HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, January 18, 2022

WAZIRI NAPE ATAKA ZOEZI LA ANUANI ZA MAKAZI YA WATU KUKAMILIKA NDANI YA MIEZI MITANO MKOA WA PWANI

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Clarence Ichwekeleza akimuonesha Katibu wa CCM Mkoa wa Pwani Cde, Said Yusuf Goha namna ya kupata postikodi ya kata mbalimbali nchini kwa kutumia simu ya mkononi wakati wa semina ya kuwajengea uwezo wataalam wa Mkoa Pwani kuhusu mfumo wa anwani za Makazi na Postikodi iliyofunguliwa na Waziri wa Wizara hiyo, Nape Nnauye, Mkoani hapo.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa semina ya kuwajengea uwezo wataalam wa Mkoa wa Pwani kuhusu mfumo wa anwani za Makazi na Postikodi katika ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Mkoa huo leo Januari 18, 2022.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge, akitoa salamu za Mkoa kabla ya kumkaribisha Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye (hayupo pichani) kwa ajili ya kufungua semina ya kuwajengea uwezo wataalam wa Mkoa huo kuhusu mfumo wa anwani za makazi na postikodi iliyofanyika kwenye ukumbi wa Mkuu wa Mkoa huo.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Nickson John na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Zainabu Abudallah wakifuatilia maelezo kuhusu namna ya kupata postikodi ya kata mbalimbali nchini kwa kutumia simu ya mkononi wakati wa semina ya kuwajengea uwezo wataalam wa Mkoa Pwani kuhusu mfumo wa anwani za makazi na postikodi iliyofunguliwa na Waziri wa Wizara hiyo, Nape Nnauye, Mkoani hapo.

Mhandisi Jampyion Mbugi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari akiwasilisha mada ya kuwajengea uwezo wataalam wa Mkoa wa Pwani kuhusu mfumo wa anwani za makazi na ostikodi iliyofunguliwa na Waziri wa Wizara hiyo, Nape Nnauye, mkoani hapo.

Na Khadija Kalili , Kibaha
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nape Nnauye amewataka Viongozi wa Chama na Serikali kuhakikisha kuwa wanasimmia ipasavyo zoezi la anuani na makazi ya wananchi Mkoani Pwani.

"Awali uwekaji wa mfumo wa anuani za makazi ulikua mradi wa miaka mitano lakini sasa zoezi litafanyika ndani ya miezi mitano badala ya miaka mitano kama ilivyokuwa itekelezwe hapo mwanzo kulingana na Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Ibara ya 61(M), ya mwaka 2020.

Waziri Nape alisema hayo leo Kibaha katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya utekelezaji mfumo huo katika Mkoa wa Pwani, Waziri Nape alisema kuwa zoezi hilo linafanyika kutokana na misingi mitatu ikiwemo ile ya Ilani ya CCM, Sera ya Posta ya mwaka 2003 pamoja na Tanzania kuwa sehemu ya dunia kwani ni mwanachama wa Posta Afrika na Duniani., “Msingi wa anuani za makazi unajengwa na msingi mitatu ikiwemo Ilani ya CCM mwaka 2020, Sera ya Posta ya mwaka 2003 pamoja na Tanzania kuwa mwananchama wa Posta Afrika na UN, "suala hili linatekelezwa kwa miezi mitano tu badala ya miaka mitano kama Ilani inavyoelekeza, kwani itasaidia sana katika utekelezaji wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti maka huu”, alisema Waziri Nape.

Nape alisema kuwa katika utekelezaji wa zoezi hili hakuna mbadala isipokuwa ni kutekeleza kwa nguvu zote kwani Serikali ya Awamu ya Sita inadhamiria kuwasdaidia wananchi katika kuboresha mawasiliano katika sehemu mbalimbali ikiwemo makazi yao, sehemu zao za biashara na maeneo mengine ya huduma za kijamii.

 Aidha, Waziri Nape alisema utekelezaji wa zoezi la Anwani za Makazi ni Jambo la kihistoria ambapo Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuacha alama kwa watanzania na lengo lake ni kurahisisha mawasiliano na kuifanya jamii kuwa ya kisasa zaidi bila kusahau kuimarisha ulinzi katika makazi yao. 

Nape aliwataka viongozi wa mkoa wa Pwani kusimamia kwa jitihada kubwa ili kurahisisha utekelezaji wa zoezi hilo kwani mkoa huo bado uko nyuma katika utekelezaji huku akiwaomba uongozi wa CCM kutoka ngazi ya mkoa mpaka ngazi ya tawi kuhamasisha jambo hilo kwani ni moja ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho ambapo wenyewe ndiyo wasimamizi.

 “Hapa hautuna kitu kingine zaidi ya utekelezaji wa zoezi hili, iwe mvua, iwe jua lazima jambo hili litekelezwe, Pwani mko nyuma sana mna kata 3 ambazo zimetekeleza jambo hili na nguzo 439 zimewekwa lakini bado kata 139, mahitaji yenu ni nguzo 75,392 na vibao 912,640 kwa hiyo utekelezaji wenu umefikia asilimia 1 bado asilimia 99”, Waziri Nape. 

Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema kuwa zoezi la uwekeji wa anwani za makazi na Postikodi litarahisisha utambuzi wa maeneo ya shughuli mbalimbali za mkoa wa Pwani yakiwemo maeneo ya viwanda.

 “Anwani za Makazi na Postikodi ni mfumo mzuri ambao utatuonesha maeneo yetu mbalimbali kama mnavyofahamu kuwa Pwani ina viwanda vingi sana kwa hiyo uwepo wa anwani za makazi zitawarahisishia wananchi na zitarahisisha usafirishaji katika maeneo yetu”, Alisema Kunenge.

 Naye, Mkurugenzi wa Mawasiliano kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Clarence Ichwekeleza alisema kuwa sekta ya Mawasiliano ni sekta mtambuka ambayo inawezesha sekta zingine kuendelea.

 “Kama mnavyofahamu kwamba Mawasiliano ni sekta mtambuka sekta zote zinategemea sekta hii, kwa hiyo uwekaji wa anwani za makazi na postikodi itarahisisha mawasiliano kwa wananchi, Wizara ya Mawasiliano inashirikiana na TAMISEMI na Wizara ya Ardhi ili kutekeleza hili jambo”, Mhandisi Ichwekeleza.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad