HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, April 6, 2022

WAFANYAKAZI WA MIGODI YA MAKAA YA MAWE WAANZA KUCHUNGUZWA KIFUA KIKUU


Baadhi ya wafanyakazi wa mgodi wa makaa ya mawe wa Ruvuma Coal wakimsikiliza Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa mkoa wa Ruvuma Dkt Xavier Mbawala(hayupo pichani)alipokuwa akitoa elimu ya ugonjwa wa kifua kikuu kwa wafanyakazi hao iliyokwenda pamoja na uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa huo. 

Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa mkoa wa Ruvuma Dkt Xavier Mbawala kushoto,akimsikiliza mkazi wa kijiji cha Mkako Halmashauri ya wilaya Mbinga ambaye hakufahamika jina lake mara moja wakati wa kampeni ya kupambana na ugonjwa wa kifua kikuu inayoendelea katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Ruvuma.
Baadhi ya wafanyakazi wa mgodi wa Ruvuma Coal uliopo kata ya Ruanda wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wakiwasili kwenye kampeni ya mapambano ya ugonjwa wa kifua kikuu kwa wafanyakazi hao iliyoendeshwa na Hospitali ya mkoa Ruvuma kupitia kitengo cha kifua kikuu chini ya ufadhili wa wadau wa maendeo ya afya ikiwamo shirika lisilo la kiserikali la MDH.

Na Muhidin Amri, Mbinga
WIZARA ya Afya kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo shirika lisilo la Kiserikali la MDH, Amref health Africa, kwa ufadhili wa mfuko wa Dunia imeanza kutoa huduma ya uchunguzi wa maambukizi ya ugonjwa wa kifau kikuu kwa kutumia kliniki tembezi(Mobile Clinik) kwa wafanyakazi wa migodi ya makaa ya mawe wilayani Mbinga.

Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa Hospitali ya mkoa wa Ruvuma Dkt Xavier Mbawala alisema,mpango huo utahusisha maeneo yote ya migodi ya makaa ya mawe na kwenye machimbo ya madini mengine.

Kwa mujibu wa Dkt Mbawala,hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba wafanyakazi wa migodi wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa kifua kikuu kutokana na kazi wanazofanya kwani wasipochukua tahadhari kuna uwezekano wa kuvuta vumbi linalokwenda moja kwa moja kwenye mapafu na kupata ugonjwa wa Silicosis.

Alisema,ugonjwa wa Silicosis unasababisha mwili kuwa dhaifu hivyo ni rahisi mtu mwenye ugonjwa huo kuwa katika hatari ya kupata ugonjwa wa kifua kikuu,jambo linaloweza kusababisha kushindwa kushiriki kazi za maendeleo na kupoteza nguvu kazi ya Taifa.

Alisema, katika kampeni hiyo wanatoa elimu kuhusu kifua kikuu,kufanya uchunguzi,namna ya kuchukua tahadhari ili wasipate kifua kikuu na wale wanaobainika kuambukizwa ugonjwa huo wanaanzishiwa matibabu yanayotolewa bure.

Alisema, kampeni hiyo ni maalum kwa wafanyakazi wa migodi,machimbo ya madini na wananchi wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka migodi ili kuwaepusha na uwezekano wa kupata ugonjwa huo.

Ameshauri, wafanyakazi wa migodi ya makaa ya mawe na wachimbaji wadogo wa madini kuchukua tahadhari ikiwamo kuvaa barakoa wanapokuwa kazini ili kuepuka hatari ya kupata kifua kikuu.

Alisema,kampeni hiyo ni endelevu na itafanyika kila baada ya miezi mitatu kwa kutembelea migodi na machimbo mbalimbali ili kuwanusuru wachimbaji na jamii kwa jumla.

Kwa upande wake Afisa Usalama na Afya sehemu ya kazi wa kampuni ya Ruvuma Coal inayochimba makaa ya mawe katika kijiji cha Paradiso kata ya Rwanda James Mungo, ameipongeza Serikali na wadau hao kupeleka huduma ya uchunguzi wa kifua kikuu kw wafanyakazi wa migodini.

Alisema, hatua hiyo ni nzuri kwani licha ya kuokoa maisha ya wafanyakazi na wananchi, na itasaidia wafanyakazi wa migodi kutambua kwamba licha ya kuwepo katika sekta binafasi, lakini Serikali yao ya awamu ya sita inawatambua na kuwajali kwa kuwafikishia huduma muhimu.

Ameiomba serikali kupitia wizara ya afya, kupeleka huduma hiyo mara kwa mara katika migodi ili kunusuru maisha ya watu wanaofanya shughuli zao katika migodi na wale wanaoishi kwenye vijiji vinavyozungukwa shughuli za migodi.

Meneja mpango wa Shirika lisilo la Kiserikali la MDH linaloshughulika na mapambano dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu mkoa wa Ruvuma Dkt Veronica Asenga alisema,kampeni hiyo imefanyika kwa siku tatu ambapo wametoa elimu ya kifua kikuu na huduma ya uchunguzi kwa wafanyakazi wa mgodi wa makaa ya mawe wa Ruvuma Coal na vijiji vya Paradiso, Mkeso na Amani Makolo vilivyopo kata ya Ruanda.

Aidha alisema, wanatumia Kliniki tembezi ili kuwafikia wagonjwa wa kifua kikuu wanaoishi maeneo ya pembezoni ambao hawajapa nafasi ya kwenda katika vituo vya afya na Hospitali kwa ajili ya kupata matibabu.

Alisema, wakati wote wanashirikiana na serikali za vijiji,mitaa,Halmashauri za wilaya na Serikali za mikoa katika kutokomeza ugonjwa huo ambao unatajwa kuwa kati ya magonjwa 10 Duniani yanayoongoza kuuwa watu wengi.

Dkt Asenga,ameitaka jamii kuondoa mila potofu ya kuchanganya ugonjwa huo na imani za kishirikina, badala yake kutambua kuwa kifua kikuu sio ugonjwa wa kurogwa na unatibika kwa mgonjwa kuanza matibabu yanayotolewa bure katika zahanati,vituo vya afya na Hospitali zote hapa nchini.

Mkazi wa kijiji cha Amani makolo Antony Mapunda, ameishukuru Serikali kwa uamuzi wa kufikisha huduma hiyo kwa wananchi ambao hawana uwezo wa kwenda Hospitali kufanya uchunguzi wa afya zao na kupata matibabu.

“nawashukuru sana wataalam wetu kutuletea huduma hii hapa kijiji,sisi watu tunaoishi katika vijiji vinavyozungukwa na machimbo ni rahisi sana kupata magonjwa mbalimbali ikiwamo TB”alisema Mapunda

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad