HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, January 27, 2022

MAJALIWA: MATUMIZI YA KISWAHILI YAPEWE KIPAUMBELE

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika hafla ya kutoa tuzo kwa washindi wa uandishi katika Shindano la Tuzo ya Kiswahili ya Fasihi ya Mabati – Cornell ya Fasihi ya Afrika, kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam, Januari 27, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi hundi ya dola za Marekani 2,500, Lucas Lubango ambaye aliibuka msihindi wa pili Riwaya 2021 baada kuandika Riwaya iitwayo Bweni la Wasichana katika hafla ya kutoa tuzo kwa washindi wa uandishi katika Shindano la Tuzo ya Kiswahili ya Fasihi ya Mabati – Cornell ya Fasihi ya Afrika, kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam, Januari 27, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema matumizi fasaha ya lugha ya kiswahili yapewe kipaumbele katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo ya utoaji wa huduma za jamii, mikutano, mahakamani, warsha na makongamano yatakayofanyika ndani na nje ya nchi.

“Matumizi ya lugha ya kiswahili yaimarishwe katika kutoa huduma za kimahakama na uandishi wa nyaraka za kisheria pamoja na kutafsiri sheria mbalimbali yafanyike kwa lugha ya kiswahili ili kuwawezesha Watanzania kutambua haki zao lakini kuijua sheria yenyewe.”

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Alhamisi, Januari 27, 2022) kwenye hafla ya kutoa tuzo kwa washindi wa uandishi katika Shindano la Tuzo ya Kiswahili ya Mabati- Cornell ya Fasihi ya Afrika 2021 katika ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City, Dar Es Salaam.

Waziri Mkuu ameziagiza Wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki zishirikiane kujenga uwezo wa wataalam wa ndani wa kutafsiri lugha mbalimbali za kigeni.

“Wizara ya Elimu iendelee kufanyia kazi mkakati wa kukitumia kiswahili kufundishia katika ngazi mbalimbali za elimu na kuongeza wataalam wa lugha hiyo katika ngazi ya uzamivu. “Mafunzo ya lugha ya kiswahili yaimarishwe kwa kutoa program maalum kwa ajili ya kuzalisha wataalam na wakalimani wa kiswahili wenye kukidhi viwango vya Kimataifa.”

Ameiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ihakikishe kwamba, bidhaa zote zinazozalishwa katika viwanda vya ndani na zile zinazoingizwa nchini kutoka nje zinakuwa na maelekezo yaliyotolewa kwa lugha ya kiswahili. “Kufanya hivyo, kutawafanya watumiaji wa bidhaa hizo wazitumie wakiwa wanafahamu vyema maelekezo yaliyomo katika bidhaa hizo.”

“Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) wekeni mikakati ya kushirikiana na wadau mbalimbali wenye nia ya kuwekeza katika lugha ya kiswahili ikiwemo katika kuendesha makongamano na warsha zinazolenga kukuza na kuendeleza Lugha ya Kiswahili nchini.”

Waziri Mkuu ameagiza wataalam wa lugha ya kiswahili kutoka vyuo vikuu na kutoka Mabaraza ya Kiswahili nchini watumike kikamilifu katika kushauri na utekelezaji wa mikakati ya kuendeleza lugha ya kiswahili. “Mikakati ya kukibidhaisha kiswahili iendelezwe kwa ushirikiano na Balozi zetu mbalimbali.”

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kukipongeza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuendelea kuwekeza katika lugha ya kiswahili. “Hakika mnastahili kuwa mfano wa kuigwa. Wengi wetu ni matunda ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.”

“Ninatoa wito kwenu kutimiza ndoto ambayo mmekuwa nayo kwa muda mrefu ya kuwa na Kituo Mahiri cha Taaluma za Kiswahili Duniani. Aidha, endeeleni kushirikiana na ALAF na wadau wengine kuhakikisha kwamba wanafunzi wengi wanapewa ufadhili wa kusoma Kiswahili hususan katika ngazi ya umahiri.”

Naye, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohammed Mchengerwa ametoa wito kwa wataalamu wa lugha ya kiswahili wasilale na badala yake wachangamkie fursa zitokanazo na matumizi ya lugha ya kiswahili katika Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika kama ukalimalini.

“…Tutaendelea na jukumu hili kwa jitihada na kasi kubwa ya kuhakikisha kiswahili kinaendelea kukua zaidi na pia dunia itambue kuwa nchi ya Tanzania ndio chimbuko la lugha ya kiswahili na ipewe kipaumbele cha kufundisha lugha hiyo. Tuandae kanzidata ya kuwatambua wataalamu wote wenye ufahamu wa kwenda kufundisha lugha ya kiswahili kwenye nchi mbalimbali”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini ya Chuo Kikuu Cornell ameziomba Serikali za nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zishirikiane na waandaaji wa tuzo hizo kwa lengo la kukuza lugha ya kiswahili. “Utamaduni ni kitu muhimu sana.”

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Alaf, Ashish Mistry ambao ndio wadhamini wa mashindano hayo amesema kampuni yao inatambua umuhimu wa lugha ya kiswahili katika mchango wake mkubwa kukuza uchumi. Amesema wamedhamini wanafunzi sita kusomea shahada ya uzamili ya lugha ya kiswahili na kati yao watatu wameshahitimu.

Kwa upande wake, Msanifu Lugha Mkuu wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Consolata Mushi amesema baraza hilo linatambua na kuthamini jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha lugha ya kiswahili inakua na kuheshimiwa duniani kote.

Awali, akiwa katika tukio hilo aliwaomba washiriki wasimame kwa muda na kuimba wimbo wa kumtakia kheri ya kumbukizi ya siku ya kuzaliwa kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambapo walimpongeza kwa kuimba wimbo kwa lunga ya kiswahili.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad