HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, February 21, 2022

SERIKALI YAIPONGEZA WCF KWA UTENDAJI BORA

  Naibu Waziri wa Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi (MB), amesema Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ni miongoni mwa Taasisi za Serikali ambazo ni mfano wa kuigwa barani Afrika. 

Ameyasema hayo wakati wa hafla ya kukabidhi kompyuta za mezani kwa Tume ya Utumishi wa Umma (PO-PSC) kwa ajili ya kuboresha utekelezaji wa majukumu yao    iliyofanyika katika Ofisi za Mfuko huo zilizopo Jijini Dodoma.

Mfuko huu umekuwa ukitekeleza majukumu yake kisasa zaidi na umewekeza sana kwenye matumizi ya Teknolojia (TEHAMA) kuanzia usajili, kupokea michango hadi kuchakata madai vyote kwa njia ya mtandao, amesema Mhe. Katambi.

Ameongeza kuwa WCF imefanikiwa kulipa mabilioni ya fidia kwa kipindi kifupi sana tangu kuanzishwa kwake 2015. Serikali ya Awamu ya Sita iliona umuhimu wa kuboresha mazingira ya uwekezaji ndio maana iliridhia punguzo la michango ya wafanyakazi kwa waajiri wa Sekta Binafsi kutoka asilimia moja (1%) hadi sifuri nukta sita (0.6%) pamoja na punguzo la tozo kutoka asilimia kumi (10%) hadi asilimia (2%) kwa lengo la kuweka mazingira rafiki zaidi ya uwekezaji hapa nchini, na hii ndio dira ya Mhe. Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan. 

Mhe. Katambi amesema WCF imejijengea utamaduni mzuri wa kusaidia bila kubagua ambapo wamekuwa wakiwakumbuka wadau mbalimbali. 

Amesema, kwa upande wa Tume ya Utumishi wa Umma, anatambua wanawajibu mkubwa sana katika kuhakikisha wananchi wanapokea huduma zilizokusudiwa kwa kusimamia vyema nidhamu ya watumishi wa umma. Amesisitiza ili Tume iweze kutekeleza majukumu yeke kwa ufanisi zaidi, matumizi ya TEHAMA kwenye ulimwengu wa sasa ni muhimu sana. 

“Wajibu wenu ni kuhakikisha mnafanya kazi kwa kuzingatia sheria, simamieni nidhamu ya Utumishi wa Umma na endeleeni kuangalia maeneo mengine yanayoweza kuboresha utendaji kazi wenu. TEHAMA inapunguza urasimu hakikisheni mnatumia kompyuta hizi katika kuongeza tija kwenye shughuli zenu za kila siku hususan wakati huu ambao Serikali ya Awamu ya Sita ina dhamira ya dhati ya kumaliza kero ya urasimu katika utoaji wa huduma za Serikali kwa wananchi wake”, amesema Mhe. Katambi.

Mhe. Katambi pia amewapongeza WCF kwa kuandaa machapisho yenye miongozo mbalimbali kuhusu fidia kwa wafanyakazi kwa nukta nundu ambayo yalikabidhiwa kwa Jumuiya ya Watu Wasioona (TAB) wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Maandishi ya Nukta Nundu(Braille). Vilevile amewapongeza kwa misaada ya fimbo nyeupe kwa jamii hiyo yenye mahitaji maalum. Huu ni utamaduni mzuri endeleeni kugusa makundi yote kwenye jamii yetu, amesisitiza Mhe. Katambi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma amesema pamoja na punguzo hilo la michango ya waajiri la kutoka asilimia moja (1%) hadi kufikia asilimia sifuri nukta sita (0.6), malipo ya fidia kwa wafanyakazi hayataathirika. 

Akizungumzia kuhusu vifaa walivyotoa, Dkt. Mduma amesema walipokea maombi ya vifaa mbalimbali vya kiutendaji kutoka Tume ya Utumishi wa Umma na kwa kutambua umuhimu wa mahitaji hayo WCF iliona ishiriki katika kusaidia upatikanaji wa kompyuta za mezani kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utendaji pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Mama Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuleta maendeleo kwa wananchi.

“Tunatambua umuhimu wa Tume hii katika kusimamia uwajibikaji nchini hususan watumishi wa umma. Usimamizi wao madhubuti utachangiwa sio tu na uweledi wa wafanyakazi wa Tume katika utekelezaji wa majukumu yao bali pia uwepo wa vifaa vitakavyorahisisha utendaji kazi”, alisisitiza Dkt. Mduma. 

Naye Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Mathew Kirama ameishukuru WCF kwa msaada huo na kuongeza kuwa umekuja wakati muafaka.

“Tunatambua kuwa zipo Taasisi nyingi zinazokabiliwa na changamoto ya vitendea kazi lakini mmeipa Tume kipaumbele tunawashukuru sana na kuahidi kuongeza bidii zaidi ambapo vifaa hivi ni sehemu ya uboreshaji wa utendaji kazi wetu”, amesema Bw. Kirama.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi (katikati) akiongea kwenye hafla ya makabidhiano ya kompyuta baina ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Tume ya Utumishi wa Umma jijini Dodoma. Kushoto ni Katibu wa Tume Bw. Mathew Kirama na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi (mwenye tai nyekundu) akikabidhi kompyuta kwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Mathew Kirama (kulia) kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma (kushoto). Wanaoshuhudia ni watumishi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) pamoja na wa Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi (mwenye tai nyekundu) akikabidhi kompyuta kwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Mathew Kirama (kulia) kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma (kushoto).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad