HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, April 2, 2022

MALALAMIKO YA UKIUKWAJI WA MAADILI KWA VIONGOZI YASHUGHULIKIWE KIKAMILIFU KWA MANUFAA YA TAIFA-Mhe. Jenista


Muonekano wa jengo la ofisi za makao makuu ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma linaloendelea kujengwa jijini Dodoma na Mkandarasi ambaye ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Menejimenti ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma alipokutana na Menejimenti hiyo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji na kukagua ujenzi wa Ofisi za makao makuu ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma jijini Dodoma. Kulia kwake ni Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi na kushoto kwake ni Mkurugenzi Idara ya Ujenzi Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mhandisi Loishorwa Likimaitare.
Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi, Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na Menejimenti hiyo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji na kukagua ujenzi wa Ofisi za makao makuu ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma jijini Dodoma.

Na James K. Mwanamyoto-Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ameielekeza Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kushughulikia malalamiko na tuhuma zinazowasilishwa na wananchi kuhusu Viongozi wa Umma wanaokiuka maadili ili kuwa na viongozi waadilifu wanaotekeleza majukumu yao kwa maendeleo ya taifa.


Mhe. Jenista ameyasema hayo leo alipokutana na Menejimenti ya Sekretarieti hiyo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji na kukagua ujenzi wa Ofisi za makao makuu ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma jijini Dodoma.


Mhe. Jenista amesema, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu mwenendo wa baadhi ya Viongozi wa Umma kwenye eneo la uadilifu, hivyo Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi ina jukumu kubwa la kuyapokea malalamiko hayo na kuyafanyia kazi ili viongozi wawe na maadili na miiko ya uongozi unaotakiwa.


“Mnapokea tuhuma zinazohusu ukiukwaji wa maadili ya viongozi, hivyo mna jukumu la kufanya uchunguzi ili kuthibitisha ukweli wa tuhuma hizo na kuzifanyia kazi kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na.13 ya Mwaka 1995,” Mhe. Jenista amesisitiza.


Aidha, Mhe. Jenista ameitaka Sekretarieti hiyo kutoa elimu ya uzingatiaji wa maadili kwa Viongozi wa Umma ili wasikiuke maadili na miiko ya uongozi kwa kutokuwa na uelewa.


“Katika kipindi hiki tujikite zaidi kutoa elimu ya uzingatiaji wa maadili ili viongozi wetu wa umma waelewe umuhimu wa kuzingatia maadili katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, hii inatokana na baadhi ya viongozi kukiuka maadili kwa kutokuelewa na hatimaye kujihusisha na vitendo vya ukiukaji wa maadili.” Mhe. Jenista amehimiza.


Amesema azma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan inamtaka kila Mtanzania ajifunze kutii sheria bila shuruti na kama ni kiongozi basi atii Sheria ya Maadili ya Viongozi bila kushurutishwa, hivyo suala ya utoaji wa elimu ya uzingatiaji wa maadili haliepukiki ili kuwa na uongozi unaozingatia utawala bora.


Kwa upande wake Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili wa Viongozi wa Umma, Mhe. Jaji Sivangilwa Sikalalilwa Mwangesi amezitaja kazi za msingi za Sekretarieti hiyo kuwa ni pamoja na kupokea matamko yanayotakiwa kutolewa na Viongozi wa Umma kwa mujibu wa Katiba na Sheria, kupokea malalamiko na tuhuma za ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kuanzisha na kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma za ukiukwaji wa maadili na kufanya uhakiki wa Matamko na Rasilimali na Madeni yanayotolewa na Viongozi wa Umma kwa mujibu wa Sheria.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad