HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, April 13, 2022

KONGAMANO LA BIASHARA NA UWEKEZAJI KATI YA TANZANIA NA INDIA-CHENNAIBalozi wa Tanzania nchini India, Mhe Anisa Mbega akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa masuala ya biashara na uwekezaji kutoka Tanzania na India katika hafla ya uzinduzi rasmi wa ofisi ya uratibu wa biashara na uwekezaji ITTC UBALOZI wa Tanzania nchini India kwa kushirikiana na taasisi ya Uchumi na Biashara ya India (Indian Economic Trade Organization) umeratibu na kufanikisha kufanyika kwa kongamano kubwa la biashara na uwekezaji (Tanzania India Trade Conference) lililofanyika katika jiji la Chennai, India kuanzia tarehe 11 - 12 Aprili 2022.

 Lengo la Kongamano hilo lilikuwa kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania kwa wafanyabishara na wawekezaji waliopo nchini India. Washiriki wa Kongamano hilo waliweza kukutana na taasisi mbalimbali zinazohusika na masuala ya uwekezaji na biashara nchini Tanzania ikiwepo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya maendeleo ya biashara Tanzania (TANTRADE), na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Aidha, kongamano hilo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya India kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara inayosimamia masuala ya biashara na wajasiriamali na viongozi wa serikali kutoka Jimbo la Tamil Nadu lenye makao yake makuu Jijini Chennai.

Kongamano hilo lilifunguliwa na Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe Anisa Mbega ambapo alisema “Tanzania na India ni marafiki na Nchi hizi zimekuwa na mahusiano mazuri ya kidiplomasia kwa muda mrefu ambayo yamejenga msingi imara katika biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo”. Aidha, aliongeza kuwa India ni nchi muhimu kwa Tanzania kwani ni nchi ya tano kwa uwekezaji na biashara nchini Tanzania ambapo wawekezaji kutoka India wamewekeza mtaji wa kiasi cha dola za Marekani Bilioni 3.7.
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe Anisa Mbega akifungua Kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na India Jijini Chennai India.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na wafanyabiashara na wawekezaji takribani 110 ambapo kupitia mawasilisho mbalimballi yaliyotolewa na Ofisi ya Ubalozi, TIC, TANTRADE na TRA waliweza kufahamishwa fursa za biashara kwa bidhaa za mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi na fursa za uwekezaji katika sekta za Miundombinu, Madini, Ujenzi wa majumba, viwanda vya madawa, mitambo ya viwandani, nguo, Elimu na Afya. 

Aidha, Wawekezaji na wafanyabiashara walipatiwa orodha ya miradi mbalimbali katika sekta le ngwa na sekta nyinginezo kutoka sekta binafsi na serikali ya Tanzania ambayo inatafuta uwezekano wa kuingia ubia na wawekezaji kutoka India kwa lengo la kuingiza mitaji, teknolojia na ujuzi kuanzisha na kuendesha miradi hiyo.
Wawakilishi wa taasisi za uhamasishaji na uratibu biashara na uwekezaji wakitoa mada kuhusu fursa zilizopo nchini Tanzania

Kutokana na kongamano hilo, tayari wawekezaji mbalimbali wa India wameonesha nia ya kuwekeza nchini Tanzania ambapo kundi la kwanza la wawekezaji kwenye sekta ya ujenzi wa viwanda vya madawa ya binadamu na vifaa tiba kutoka India, wanatarajia kutembelea Tanzania kuanzia tarehe 19 Aprili, 2022 ili kukutana na wadau na kuanza taratibu za kuwekeza Tanzania. 


Aidha, wafanyabiashara wa India walioshiriki Kongamano wameonesha nia ya kushiriki maonesho ya 46 ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam ambayo yataanza tarehe 28 Juni hadi tarehe 13 Julai, 2022 ambapo watakutana na wafanyabiashara na kuona bidhaa zinazozalishwa nchini Tanzania. 

Pia tayari wazalishaji wa bidhaa za Ngozi na korosho wa Tanzania wameunganishwa na wafanyabiashara wa India ambapo watapata fursa ya kuuza bidhaa hizo katika soko la India.

Sambamba na kufanyika kwa kongamano la biashara Ubalozi pia ulishiriki katika hafla ya uzinduzi wa ofisi ya uhamasishaji na uratibu wa biashara na uwekezaji inayojulikana kwa jina la INDIA TANZANIA TRADE COMMISSION (ITTC) iliyopo katika jengo la JJ Diamonds Mart No. 85, Barabara ya Gopathi Narayanaswani Chetty Chennai katika eneo la Thyagaraya Nagar ambalo ni kitovu cha biashara jijini Chennai. Ofisi hiyo itaongozwa na kusimamiwa na Dkt. J. Shrenik Nahar kama Kamishna wa biashara wa ITTC.

Uwepo wa ITTC utasaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa haraka wa taarifa sahihi za biashara na uwekezaji zilizopo nchini Tanzania, kwa kuwa ITTC itakuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na taasisi zinazosimamia masuala ya biashara na uwekezaji za nchini Tanzania. ITTC ipo chini ya taasisi ya Indian Economic Trade Organization (IETO).

Katika hotuba yake ya ufunguzi Mhe. Balozi Anisa Mbega alimshukuru Dkt. Asif Iqbar, Rais wa IETO kwa ushirikiano alioutoa kwa Ubalozi wakati wa mchakato wa kufanikisha uanzishwaji na ufunguzi wa ofisi ya uratibu wa masuala ya biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na India.
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe Anisa Mbega akikata utepe na kuwasha mshumaa kuashiria uzinduzi rasmi wa ofisi ya uratibu wa biashara na uwekezaji ITTC.

Kwa upande wake Dkt. J. Shrenik Nahar, Kamishna wa biashara wa ITTC alimshukuru Mhe. Balozi pamoja na washiriki kutoka taasisi zinazohamasisha na kuratibu biashara na uwekezaji kutoka Tanzania walioshiriki katika ufunguzi wa ofisi hiyo. Aidha, aliahidi kutoa ushirikiano kwa Ubalozi pamoja na taasisi hizo katika kufanikisha azma ya serikali ya kuendelea kuimarisha biashara na uwekezaji kati ya India na Tanzania.

Ufunguzi wa ofisi ya uratibu wa masuala ya biashara na uwekezaji umefanikishwa kwa ushirikiano wa Ubalozi na taasisi ya uchumi na biashara ya India IETO.

Ubalozi wa Tanzania nchini India unatoa shukrani kwa ushirikiano mkubwa uliopata kutoka kwa uongozi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambazo zimewezesha kongamano hili kuwa na mafanikio makubwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad