HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, March 4, 2022

WAZIRI GWAJIMA ATEMBELEA MIRADI YA MAENDELEO YA WATOTO YA BRAC

 

 Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dokta Dorothy Gwajima amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itahakikisha malezi ya watoto yanapewa kipaumbele katika awamu hii ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Hayo ameyasema wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi ya watoto ya  Play Lab na Mpango wa Taifa wa Msaada kwa Mtoto – National Child Help Line unaotekelezwa na BRAC Maendeleo Tanzania.

Waziri Gwajima ametembelea miradi hiyo ambapo mradi wa Mpango wa Taifa wa Msaada kwa Mtoto – National Child Help Line ambao unatekelezwa na Shirika la C-Sema kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania ambao unawasaidia watoto wanaohitaji huduma na ulinzi kupitia laini ya simu isiyo na malipo ya 116 inayopatikana katika mitandao yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akiwa katika ziara ya kutembelea kituo cha kijamii cha awali cha uchangamshi wa watoto kilichopo kata ya Mbagala kuu wilayani Temeke leo Machi 2,2022 Gwajima amewataka wazazi na wadau mbalimbali kushirikiana na serikali kuhakikisha watoto wanapata malezi wanayostahili kwani watoto ni kitambulisho cha Taifa.

Kituo hicho kilichojengwa kwa msaada wa Taasisi ya BRAC Maendeleo Tanzania kinachotoa elimu ya makuzi,kimwili,kiakili na kimawasiliano ni moja kati ya vituo vya aina hiyo vilivyojengwa nchini vinavyosaidia kuelimisha jamii kuhusu malezi sahihi.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo amesema wako tayari kutekeleza Sera hiyo ya mtoto kwanza kwani watoto ndio taifa la kesho huku akitoa shukrani kwa Taasisi hiyo kushirikiana na Serikali kufanikisha ujenzi wa vituo hivyo vya kulelea watoto wadogo.

Nae Mkurugenzi wa BRAC  Suzan Bipa amesema wamejikita katika ujenzi wa vituo hivyo ambapo zaidi ya vituo 30 vimekamilika katika sehemu mbalimbali hapa nchini.

"Tunawasaidia watoto wenye umri wa miaka 3 mpaka 5 kuwapa elimu changamshi au ya awali inayowajenga vizuri katika makuzi ya kimwili,akili katika lugha na mawasiliano"amesema Suzan

“Jukumu la malezi bora kw watoto ni suala mtambuka ambalo jamii yote inapaswa kushiriki malezi hayo ili kujenga jamii bora na yenye maadili mema Mwaka 2020, BRAC Maendeleo kwa maelekezo kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Vikundi Maalum, ilichagua shule 30 za msingi za serikali kwa ajili ya kuweka vituo vya malezi na makuzi ya watoto wadogo katika mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam,” 

Akizungumza miradi mingine, Suzan amesema Vituo vyote vya ECD katika mradi huu vimejengwa kwa ufadhili wa Shirika la Tuzo ya Yidan la Korea na kutumia mtaala wa michezo ambao uliundwa na BRAC kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TEA) na wadau wengine wa watoto. 

“Mtaala huu ulichaguliwa kwa sababu ya njia yake ya ubunifu ya kuhakikisha fursa bora za kujifunza kwa gharama nafuu kwa watoto hasa walio katika mazingira magumu. Mradi huu hutumia michezo ya ndani na nje ya darasa ili kuwapa watoto ujuzi na na pia kuwaandaa kwa shule za msingi,”

“Kupitia vituo hivi, watoto wanashiriki katika mafunzo ya miaka miwili ambapo watoto waweza kuendeleza uwezo wa utambuzi, kihisia, lugha, na hesabu. Baada ya kuhitimu kutoka vituo hivi, watoto wataingizwa kwenye madarasa ya awali katika shule za serikali husika ambapo BRAC itaendelea kutoa msaada wa kiufundi ili kujenga uwezo wa walimu wa awali”amesema 

 Aidha, amesema kuanzia mwaka 2016 BRAC ilipoanzisha mfumo wa kufundisha kupitia michezo kupitia mradi wa Play Lab, zaidi ya watoto 3,500 wenye umri wa miaka mitatu hadi mitano kutoka BRAC Play Labs katika mikoa ya Dar es Salaam na Mbeya wameingizwa katika shule za msingi na zaidi ya watoto 1670 wamejiunga katika shule za msingi 35 katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe na Tanga.

 Na mwaka 2020, BRAC Maendeleo iliungana na  C-Sema kuunga mkono mpango huu kupitia ufadhili kutoka kwa LEGO Foundation, ikiwa ni kama muendelezo wa mpango wa BRAC katika kusaidia maendeleo ya watoto wadogo nchini.

Kituo cha simu cha C-Sema kinasaidia utunzaji wa watoto wenye umri wa miaka 0-8 na wazazi wa watoto wote, kuwapa kipaumbele wale walio katika hatari na kutengwa sana. 

Kituo pia kinajulisha jamii na walezi kuhakikisha afya na lishe bora ya watoto, na kuwalinda kutokana na vitisho na hatari. Zaidi ya hayo, kituo kinawapa watoto wadogo fursa za kujifunza, kupitia mwingiliano ambao ni msikivu na wa kihisia na pia kusaidia afya ya akili na ustawi wa walezi.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalum Dorothy Gwajima akimsikiliza moja ya watoto wanaopata elimu  ya makuzi, Kimwili, kiakili na Mawasiliano inayotekelezwa na Taasisi ya BRAC Maendeleo Tanzania katika Kata ya Mbagala Kuu Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalum Dorothy Gwajima akimsikiliza moja ya watoto wanaopata elimu  ya makuzi, Kimwili, kiakili na Mawasiliano inayotekelezwa na Taasisi ya BRAC Maendeleo Tanzania akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo na Mkurugenzi wa BRAC Tanzania Suzan Bipa.
Mkurugenzi wa BRAC Maendeleo Tanzania Suzan Bipa akizungumza na wazazi wa watoto wanaopata elimu katika kituo cha elimu  ya makuzi, Kimwili, kiakili na Mawasiliano inayotekelezwa na Taasisi ya BRAC Maendeleo Tanzania katika Kata ya Mbagala Kuu Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalum Dorothy Gwajima akizungumza na wazazi mara baada ya kutembelea kituo cha  elimu  ya makuzi, Kimwili, kiakili na Mawasiliano inayotekelezwa na Taasisi ya BRAC Maendeleo Tanzania katika Kata ya Mbagala Kuu Jijini Dar es Salaam, Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo
Wazazi wakiipongeza serikali na Taasisi ya BRAC Maendeleo Tanzania kwa kuanzisha Kituo hicho na kuwataka kuongeza vingine kwa sababu mahitaji ya watoto ni wengi sana
Picha ya Pamoja ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalumu, Mkuu ww Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo, Mbunge wa Jimbo la Temeke Dorothy na Mkurugenzi wa BRAC Tanzania Suzan Bipa, Walimu, watoto na wazazi

















No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad