HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 27, 2022

WANAWAKE 16 WANAOVUNJA SHERIA WAKAMATWA DAR

 

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini, akizungumza na waandishi wa habari leo, Mei 27, 2022 jijini Dar es Salaam wakati wa kutoa taarifa ya kukamatwa kwa wanawake  16 ambao wanajihusisha na vitendo viovu na kuvunja sheria za nchi na kuvunja mila na Desturi za kitanzania. Kulia ni Naibu waziri Maendeleo ya jamii, jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis.
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar Es Salaam, ACP, Muliro Jumanne Muliro akizungumza wakati wa kutoa utekelezaji wa suala la kuwakamata wanawake na watoto 16 ambao wanajihusisha na vitendo viovu nchini.

Na Avila Kakingo, Michuzi TV
WANAWAKE 16 wakamatwa kwa kucheza Vigoma na Kibao kata huku wakibinua vijora na Madira na kubaki watupu wanapokuwa wanacheza ngoma hizo katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar Es Salaam.

Wachezaji hao ni wanawake na Mabinti ambao wamekuwa wakicheza nyakati za usiku bila staha.

Wanawake hao waliokamata ni katika maeneo ya Mwananyamala, Kinondoni, Mkwajuni, Tandale, Sinza, Magomeni na Buza.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mei 27, 2022 jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini amesema kuwa wanaofanya hivyo wanakiuka kabisa sheria, Kanuni, Mila, desturi na maadili mema ya watazania.

Amesema kuwa Watu hao bila chembe ya woga wala aibu wamekuwa wakitangaza matendo maovu na kuyaweka katika mitandao ya kijamii huku wakihamasisha wengine waige kufanya kama wao.

Sagini ametoa onyo kali kwa mtandao unaoendesha shughuli hizo zinazokiuka maadili na sheria za nchi huku zikichochea vitendo vya uasherati, udhalilishaji utu na kushusha heshima ya mwanamke.

Amesema kuwa vitendo hivyo huchochea kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza kwa njia ya kujamiana na mimba zisizotarajiwa pamoja na ukatili dhidi ya watoto wanaotumikishwa kucheza ngoma hizo.

Amesema uchunguzi uliofanywa na vyombo vya dola umebaini kuibuka kwa baadhi ya wanawake wanaofundisha kufanya matendo ya ngono kwa kutumia vitu hatarishi kama chupa za bia na soda, matango, Mahindi ya kuchoma na ndizi huku baadhi ya wengine wameunda makundi kwenye mtandao wa WHATSAP ili kuweka picha zao za utupu na wengine kuweka kwenye mitandao mingine ya kijamii.

Amesema uchunguzi huo umebaini kuwa wanawake na mabinti hao wanaonesha kukubuhu kufanya vitendo hivyo ikiwa ni pamoja na kuwasafirisha kwenda ughaibuni kwaajili ya kuwatumikisha katika biashara ya ukahaba jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Aidha vyombo vya dola na mamlaka vinaendelea kukamilisha taratibu za kisheria ili wafikishwe Mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.

Sagini ametoa wito kwa jamii wanaodhani wanaweza kuondoa umasikini unawakabili kwa kufanya matendo yasiyo ya kimaadili kuachana nayo mara moja.

Kwa upande wake Naibu waziri Maendeleo ya jamii, jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis ametoa onyo kwa wale ambao wanatekeleza vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto.... "Waache Mara moja endapo akikamatwa tutawachukulia hatua kali za kisheria."

Hata hivyo amewaomba wadau wa maendeleo ya Mwanamke na watoto nchini kuendelea kutoa elimu ili jamii iachane na ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa kutumia vyombo vya habari, Magari ya matangazo mitaani pamoja na makongamano.

Licha ya hilo jamii imetakiwa kuhamasika kutoa taarifa za vitendo vya ukatili dhidi ya watoto pindi wanapoona dalili za matukio yanayomdhalilisha au kunyima haki mtoto.

Pia jamii imetakiwa kupiga simu namba 116 ili kutoa taarifa dhidi ya ukatili wa watoto ili kuunganishwa na watoa huduma zinazostahili kwaajili ya kupata msaada zaidi.

Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Naibu waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar Es Salaam, ACP, Muliro Jumanne Muliro amesema kuwa watafuatilia kwa kina kwa wale wote wanaojihusisha na vitendo viovu na kuvunja sheria za nchi.

Kwa upande wa waliokamatwa ACP Muliro amesema kuwa waliokamatwa watachukuliwa sheria kali na kufikishwa Mahakamani ikiwa ni pamoja na kusimamia kwa karibu kesi hiyo.

"Tutasimamia kwa karibu kesi hii mpaka tuone wanachukuliwa hatua za kisheria na iwe fundisho kwa wengine na sio fasheni kwa watu wengine ambao wanatamani kufanya vitendo hivyo viovu." Amesema ACP Muliro.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad