HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 20, 2022

Wazazi watakiwa kutambua jukumu lao katika kuwasaidia watoto wafaulu

  WAZAZI watakiwa kutambua jukumu lao katika kuwasaidia watoto wafaulu kwani kazi ya kufundisha mtoto haiishii kwa walimu darasani.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwanamke, Initiatives Foundation inayoshughulika na masuala ya kuimarisha elimu ya kawaida na mafunzo ya amani Fatma Mwassa, alisema jana kuwa amegundua kuwa changamoto kubwa iliyopo ni wazazi kutotambua majukumu yao.

Mwassa alisema hayo wakati akitoa sehemu ya msaada wa vifaa vya shule na mahitaji muhimu ya kila siku vyenye thamani ya jumla ya shilingi millioni 11 kwa wanafunzi wa Chuo cha Maendeleo ya wananchi cha Kilwa Masoko jana ambao wanatokea Visiwani Unguja.

“Kazi ya kufundisha haiishii kwa mwalimu darasani, mwalimu analo jukumu, mwanafunzi, lakini na sisi wazazi tunalo jukumu la kuhakikisha watoto wanasoma.” Alisema Mwassa.

Alitolea mfano kwa wanafunzi wanaosoma katika chuo cha maendeleo ya wananchi kilichopo Kilwa Masoko mkoani Lindi kupitia program ya wanafunzi waliokosa fursa ya kumaliza elimu ya sekondari alisema wazazi wamekuwa wakipiga simu wakiwataka watoto wao kurudishwa pale tu watoto wao wanapowaeleza kuwa wamewakumbuka.

“Mfano Wazazi hata hawa waliokuja hapa mtoto akipiga simu tu kwa mama mimi nakumbuka nyumbani mama anatupigia mwanangu arudi arudi, hakuna amisha ya hivyo lazima watoto waweko shule wasaidiwe wasome, wafundishwe kujitambua, sisi wazazi leo tupo duniani kesho hatutakuwepo watoto wanatakiwa waendelee kuishi, wataishije kama hatukuwaandaa kuishi vizuri kwa hiyo wazazi lazima tutimize wajibu wetu” alisema Mwasa.

Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundations imepeleka jumla ya wanafunzi 30 katika vyuo vya maendeleo ya wananchi vya Kilwa Masoko na Kisarawe kupitia mpango wa serkali wa elimu ya sekondari kwa walioshindwa kumaliza kidato cha nne kwa sababu mbalimbali zikiwemo mimba.

Alisema Taasisi yake ambayo inafanya shughuli zake zaidi Zanzibar kwa kushirikiana na wizara ya elimu ya Zanzibar imeiona fursa katika vyuo vya maendeleo ya wananchi ambayo ilitangazwa na Rais.

Alisema serikali imefanya juhudi kubwa ya kuvikarabati na kutoa fursa na msamaha wa malipo yote ili vijana na wasichana walioshindwa kumaliza kidato cha nne kwa kupata mimba au kwa sababu mbali mbali waendelee na masomo yao hivyo taaisisi hiyo ikaona inayo kila sababu ya kuitumia hiyo fursa.

Wapo wanaosoma fani ya umeme na wengine fani ya ufundi.

Alisema lengo ni wanafunzi hao wapate ujuzi ambao utawawezesha kujiajiri lakini mwisho kutengeneza ajira kwa vijana wote ambao tumewawezesha kuja kupata mafunzo katika vyuo hivi.

Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Karibu Tanzania Organization, (KTO), Maggid Mjengwa ambayo inafanya kazi na vyuo vya maendeleo ya wananchi vipatavyo 54, Tanzania alisema kuwa changamoto kubwa iliyopo ni uelewa wa mpango wa elimu ya sekondari kwa wanafunzi ambao hawakumaliza elimu hiyo.

“Sio wote wanaoelewa kwamba programu hii inaendeshwa kwenye vyuo vyote 54 inagharamiwa na serikali, unachotakiwa wewe ni nauli yako na vitu vya kujikimu tu, ni fursa ya kipekee, ni uelewa” alisema Maggid.

Alisema katika jamii hata wenye elimu hawafatilii masuala haya ili kuwafahamisha wale wasioelimika juu ya uwepo wa mpango huo katika vyuo vya maendeleo ya wananchi.

Alisema taasisi yake ya KTO ina programu tatu ambazo ni fursa ya elimu ya makuzi na malezi kwa mtoto na elimu haina mwisho ambazo zote wanashirikiana na vyuo hivyo 54 ambavyo viko chini ya wizara ya elimu, sayansi na teknolojia.

Chuo cha maendeleo ya wananchi cha Kilwa Masoko ni moja wapo ya vyuo vilivyopokea awamu ya kwanza ya wanafunzi kutoka Zanzibar chini ya mpango wa elimu ya sekondari kwa waliokosa fursa ya kumaliza.

Taasisi ya KTO imekuwa ikishirikiana na Mwanamke Initiative Foundation katika kutekeleza mpango huo wa elimu ya sekondari kwa ambao hawakumaliza.

Alisema Katika vyuo vyote 54 tuna wanachuo 2600 kwa mwaka huu ambao tayari wamejiunga na mafunzo hayo ya miaka miwili.

Mwanakombo Mohamed Ally mmoja wa wanafunzi wanaosoma chuoni hapo alisema kuwa anashukuru kwa msaada waliopatiwa.
Picha ya pamoja
Wanafunzi wa Chuo cha maendeleo ya wananchi cha Kilwa Masoko mkoani Lindi kutokea Zanzibar ambao wako chuoni hapo kupitia mpango wa elimu ya sekondari kwa walioshindwa kumaliza kutokana na sababu mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwanamke Initiatives foundation, Fatma Mwasa mwenye buibui jeusi na mtandio wa njano.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad