HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, April 25, 2022

Kukosekana kwa mifumo imara inayotoa fursa sawa za upatikanaji wa haki za msingi kwa wanawake

 IMEELEZWA kuwa kukosekana kwa mifumo imara inayotoa fursa sawa za upatikanaji wa haki za msingi kwa wanawake na wanaume katika jamii nyingi nchini ndio chanzo cha wanawake wengi kukosa uwezo wa kusimama kudai haki zao na kushiriki kikamilifu katika ngazi mbalimbali za maamuzi.


Hayo yalibainishwa na wadau wa asasi za kiraia kisiwani Pemba wakati wa mkutano wa asasi hizo kujadili changamoto na vikwazo vinavyokwaza upatikanaji wa haki za wanawake ulioandaliwa kwa mashirikiano ya taasisi za Pemba Gender Advocacy and Environmental Organization (PEGAO), Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, (TAMWA Zanzibar) na Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) pamoja na Ubalozi wa Norway.

Walieleza mifumo mingi iliyopo katika jamii imejengeka kwa kulenga kumkandamiza zaidi mwanamke na kutoa fursa kwa wanaume jambo ambalo linaweka ugumu kwa wanawake pale wanapohitaji kusimama kutetea haki zao.

Walitaja baadhi ya mifumo hiyo kuwa ni pamoja na elimu na huduma nyingine za kijamii ambapo wanawake huonekana kama kundi la utegemezi kwa wanaume.

Walisema licha ya wanawake wengi kujitahidi kusimama kutetea na kudai haki zao za msingi lakini changamoto za kijamii bado ni kikwazo kikuu kupata haki hizo kutokana na dhana potofu iliyojengeka kwa muda mrefu katika baadhi ya jamii dhidi ya uwezo wa wanawake.

Halima Mkubwa Juma, kutoka taasisi ya Pemba Rapid Development Organization (PRADO), alitaja mfumo dume uliojengeka kwenye jamii nyingi wa kumfanya mwanamke kuwa mama wa nyumbani umeathiri pakubwa uwezo wa wanawake kusimama kudai haki zao ikiwemo nafasi za uongozi katika vyombo vya maamuzi.

Alifahamisha, “wanawake kwa muda mrefu tumefanywa kuwa watu wa nyumbani tu, na kuwa wanaume ndio wa kufanya machumi, lakini kwasasa unakuta mwanamke kwenye familia ndiye anayefanya hayo machumikuliko hata mwanaume lakini likija suala la uongozi tunaonekana wanawake hatufai jambo ambalo sio sahihi.”

Nae Hamad Juma Kombo alieleza ili kuondokana na tatizo hilo na kuhakikisha upatikanaji na utoaji wa fursa sawa za kijinsia katika ngazi mbalimbali ni lazima wadau wa maendeleo kuendelea kuchukua hatua za kufahamisha jamii kukubali katika uwezo wa wanawake.

Aidha alisema kutokana na kuwepo kwa mifumo isiyo rafiki, wanawake wengi wanaogopa kujiunga katika vyama vya siasa hasa vya upinzani na kupelekea kukosa uzoefu wa uongozi.

“Suluhisho la ushiriki wa wanake katika uongozi ni wao kuwa tayari kujiunga katika vyama vya siasa na kushiriki nafasi za uongozi katika ngazi za matawi, kwani changamoto kubwa inayowafanya wanawake kushindwa kuonekana kwa wingi kwenye nafasi hizo ni kukosa misingi ya uongozikuanzia kwenye ngazi za chini,” alieleza Kombo.

Kwa upande wake Tatu Abdalla Msellem, kutoka Jumuiya ya Tumaini Jipya Pemba (TUJIPE) alitaja rushwa ya ngono na pesa kuwa moja ya vikwazo vinavyowakatisha tamaa wanawake wanaojitokeza kudai haki zao na kushiriki kugombea nafasi za uongozi kutokana na mfumo uliopo kutawaliwa zaidi na rushwa.

Aidha aliwataka wanawake kuchukulia vikwazo wanavyokumbana navyo pale wanapojitokeza kudai haki zao kama njia ya kuwaimarisha kuendelea kupigania hazi zao.

“Wanawake tusiseme kwamba hatutaki kugombea nafasi za uongozi kwasababu tunaogopa kuna changamoto ya rushwa ya ngono na pesa, tunachotakiwa kufanya ni kujitokeza kwa wingi na kutambua namna ya kushinda vikwazo hivyo bila kuathiri juhudi zetu,” alieleza Tatu.

Mapema mkurugenzi wa PEGAO, Hafidh Abdi alisema mkutano huo umewakutanisha wadau hao ili kujadili changamoto zilizoibuliwa na wahamasishaji jamii kutoka kwenye shehia na kuzitaftia ufumbuzi kwa lengo la kuweka mazingira rafiki ya upatikanaji wa haki za wanawake katika jamii.

“Baada ya timu yetu ya wahamasishaji jamii kufanya mikutano ya ufuatiliaji wa changamoto kwenye jamii zipo changamoto na vikwazo ambavyo vilibainika kukwaza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi ambazo ni pamoja na kisheria, kisiasa, kijamii na kidini ambapo sisi wadau wa haki za wanawake tunahitaji kujadiliana kwapamoja namna ya kuweza kuzitaftia suluhu,” alisema Hafidh.

Mkutano huo uliwashirikisha wawakilishi kutoka asasi za kiraia 40 kisiwani Pemba ambapo walipata fursa ya kujadili changamoto na vikwazo vinavyokwaza upatikanaji wa haki za wanawake na kuandaa mpangokazi wa namna ya kuzitatua baadhi ya changamoto zilizoibuliwa.

Mradi wa kuwezesha wanawake katika nafazi za uongozi Zanzibar unatekelezwa kwa mashirikiano ya taasisi za Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, (TAMWA Zanzibar), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na Pemba Gender Advocacy and Environmental Organization (PEGAO), kwa ufadhili wa Ubalozi wa Norway.
Baadhi ya washiriki kutoka asasi za kiraia Pemba wakishiriki mkutano
Washiriki wakiwa katika kazi za vikundi kuandaa mpangokazi wa namna ya kuzitatua baadhi ya changamoto zilizoibuliwa.
Mkurugenzi wa PEGAO, Hafidh Abdi akizungumza wakati wa mkutano.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad