HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, January 22, 2022

Nyumba 27 zaezuliwa na upepo mkali wilayani Wanging'ombe, mtoto ajeruhiwa

 Na Amiri Kilagalila,Njombe.

Nyumba 27 zimeezuliwa na mvua iliyoambatana na upepo mkali huku watu wawili  wakijeruhiwa akiwemo mtoto mwenye umri wa miaka miwili faraja City katika kijiji cha Banawanu kata ya Udonja wilayani Wanging'ombe mkoa wa Njombe.

Akizungumza mbele ya kamati ya tathimini ya maafa ya halmashauri ya wilaya ya Wanging'ombe,mwenyekiti wa kijiji cha Banawanu Waston Mwenda   alisema tukio hilo limetokea Januari 20 majira ya saa 10 jioni ambapo majeruhi mwengine ni Amos Kuyava(45).

Alisema maafa hayo yameathiri sana kitongoji cha Talibato ambapo katika vitongoji vyengine kumeezuliwa nyumba moja moja.

"Kijiji chetu kina vitongoji vitano lakini kulipoathirika sana ni kitongoji cha Talibato nyumba 21,kwengine ni kidogo kidogo kama kitongoji cha Mji mwema nyumba tatu cha Banawanu kati kumeezuliwa nyumba mbili,Nyaubaga nyumba moja kwa hiyo kwa jumla nyumba zote zilizoezuliwa ni 27"amesema Waston Mwenda

"Kwa athari zilizotokea ni watu wawili mmoja ameumia na mtoto amepelekwa hospitali ya ikelu anaendelea na matibabu vizuri kwa hiyo aliyejeruhiwa hadi kifo amna,ila watu nyumba zao nyingi zimeezuliwa mapaa na nyingine zimebomoka kabisa"aliongeza Mwenda.

Kwa upande wa waathirika hao wameiomba serikali kuona namna ya kuwasaidia kwa sababu pamoja na nyumba zao kuezuliwa lakini na vyakula vimeharibika.

"Mimi sina pa kulala nalala jikoni ambako hakuna mlango,nilikua nimeweka mahindi yangu lakini yote yameloana na mvua,unga pamoja na nguo kwa kweli naiomba serikali itusaidie ione namna ya kutusaidia kwa sababu hili janga limetukuta katika kipindi kigumu"amesema Beatrice Mtivike mama wa watoto watano.

Beatrice alisema kuwa wanamshukuru Mungu kwa sababu wakati tukio hilo linatokea walikua shambani kulima.

Naye Abel Kidegelime amesema kuwa kuezuliwa kwa nyumba hizo imewaathiri kwa kiasi kikubwa na kwamba kungekua na watu ndani wasingepona.

Geofrey Benela amesema tukio hilo limewakuta kipindi ambacho ni cha maandalizi ya kuwapeleka watoto shule.

"Janga hili limetukuta kipindi ambacho tunatakiwa kuwapeleka watoto shule,janga hili linadhoofisha sana kimaisha,upepo ulikua mkali ndo maana umeleta madhara makubwa namna hii"amesema Benela.

Afisa Mazingira wilaya ya Wanging'ombe Frank Ngogo,alitoa pole kwa kaya zilizokutwa na maafa hayo na kuwataka kuwa watulivu katika kipindi hiki na kutoa wito kwa wakazi wa kijiji cha Banawanu kuongeza juhudi za kupanda miti ili iweze kusaidia kuzuia upepo mkali.




mwenyekiti wa kijiji cha Banawanu Waston Mwenda akizungmza na wanakijiji mara baada ya nyumba kuezuliwa na upepo Mkoani Njombe.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad