HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, March 23, 2022

Maadhimisho Siku ya Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika yafana Kongwa

Na Eleuteri Mangi-WUSM, Kongwa
MAADHIMISHO ya Siku ya Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika yamefanyika Wilayani Kongwa kwa lengo la kuimarisha utangamano wa kikanda baina ya nchi za Kusini mwa Afrika ili kuenzi jitihada za viongozi na majeshi ambayo yaliyojitoa mhanga kwa ajili ya nchi za Afrika.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu Machi 23, 2022 Kongwa mkoani Dodoma kwa niaba ya Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Pauline Gekul wakati akifungua maadhimisho ya Siku ya Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika.


Katika kuadhimisha siku hiyo hapa nchini Naibu Katibu Mkuu huyo amesema Serikali itaendelea kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa kuyatambua maeneo ya kihistoria, kuyalinda, na kuyaendeleza ili kuenzi historia ya taifa na kuyafanya sehemu ya utalii wa kihistoria katika maeneo ya urithi wa ukombozi yaliyopo nchini.


“Serikali itashirikiana na nchi tulizozipa hifadhi wakati wa harakati za ukombozi kwa kukarabati majengo yaliyotumika na wapigania uhuru wa Afrika ikiwa ni sehemu ya kuenzi mchango wao na kuitunza historia hiyo kwa ajili ya kizazi cha sasa na cha baadae” amesema Naibu Katibu Mkuu Bw. Yakubu.


Hatua ya kuanza kwa maadhimisho hayo ni kuenzi matamanio ya Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambaye aliona Tanzania haitakuwa huru kama nchi nyingine zikiendelea kuwa chini ya Ubepari na Ukoloni.


Ametaja malengo mengine ni kuendelea kukumbusha jamii ya Afrika usawa kwa wote, pasipo kubaguana kwa rangi, kabila au uwezo na kurithisha, kuhifadhi na kuendeleza amali za urithi wa ukombozi zilizopo katika nchi za Kusini mwa Afrika ikiwa ni vielelezo muhimu vya utalii wa kiukombozi.


Katika harakati hizo za Ukombozi kusini mwa Afrika, wananchi wa Halmashauri ya Kongwa ni wadau muhimu katika harakati hizo ambapo walijitoa kwa moyo na uzalendo kuwapokea wapigania Uhuru wa nchi za Kusini Mwa Afrika.


“Natambua mliwapa makazi, vyakula, mashamba na hadi Watoto, mlilinda roho nyingi ambazo leo hii ndio viongozi wa nchi za Kusini Mwa Afrika. Ukweli utabaki ulivyo kuwa, mchango wa wananchi wa Kongwa katika harakati za Ukombozi wa Afrika utaenziwa kikamilifu” amesema Naibu Katibu Mkuu Bw. Yakubu.


Aidha, Watanzania wenye vielelezo vya harakati za ukombozi wa Afrika wametakiwa kuviwasilisha katika Ofisi za Programu ya Ukombozi wa Afrika ili vihifadhiwe kitaalamu visipotee ama kuharibika kwa manufaa ya Taifa vya kiushahidi vya harakati za ukombozi.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Bw. Remidius Mwema Emmanuel amesema wananchi wa Kongwa wanatambua thamani ya eneo hilo ambalo linahistoria kubwa hapa nchini na Barani Afrika.


Bw. Remidius amesema kuwa wilaya hiyo inaendelea kupokea wageni wengi kutembelea eneo hilo akiwemo Waziri wa Habari na Utangazaji kutoka Jamhuri ya Zimbabwe ambaye pia ni miongoni mwa wapigania uhuru wa taifa hilo Mhe. Monica Mutsvangwa ambaye alifanya ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia Desemba 17-19, 2021 ili kuandaa makala Maalumu ya Ukombozi wa Taifa hilo. Wageni wengine wanatoka katika mataifa ya Afrika Kusini, Angola, Msumbiji, Namibia.


Maadhimisho hayo ni maelekezo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo imeazimiwa kuwa Machi 23 kila mwaka itaadhimishwa kama Siku ya kumbukizi ya kukomeshwa kwa utawala wa kimabavu na ubaguzi wa rangi kwa Nchi za Kusini mwa Afrika ambapo zoezi hilo lilihitimishwa na majeshi ya Afrika Mwaka 1994.


Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na viongozi wa Serikali, wananchi, wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya Utamaduni na Sanaa kutoka wilaya ya Kongwa pamoja na wilaya jirani za mkoa wa Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu
ameongoza maadhimisho ya Siku ya Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika ambayo yamefanyika Wilayani Kongwa ambapo Machi 23, 2022 Kongwa mkoani Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad