WATANZANIA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA UJENZI WA BOMBA LA MAFUTA UGANDA, TANZANIA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 4, 2021

WATANZANIA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA UJENZI WA BOMBA LA MAFUTA UGANDA, TANZANIA

 


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF,) Francis Nanai (katikati,) akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutoa taarifa ya mkutano maalumu utakaowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta binafsi kwa lengo la kujadili na kubainisha fursa zitokanazo na ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanzania, Leo jijini Dar es Salaam.
TAASISI ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi Uganda (PSFU,) wameandaa mkutano wa pamoja utakaofanyika Novemba 25 mwaka huu jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwakutanisha wafanyabiashara na wadau wa sekta binafsi kutoka Tanzania na Uganda na kujadili ushiriki wa sekta binafsi katika mradi mkubwa wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani Tanga nchini Tanzania pamoja na kubainisha na kujadili fursa za kiuchumi kwa wananchi wa nchi hizo kupitia mradi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaaam Mkurugenzi Mtendaji wa TPFS Francis Nanai amesema malengo ya mkutano huo ni kutengeneza jukwaa kwa ajili ya kuwakutanisha wafanyabiashara na wadau wa sekta binafsi kutoka Tanzania na Uganda na kubadilishana mawazo pamoja na kutengeneza urafiki wa biashara, uwekezaji na kubadilishana ujuzi.

Nanai amesema, katika kuiandaa jamii ya Tanzania katika kunufaika na mradi huo TPSF kwa kushirikiana na PSFU wameandaa mkutano huo maalumu kwa kujadili sekta ya mafuta na gesi jukwaa ambalo litatengeneza mtandao mkubwa baina ya mataifa hayo mawili katika kushirikishana teknolojia, biashara, uwekezaji pamoja na masuala la sera za uendeshaji wa sekta hiyo katika nchi hizo.

Amesema mradi huo wenye kilomita 1,443 utakaogharimu dola za kimarekani bilioni 15 utasafirisha mafuta kutoka Magharibi mwa Uganda mpaka Tanga Tanzania ni fursa kwa sekta binafsi katika nyanja za kiuchumi na kijamii.

''Watanzania lazima wafahamu fursa za kiuchumi ambazo zitapitiwa na mradi huu ikiwemo sekta ya usafirishaji, hoteli na malazi, ulinzi, chakula na vinywaji,rasilimali watu, vifaa vya ofisi na ujenzi, fedha na mabenki, huduma za mabenki. kukodi mitambo, mazingira, TEHAMA na afya....mradi huu utagusa kila sekta nchini tuwaombe watanzania wadau wa sekta binafsi wajiweke karibu na mradi huo wenye faida lukuki za kiuchumi.'' Amesema.

Aidha amesema, kupitia mkutano huo wanatarajia kutengeneza jukwaa la kushirikishana teknolojia, ujuzi katika sekta ya mafuta na gesi kupitia mradi huo pamoja na kujenga uhusiano imara wa sekta binafsi kwa nchi hizo.

''Baada ya mkutano huu tunategemea uelewa zaidi wa sekta binafsi kupitia mradi huu hasa katika nyanja za sheria, sera na miongozo katika mradi huu kwa nchi za Uganda na Tanzania, na uhusiano wa kampuni za sekta binafsi kutoka Tanzania na Uganda pamoja na fursa kutoka katika sekta ya mafuta na gesi na namna wananchi wake watakavyonufaika.'' Amesema.

Kwa upande wake Balozi wa Uganda nchini Tanzania Richard Kabonero amesema kuwa mkutano huo maalumu kwa sekta binafsi kutoka nchi za Uganda na Tanzania ni fursa kubwa ambayo ikitumiwa vyema italeta mageuzi makubwa ya kijamii na kiuchumi kwa mataifa hayo.

Amesema Serikali za nchi hizo mbili zinatambua mchango wa sekta binafsi na itaendelea kutoa ushirikiano na kuwashauri wazawa kutorubuniwa kwa kutoa majina yao kutumika bila kupata faida yoyote.

Balozi wa Uganda nchini Tanzania Richard Kabonero (katikati,) akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutoa taarifa ya mkutano maalumu utakaowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta binafsi kwa lengo la kuwakutanisha na kubainisha fursa zitokanazo na ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanzania, Leo jijini Dar es Salaam.
Matukio mbalimbali katika picha, leo jijini Dar es Salaam.No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad