HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, April 2, 2022

PAC YAKAGUA KITUO JUMUISHI CHA UTOAJI HAKI MOROGORO


Kaimu Mwenyekiti wa Kamati, Mhandisi Isack Kamwele (aliyeshika jembe) akipanda mti wa kumbukumbu mara baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kukagua jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Morogoro.*Yaridhishwa na Mradi huo
Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) jana tarehe 31 Machi, 2022 ilitembelea na kukagua jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Morogoro ambapo imeonyesha kuridhishwa na Mradi huo na kusema kuwa unaendana na thamani ya fedha iliyotumika.

Akizungumza kwa niaba ya Wajumbe wa Kamati hiyo, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati, Mhandisi Isack Kamwele amesema kuwa Mradi wa Ujenzi wa vituo sita vya Utoaji Haki nchini ikiwemo kituo cha Morogoro ni mradi wenye mafanikio kwa kuwa inaonyesha wazi kuwa fedha iliyotumika kwa ajili ya ujenzi wake imetumika kihalali kutokana na ubora wa majengo hayo.

“Tumekagua Kituo hiki cha Morogoro, na tulianza kukagua Vituo vya Temeke na Kinondoni Dar es Salaam, napenda kusema wazi kuwa tumeridhishwa na ujenzi wa majengo haya ambayo yanaonyesha thamani ya fedha iliyotumia na yana muonekano wa kimataifa,” alisema Mhandisi Kamwele.

Aidha Mhandisi Kamwele alifafanua kuwa kamati imekuwa jicho la Bunge katika kuhakikisha pesa inayotolewa na Serikali inaenda kwenye matumizi sahihi hivyo basi wameridhishwa na kazi nzuri iliyofanywa na Mahakama kwani thamani ya pesa inaonekana, “Nafurahi Value for Money unaiona, wabunge wote tunafikiri kazi imefanyika vizuri” aliongeza.

Mhandisi Kamwele alielezea kuwa uwepo wa vituo Jumuishi nchini umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza mrundikano wa mashauri mahakamani kwani hudumu zote zinapatikana katika jengo moja na hivyo kurahisisha mchakati wa upatikanaji wa huduma ya utoaji haki huku ikiondoa gharama na kuokoa muda.

Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania. Prof.Elisante Ole Gabriel amesema kuwa vituo Jumuishi vya utoaji Haki vimejengwa sita nchini na matarajio ni kujengwa vituo vipya tisa hadi kumi na mbili nchi nzima hii ikiwa ni jitihada inayofanywa na serikali kuhakikisha wanaboresha upatikanaji wa huduma ya haki kwa wananchi.

Akitoa shukrani zake kwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Prof.Ole Gabriel ameishukuru Serikali kwa kuwezesha ujenzi wa vituo hivyo na kuongeza kuwa lengo la Mahakama ni kuendelea kusogeza huduma ya haki katika maeneo yasiyokuwa na Mahakama ili huduma ya haki iweze kuwafikia wananchi popote walipo.

Aliongeza kuwa kuwepo kwa vituo hivyo kumepokelewa kwa namna chanya na wananchi kwa kuwa kiu ya huduma kama hii kwa wananchi ilikuwa ni kubwa.

“Sisi kama Mahakama tunaomba Watanzania wathamini jitihada zinazofanywa na Serikali sanjari na kutambua juhudi zinazofanywa na Mahakama katika kuhakikisha huduma ya utoaji haki inapatikana kwa wakati na bila vikwazo vya aina yoyote ile”alisema Mtendaji Mkuu.

Jengo la kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro lenye sakafu nne limegharimu Bilioni 9.13 ukiondoa gharama za Mkandalasi likiwa na ukubwa wa ‘Square meters’ 6178 na inaelezwa kuwa jengo hilo limemsogezea Mwananchi wa Morogoro huduma ambayo awali alilazimika kuifuata Dar es salaam hususani huduma za Mahakama Kuu.

Kabla ya ujenzi wa kituo hicho, Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro iliyokuwa ikitumika ilikuwa ikipokea watu mia moja kwa siku lakini mara baada ya uwepo wa kituo hiko sasa Mahakama imekuwa ikipokea watu zaidi ya 350 mpaka 400 kwa siku moja hii ni ishara kuwa muitikio wa watu na imani ya wananchi juu ya Mahakama yao imeongezeka.

Vituo hivyo vya hadhi ya kimataifa vyenye vifaa vya kisasa vya TEHAMA Vituo hivyo vimejengwa pia Dar es Salaam (Kinondoni &Temeke) Morogoro, Arusha, Dodoma na Mwanza.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania. Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyenyoosha mkono) akiwaonyesha Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Kanda ya Morogoro walipofika katika Kituo hicho jana tarehe 31 Machi, 2022 kwa ajili ya ukaguzi.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (waliosimama kushoto) wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) alipokuwa akitoa maelezo kuhusu Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Kanda ya Morogoro kilichokaguliwa na Kamati hiyo.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali wakiwa katika moja ya kumbi za Mahakama katika jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Kanda ya Morogoro.




Ukaguzi ukiendelea.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Mhe. Aida Kenani akichangia jambo wakati ya ukaguzi wa jengo la 'IJC' Morogoro.
Kulia ni sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania walioshiriki katika mapokezi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali.
Picha ya pamoja kati ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na baadhi ya Watumishi wa Mahakama. Aliyeketi katikati ni Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhandisi Isack Kamwelwe na wa pili kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.
Picha ya pamoja kati ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ( wa pili kushoto).

(Picha na Mary Gwera, Mahakama)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad