HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, January 19, 2022

WATUMISHI HOUSING KUJENGA NYUMBA ZA WATUMISHI KATIKA WILAYA NA MIKOA YENYE UHITAJI

 WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ameielekeza Menejimenti ya Watumishi Housing kuangalia uwezekano wa kujenga nyumba za kuwauzia na kuwapangisha Watumishi wa Umma waliopo katika Wilaya na Mikoa yenye uhitaji badala ya kutoa kipaumbele kikubwa cha ujenzi wa nyumba hizo mijini.


Mhe. Jenista ametoa maelekezo hayo mara baada ya kukagua utekelezaji wa ujenzi wa nyumba za Watumishi wa Umma zilizojengwa na Watumishi Housing eneo la Gezaulole, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Mhe. Jenista amesema kuna uhitaji mkubwa wa nyumba za watumishi katika Halmashauri za Wilaya na Sekretarieti za Mikoa hususan kwa Walimu, Watumishi wa Sekta ya Afya, Askari wa Jeshi la Polisi na Watumishi wa Kada za chini, hivyo ni vema Watumishi Housing ikawa sehemu ya utatuzi wa changamoto hiyo.

Ameongeza kuwa, katika kutatua changamoto hiyo ya upungufu wa nyumba za watumishi, Ofisi yake itashauriana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI ili kuona namna bora ya kuitumia Watumishi Housing kujenga nyumba za watumishi.

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imejenga vituo vya afya katika kila Halmashauri ya Wilaya na kupeleka Watumishi wa kutoa huduma katika vituo hivyo, hivyo wanahitaji nyumba kwa ajili ya kuishi ili waweze kufanya kazi kwa ufasaha,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Mhe. Jenista ametoa wito kwa Watumishi wa Umma kupanga na kuzinunua nyumba zinazojengwa na Watumishi Housing kwani ni za gharama nafuu kwa asilimia 10 mpaka 30 ya bei za nyumba zilizoko kwenye soko.

Mhe. Jenista ameishauri Watumishi Housing kushirikiana na Halmashauri ili kupata viwanja vya gharama nafuu vitavyowezesha kujenga nyumba ambazo Watumishi wenye kipato cha chini watamudu kupanga na kuzinunua.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing, Dkt. Fred Msemwa amemhakikishia Mhe. Jenista kuwa ataisimamia taasisi yake katika kutekeleza maelekezo aliyoyatoa ili watumishi wanufaike na nyumba za gharama nafuu.

“Nikuhakikishie Mhe. Waziri, mimi na wasaidizi wangu tutaendelea kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa bidii ili kukidhi azma ya Serikali ya kuwawezesha Watumishi wa Umma kupata nyumba za gharama nafuu,” Dkt. Msemwa ameahidi.

Mhe. Jenista amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili jijini Dar es Salaam ya kutembelea Chuo cha Utumishi wa Umma na Watumishi Housing kwa lengo la kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji katika taasisi hizo.
 




Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa ameambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing, Dkt. Fred Msemwa,Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Nyangasa akikagua miradi ya Watumishi Housing eneo la Gezaulole, Kigamboni jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kikazi ya kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo. (Picha zote na Emmanuel Mssaka wa Michuzi Tv)

Mafundi wakiendelea na kazi ya ujenzi wa ukuta katika Mradi Nyumba za Watumishi Housing Company zilizopo Gezaulole wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama,Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing, Dkt. Fred Msemwa,Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Nyangasa wakimsalimia mkazi wa nyumba zilizojengwa na Watumishi Housing eneo la Gezaulole Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kikazi ya kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na watumishi wa Watumishi Housing jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kikazi ya kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing, Dkt. Fred Msemwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Jenista ya kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo. (Picha zote na Emmanuel Mssaka wa Michuzi Tv)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad