HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, March 22, 2022

Msechu ahimiza wafanyakazi wa NHC kufanya kazi kwa Bidii


Mkurugenzi Mkuu Nehemiah Mchechu akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Shirika na wafanyakazi wengine. Na Mwandishi Wetu
MKURUGENI Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw. Nehemiah Kyando Mchechu ameishukuru Serikali kwa kumuamini na kumpa nafasi nyingine ya kuliongoza Shirika na kuahidi kuwa ataifanya kazi hiyo kwa weledi mkubwa ili kuleta tija kwa Taifa.

Ameyasema hayo leo (tarehe 21 Machi, 2022) wakati akizungumza na wafanyakazi wa NHC mkoa wa Dar es Salaam mara baada ya kuripoti ofisini kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Machi 14,2022 kushika wadhifa huo.

Amewataka wafanyakazi wa NHC kufanya kazi kwa bidii na mshikamano na kwamba hatawavumilia watumishi wazembe wanaofanya kazi kwa mazoea.

“Ninataka yale yote tuliyoyafanya kwa miaka minane kipindi kile nikiwa NHC , yafanyike mengine makubwa kama yale kwa kipindi kifupi cha miaka minne tu, kwa maana hiyo ninasema tunahitaji kufanya kazi kwa kasi kubwa na nguvu zaidi ili kukidhi matarajio ya watanzania,’’amesema.

Amewaahidi wafanyakazi hao kuwa yupo tayari kuondoa vikwazo mbalimbali vitakavyojitokeza ili kazi iendelee kwa ufanisi mkubwa.

Pamoja na kukamilisha miradi ya Kawe 711 na Morocco Square, Bw. Mchechu amewataka wafanyakazi hao kuwa wabunifu ili kuifikisha nchi mahala pazuri kwenye sekta ya nyumba ambayo ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi. ‘Tupendezeshe majiji yetu, tukuze biashara ya nyumba kwa kujenga nyumba mpya kwa ushirikiano na wawekezaji kwani mahitaji ya nyumba bado ni makubwa sana hivyo ni vyema kuwa na tafakari ya kina ili kuweza kuyafikia.”

Amesema NHC katika kipindi chake inatarajia kujenga nyumba na kuboresha makazi nchini ili kusukuma mbele malengo ya serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais Samia. Miradi itamaliziwa na kuanzishwa mingine na kukamilisha mazungumzo ya ubia ambayo hadi sasa bado imesimama.

Ametaka wafanyakazi kufunga mikanda, kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kwamba wale wanaohisi kuwa hawataendana na kasi yake ni bora waombe uhamisho kwa kuwa kasi ya utendaji anayoitaka itakayoanza muda mfupi ujao ni kubwa kwa ajili ya mustakabali wa Shirika na Taifa kwa ujumla.

Amesema mambo yote mazuri yaliyofanyika kipindi kilichopita yatachukuliwa. Akabainisha kuwa muundo wa Shirika utapitiwa upya ili kuweza kuendana na mabadiliko ya kibiashara na soko la nyumba kwa sasa.

“Kuna vitu havitabadilika vitabaki vile vile na kuna mambo lazima yabadilike kwa mustakabali wa Shirika hivyo ni lazima tubadilike, ni lazima tuwe wabunifu, kuzingatia utaalamu, ufanisi na usikivu wa hali ya juu ili tuweze kukidhi mahitaji ya soko,”amesema.

Ametaka kila mfanyakazi katika idara yake afanye kazi kwa weledi na kuhakikisha kuwa rasilimali muda na fedha za umma zinatumika vizuri, kuwa na nidhamu ya hali ya juu na ufanisi wa kiwango cha juu na anaamini kwamba Shirika bado lina wafanyakazi wenye ari na wanayoyaishi ipasavyo maadili ya msingi ya Shirika.

Amesisitiza Mameneja wa Mikoa ya NHC kujitahidi kukusanya kodi na malimbikizo yote na kwamba amewapa mamlaka ya kumuondoa kwenye nyumba mpangaji asiyelipa kodi bila ya kuomba kibali cha Mkurugenzi Mkuu. “Nasema hivyo kwa kuwa naamini uondoaji wa wapangaji hao unafanywa na watu wenye taaluma na bila kumuonea mtu, kitakachopaswa kufanyika ni kunipatia taarifa tu kwamba ni wapi na lini jambo hilo linafanyika,” amesema.

Aliwapongeza wafanyakazi kwa kazi nzuri iliyofanywa na kwamba suala kubwa analolitizama kwa sasa ni kufikia matarajio ya Watanzania ambayo ni makubwa.

Shirika la Nyumba la Taifa kwa sasa lina mtaji unaofikia trilioni 5.1, mtaji unaoliwezesha kufanya mapinduzi makubwa ya sekta ya nyumba. Bw. Nehemia Mchechu aliteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mkurugenzi Mkuu wa NHC Machi 2010 na kunyanyua mtaji wa Shirika kutoka trilioni 1.5 hadi trilioni 4.5 mwaka 2018.
Bi Ruth Ngakuka wa Kitengo cha Manunuzi na Ugavi akimkaribisha Mkurugenzi Mkuu Nehemiah Mchechu kwa kumpa zawadi ya ua mara baada ya kuwasili katika ofisi za NHC.
Mkurugenzi Mkuu Nehemiah Mchechu akiwasili katika ukumbi wa mkutano kwa ajili ya kikao na wafanyakazi.
Mkurugenzi Mkuu Nehemiah Mchechu akikabidhiwa ofisi na mtangulizi wake aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika, Dk. Maulidi Abdallah Banyani leo hii.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad