilimo Mhe.Hussein Bashe akifafanua jambo kwenye kikao hicho

Wajumbe wa Bodi ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika kikao cha pamoja na Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe jijini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad