Hii ifike Dar.... Wanaovaa vimini, mlegezo kulipa faini mifuko mitano ya saruji - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 30, 2022

Hii ifike Dar.... Wanaovaa vimini, mlegezo kulipa faini mifuko mitano ya saruji

 

*Wanaovaa nguo fupi, mlegezo watungiwa sheria, atakayekamatwa kulipa faini mifuko 5 ya saruji

Na Amiri Kilagalila,Njombe
KATIKA jambo ambalo sio la kawaida, kumeibuka mjadala mzito kwa baadhi ya wananchi wa wilaya ya Makete mkoani Njombe mara baada ya baadhi ya maeneo yenye mamlaka kiutawala kutunga sheria ndogo zinazotajwa kuwa ni maumivu kwa wananchi.

Hali hiyo imeibuka mara baada ya uongozi wa kata ya Tandala wilayani humo kupitia vikao vyao vya kata (KAMAKA) kutunga sheria ndogo ya kuwakamata wanawake wanaovaa nguo fupi,nguo zinazochora maumbile yao pamoja na wanaume wanaovaa suruali zikiwa chini ya makalio (Mlegezo) na kuwapiga faini ya mifuko mitano ya saruji inayokwenda kutumika kwenye ujenzi wa miradi ya kata.

Mtendaji wa kata hiyo bwana Maximilian Msigwa amesema uamuzi huo umefanyika ili kudhibiti mavazi yasiyofaa katika jamii na kubainisha kuwa mpaka sasa umekwishafanyika msako na tayari baadhi ya watu ambao idadi yao haijafahamika wakiwa wamekwishakamatwa katika utekelezaji wa sheria hiyo.

“Tumekuwa na mabinti wengi wanaokuja kutafuta riziki sasa wanakuja kutafuta kwa njia tofauti sasa wanapokosea lazima tuwanyooshe warudi kwenye mstari,akiweza kukamatwa analipishwa mifuko mitano ya saruji kwa ajili ya ujenzi kwasababu tuna ujenzi wa shule yetu ya msingi Tandala”alisema Maximilian Msigwa

Msigwa amesema kabla ya kuanza kwa zoezi hilo wamiliki wa sehemu za starehe na wananchi kwa ujumla walipewa taarifa kwa ajili ya kujirekebisha kabla sheria hiyo haijaanza kufanya kazi na kuongeza kuwa wote wanaoshindwa kulipa gharama hizo kumewekwa utaratibu wa kuzungumza na viongozi wao wa vijiji ili kuwatambua na kuwarudishwa kwao.

Lususu Mbilinyi na Maulo Sanga ni baadhi ya wananachi wa kata ya Tandala ambao wamepongeza uamuzi huo huku wakitaka sheria hiyo isimamiwe ipasavyo katika kulinda maadili ya Mtanzania.

Maulo amewataka mafundi kushona wasikubali kushona nguo fupi na zisizofaa katika jamii kwani zinaweza kuwaharibia kazi zao na kuwa miongoni mwa wanaosababisha suala hilo kuzidi kukua nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad