HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 6, 2021

CHUKI NA MWALIMU WA KICHAGA

 

 

ADELADIUS MAKWEGA, DODOMA.

Darasa la letu lilikuwa na wanafunzi 100 huku kukiwa na mikondo miwili ya A na B. Mwalimu wa darasa letu alikuwa binti wa Kichaga ambaye alikuwa akijipenda sana huku wanafunzi wengi wa kike tukiwa na mawazo ya kuwa kama yeye tukimaliza shule.

Mwalimu huyu alikuwa mrefu, mwenye mwili uliojengeka huku akiwa si mwembamba au mnene, rangi yake ni maji ya kunde, alikuwa na mwanya ambao ulionekana vizuri pale alipocheka, huku kicheko chake kilikuwa kikisubiriwa sana na wanafunzi wa darasa letu pale aingiapo darasani. Darasa letu lilijaliwa kuwa na wanafunzi wa aina zote,wapole, watulivu na watundu. Wanafunzi watundu walikuwa wakiweza kuhesabu vicheko vya mwalimu huyo kila aingiako darasani.

“Leo mwalimu wetu kacheka mara nne, jana mwalimu kacheka mara tano na juzi kacheka mara saba. Mbona leo kacheka kidogo? ” Hayo yalikuwa maneno ya kawaida mno ya wanafunzi  darasani kwetu.

Mawazo yangu ya utoto nilidhani kuwa huko Marangu wanawake wote ni warembo, lakini sijapata sijawahi kufika huko pengineni kweli na hata tulipokuwa tunacheza michezo ya kujipikilisha nyumbani, kaka yangu ambaye alikuwa pacha mwezangu alisema ataenda kuoa huko Marangu.  Namie dada mtu nililiunga mkono hilo kwa kuwa mwalimu wetu wa darasa alikuwa mfano na mwakilishi wa wanawake wote wa Kichaga. Kama ilikuwa taasisi basi ilikuwa imekamilika kila idara.

Jambo la kushangaza hata kaka yangu alipokuwa akifanya kosa darasani akichapwa na mwalimu huyu hakukasilika hata kidogo. Mimi na pacha wangu tulikuwa tunasoma darasa la tano A, mwalimu wetu mrembo akisimama mstarini tuliwaringishia wanafunzi wenzetu kuwa mnamuona mwalimu wetu! Huku wanafunzi wengine wakitamani kufundishwa na mwalimu huyu.

Siku moja tukiwa tumeshamaliza mitihani ya mwisho wa mwaka tukisubiri shule yetu kufungwa na huku walimu wa madarasa wakiwa bize wakitayarisha ripoti zetu. Walimu wengine wakitugawia mitihani yetu. Basi tulijulishwa kuwa darasa la tano A twendeni darasani tukagawiwe mitihani hiyo. Kweli tuligawiwa mitihani hiyo vizuri.Mwalimu wa kwanza alienda zake nasisi tukibaki kusubiri mwalimu mwingine aje kutugawia mitahani mingine.

Tukiwa tunacheza darasani mara binti mwezangu mmoja, nilishanga kumuona kuwa sketi yake imetapakaa damu. Niliibuka nakupiga kelele jamani njoni mumuone Kweli jambo hilo lilikuwa la hatari wanafunzi wote wakajaa.

Wakishangaa hilo huku wenginen wakilia kuwa mwezetu anaweza kupoteza uhai muda wowote ule wengine walichukua kanga na kumpatia na kasha alifika mwalimu wetu wa darasa na sote kutolewa nje.

Sisi tulikalisha katika mwembe huku akija mwalimu mwingine na kutugawia mitihani na binti mwenzetu alipelekwa nyumbani kwa mwalimu mmoja wa kike.

Baada ya muda, tukiwa katika mwembe huo niliitwa na mwalimu huyu wa darasa katika ofisi ya walimu kadhaa wa kike. Nilikaribishwa na mwalimu darasa Mchaga ninayempenda kwa bakora kadhaa ambazo sikuelewa kuwa ninachapiwa nini? Jambo hilo liliniuma sana na sana, mimi nilidhani nimefanya jambo la utu na la kiungwana kwa mwezangu aliyeumia kuwajulisha waje kumuokoa, kumbe nimefanya kosa?

Nilirudi nyumbani huku nikiwa nimekasirika mno. Tulipofika nyumbani. Baba yangu mzazi aliniuliza binti yangu mbona leo umekasirika sana kulikoni? Nilijaribu kumueleza lakini hakunielewa kwa kuwa nilikuwa na kaka yangu pacha yeye alilieleza tukio lililotokea darasani na namna wanafunzi wenzangu walivyomwaambia walimu na nilivyocharaza bakora.

Baba alisema sawa akasema kuwa anagemfuata mwalimu huyo na kumueleza juu ya tukio hilo lililotokea, hapo kidogo hasira zilipungua. Kweli baba alimueleza mwalimu huyu ambaye nilikuwa nampenda sana lakini sasa mimi nilishamchukia mno na roho yangu ilishaingia nyongo naye, hata kaka yangu pacha nikimwambia kuwa ukiwa mkubwa usiwaoe Wachaga kwa kuwa wanawachapa wanafunzi bila kosa.

Mazungumzo ya baba na mwalimu yalifanyika huku na kweli tulipofungua shule tuliingia darasa la sita na walikuja walimu maalumu kutufundisha juu ya Barehe na Kuvunja Ungo. Hapo ndipo nilipoelewa kuwa lile tukio la mimi kuwaita wenzangu kuja kushangaa lilikuwa ni kosa.Masomo yalimalizika huku hata yule dada ambaye tukio hilo lilimkuta tulikuwa marafiki mno na cha kushangaza miaka michache baada ya kumaliza shule alikuja kuolewa na binamu yangu na hivi sasa ana watoto nae watatu.

Hata ile chuki yangu ya kucharazwa viboko na Mwalimu wangu wa Kichaga ikapotea baada ya kugundua kile kilichotokea. Mwalimu huyu alikizungumza na mama kuwa huyu mwezao aliwahi kupevuka mapema kwa hiyo binti yako alikuwa mdogo hakufahamu kilichotokea tu na tulimchapa ili tukio kama hilo likitokea tena lisijirudie tena na kumuelekeza kwa wakati ule haukuwa wakati sahihi.Kweli chuki na Wachaga ikaondoka na hata kaka yangu(pacha wangu) alimuoana binti wa Kichaga wa huko Marangu sasa ni mke na mume na wana watoto wawili.

Ndugu msomaji wa matini hii haya yote niliyokusimulia ni tukio la kweli la lililomtokea mwanafunzi huko shule ya Msingi Mwambao, Bagamoyo mkoani Pwani.

Swali ni je matukio kama haya yanatokea mangapi katika shule zetu? Binti huyu alikimbizwa nyumbani kwa mwalimu, walimu wakijitolea khanga zao kuokoa jahazi hilo la binti wa kike aliyepevuka ambaye anakuja kumzaa raia wa Tanzania ambaye anaweza kuwa mwenye manufaa makubwa kwa taifa hili.

Shule hii haikuwa na chochote cha kujihifadhi kwa binti huyu. Kwa hakika suala la kupatikana kwa sodo mashuleni ni jambo la msingi nchini Tanzania. Suala la kufanyiwa hisani na walimu kutoa khanga na wanawake wengi wenye makaazi jirani na shule kuwasaidia mabinti zetu limekuwa jambo la kawaida. Sasa ni wakati sahihi jambo hili kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Panapokuwepo uhakika wa sodo salama inampa nafasi binti mwanafunzi kusoma kwa amani na huku elimu juu ya sodo kutolewa vizuri kukiwa na mazingira sahihi ya kutatua dharula kama hii mashuleni na siyo kutegemea hisani za walimu na nyumba za majirani mashuleni.

Kwa leo naweka kalamu yangu chini nakulikabidhi jambo hili kwa Ummy Mwalimu na  Joyce Ndalichako na mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Ikishaurilwa kuwa zitafutwe mashine za kutengeneza sodo ziwekwe jeshini na tena Waziri wa Ulinzi ni mwanamke Stigomena Tax, zitengenezwe na kusambazwa sodo mashuleni nchi nzima  bure.

makwadeladius@gmail.com

0717649257


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad